The chat will start when you send the first message.
1“Kisha Mwenyezi-Mungu akaniambia, ‘Chonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza, na sanduku la mbao, halafu uje kwangu huku juu mlimani,[#10:1-10 Mose anapokea tena amri kumi. Habari hizi zimo pia katika Kut 34:1-10.; #10:1 Sanduku hilo liliitwa “sanduku la agano” kwa vile liliweka au kuhifadhi vile vibao viwili vya mawe vilivyoandikwa amri kumi (Kut 25:10-22). Katika aya 3 tunaambiwa kwamba sanduku hilo lilikuwa la mti wa mshita, namna ya mti mgumu zaidi kuliko msunobari au mjohoro.]
2nami nitaandika maneno yaliyokuwa yameandikwa katika vibao vile ulivyovunja, kisha viweke vibao hivyo katika sanduku’.
3“Basi, nikatengeneza sanduku la mshita na vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza, nikavitwaa mkononi, nikapanda navyo mlimani.
4Mwenyezi-Mungu akaandika katika vibao hivyo maneno yaleyale kama ya hapo awali: amri kumi ambazo aliwapeni alipoongea kutoka katika moto siku ya mkutano. Halafu Mwenyezi-Mungu akanipa vibao hivyo.[#10:4 Au, neno kwa neno, “Maneno Kumi”. Amri hizo zimehifadhiwa katika orodha mbili ambazo zinahitilafiana kidogo (taz Kut 20:1-17, na Kumb 5:6-21), nazo ni amri zinazojulikana zaidi kuliko amri na maagizo yote mengine ambayo Mwenyezi-Mungu alimpa Mose.]
5Niligeuka, nikashuka kutoka mlimani, na kama Mwenyezi-Mungu alivyoniagiza, niliviweka vibao hivyo ndani ya sanduku nililokuwa nimelitengeneza, na vimo ndani ya sanduku hilo, kama Mwenyezi-Mungu alivyoniamuru.”
6(Watu wa Israeli walisafiri kutoka visima vya watu wa Yaakani hadi Mosera. Hapo, Aroni alifariki, akazikwa. Eleazari mwanawe, akachukua nafasi yake kama kuhani.[#10:6 Majina ya vituo au miji inayotajwa hapa haijulikani ilikuwa wapi. Na kuhusu Aroni itakumbukwa kwamba yeye alikuwa ndugu yake Mose na Miriamu (hao walikuwa wa kabila la Lawi) na alikuwa kuhani mkuu wa kwanza katika Israeli (Kut 28:1-3; Lawi 8:1—9:24; Hes 18:1-20). Aroni alikufa akiwa mlimani Hori akiwa na umri wa miaka 123 (Hes 20:23-38).]
7Kutoka hapo, walisafiri hadi Gudgoda, na kutoka Gudgoda hadi Yot-batha, eneo lenye vijito vingi vya maji.
8Wakati huo, Mwenyezi-Mungu aliwateua watu wa kabila la Lawi wawe wakilibeba sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, wamtumikie kama makuhani na kubariki watu kwa jina lake hata hivi leo.[#10:8 Katika Kut 32:25-29 kuchaguliwa kabila la Lawi kwa wadhifa wa makuhani kunaonekana kufungamana na tukio la yule ndama wa dhahabu, lakini hapa kuteuliwa huko kunahusiana na aanduku la agano kwa vile Walawi ndio waliokuwa na jukumu la kulibeba na pia kuwafundisha watu juu ya amri au sheria ambayo ilikuwa imehifadhiwa humo (aya 5). Taz Hes 3:5-8; Kumb 33:8. Baadaye, ni Walawi wale tu ambao waliweza kuhakikisha kuwa wazawa wa Aroni ndio waliokuwa makuhani (Hes 18:20-32). Wengine walipewa kazi ya kulitunza hema la mkutano na kuwasaidia makuhani.]
9Ndio maana kabila la watu wa Lawi halina sehemu ya nchi ya urithi pamoja na ndugu zao; walichopokea ni heshima ya kuwa makuhani wa Mwenyezi-Mungu, kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyoahidi).[#10:9 Tofauti na makabila mengine ya Israeli, kabila la Lawi halikugawiwa eneo la ardhi ambalo watu wake wangeweza kulitumia kujipatia riziki zao za maisha. Tunaambiwa kwamba urithi wao ulikuwa Mwenyezi-Mungu mwenyewe na hivyo matoleo na zaka ambazo watu walimletea Mungu ndizo zilizokuwa riziki zao za maisha (Kumb 18:1-5; Yos 13:14).]
10“Nilikaa mlimani kwa muda wa siku arubaini, usiku na mchana, kama hapo awali. Mwenyezi-Mungu alinisikiliza kwa mara nyingine tena na akakubali kwamba hatawaangamiza.
11Kisha akaniambia ‘Ondoka uendelee na safari yako ukiwaongoza watu ili waweze kuingia na kuimiliki nchi niliyowaapia babu zenu ya kuwa nitawapa’.
12“Sasa, enyi Waisraeli, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anataka nini kwenu, ila kumcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kuzifuata njia zake zote, kumpenda, kumtumikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na kwa roho zenu zote,
13na kuzitii amri na masharti ya Mwenyezi-Mungu ninayowawekea leo, kwa manufaa yenu wenyewe?
14Tazama, mbingu hata mbingu za mbingu ni mali yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; dunia na vyote vilivyomo ni mali yake.
15Tena Mwenyezi-Mungu aliwapenda babu zenu kwa dhati, akawachagua nyinyi wazawa wao kuwa watu wake badala ya watu wengine wote, kama ilivyo hivi leo.
16Kwa hiyo, takaseni mioyo yenu, msiwe wakaidi tena.
17Maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ndiye Mungu wa miungu na Bwana wa mabwana. Yeye ni Mungu mkuu na mwenye nguvu, na wa kuogofya; hapendelei wala hapokei rushwa.
18Huwapa haki yatima na wajane; huwapenda wageni na kuwapa chakula na nguo.
19Basi, wapendeni wageni kwa kuwa nanyi pia mlikuwa wageni nchini Misri.[#10:18-19 Yatima, wajane na wageni (yaani watu wasio Waisraeli) walikuwa daima watu ambao waliathirika sana katika jumuiya na mara nyingi walitegemea wengine kwa mahitaji yao ambayo hawakuyapata kwa urahisi. Waisraeli walitakiwa kuwatendea hao kwa wema wakikumbuka kwamba Mungu aliwasaidia walipokuwa kule Misri kama wageni (10:19). Taz pia Kut 22:21-24; Lawi 19:33. Na kuhusu msimamo wa A.J. juu ya jambo hilo taz hasa Luka 4:18. Taz pia Isa 61:1-2.]
20Mcheni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; mtumikieni; ambataneni naye na kuapa kwa jina lake.
21Yeye ni fahari yenu; ndiye Mungu wenu ambaye amewatendea haya mambo makubwa na ya kutisha mliyoyaona kwa macho yenu wenyewe.
22Babu zenu walipokwenda Misri, walikuwa watu sabini tu, lakini sasa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewafanya kuwa wengi kama nyota za mbinguni.[#10:22 Taz orodha ya Mwa 46:15-27.]