The chat will start when you send the first message.
1“Ikiwa mwanamume ameoa mke na baadaye akawa hapendezwi naye kwa sababu ameona kwake kitu kisichofaa, basi, huyo mwanamume akamwandikia hati ya talaka, akampa na kumfukuza nyumbani mwake, kisha huyo mwanamke akaondoka,[#24:1-4 Katika Israeli mwanamume aliyeoa aliweza kwa urahisi kumpa mkewe talaka ingawa ilimpasa kutoa sababu. Kama huyo mwanamke aliyepewa talaka akiolewa tena, mume wake wa kwanza hawezi kumwoa tena. Labda sheria hiyo ilitolewa ili kumbana mwanamume asimpe talaka mkewe kwa sababu zisizo na maana. Taz msimamo wa A.J. katika Mat 5:31; 19:7; na Marko 10:4.]
2akaolewa na mwanamume mwingine,
3kama huyo mume wa pili akimchukua, akamwandikia hati ya talaka, akampa na kumfukuza nyumbani mwake, au kama huyo mumewe akifa,
4basi, yule mume wa kwanza haruhusiwi tena kumchukua huyo mwanamke kuwa mke wake kwa sababu alikwisha kutiwa unajisi. Kufanya hivyo ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu.
5“Mwanamume aliyeoa karibuni asiende vitani wala asipewe kazi yoyote nyingine; aachwe huru kwa muda wa mwaka mmoja, ili akae nyumbani na kufurahi na mkewe.
6“Mtu yeyote asichukue jiwe la chini au la juu la kusagia kuwa rehani; kufanya hivyo ni kama kuchukua uhai wa mtu huyo.[#24:6 Hapo kale kutengeneza unga kutoka nafaka kulifanyika kwa kusaga hiyo nafaka kwa jiwe. Kulikuwa na jiwe la chini ambalo lilikuwa kubwa kiasi, ambapo nafaka iliwekwa juu yake, kisha mtu akatumia jiwe lingine (kwa kawaida ndogo zaidi) na kupitisha juu ya hiyo nafaka na hivyo kuisaga. Huko Mashariki ya kati ya Kale karibu kila familia ilikuwa na jiwe la kusaga ili kupata unga wa kuoka mikate. Mtu aliyokopesha fedha alikatazwa kuchukua jiwe hilo kama rehani ya malipo ya mkopo. Taz pia Amo 2:6-8.]
7“Mtu yeyote akimwiba Mwisraeli mwenzake na kumfanya mtumwa wake au kumwuza utumwani, mtu huyo lazima auawe. Ndivyo mtakavyokomesha uovu miongoni mwenu.
8“Kama mtu akishikwa na ukoma mnapaswa kuwa waangalifu kufuata maagizo ya Walawi. Kama nilivyowaamuru ndivyo mtakavyofuata kwa uangalifu.[#24:8 Ugonjwa unaotajwa kama ukoma katika Biblia ulihusu hata magonjwa mengine ya ngozi ambayo sisi hatuyaiti ukoma. Taz pia Hes 5:2-4; Lawi 13:1—14:54.]
9Kumbukeni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu alivyomtendea Miriamu mlipokuwa safarini kutoka Misri.
10“Ukimkopesha jirani kitu chochote, usiingie kwake kuchukua rehani.
11Msubiri nje na umwache yeye mwenyewe akuletee hiyo rehani.
12Kama yeye ni maskini usikae na rehani hiyo usiku kucha.
13Mrudishie kila siku jioni ili usiku aweze kujifunika na kukutakia baraka. Kufanya hivyo ni jambo la uadilifu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.
14“Usimdhulumu kibarua maskini na mhitaji, awe Mwisraeli au mmoja wa wageni wanaoishi katika miji yenu.
15Kila siku, kabla jua halijakuchwa, mlipe ujira wake wa siku hiyo, maana yeye ni maskini na huo ujira ni tegemeo la moyo wake; ili asije akamlilia Mwenyezi-Mungu, nawe ukawa na hatia.[#24:14-15 Watu wengi walioajiriwa nyakati hizo walikuwa vibarua nao walitegemea sana mshahara wao wa kutwa kunua chakula chao cha siku hiyo. Taz pia Lawi 19:13.]
16“Wazazi wasiuawe kwa makosa ya watoto wao, wala watoto wasiuawe kwa ajili ya makosa ya wazazi wao. Kila mtu atauawa kwa makosa yake mwenyewe.[#24:16 Agizo hili ni kinyume cha desturi ya kale ambayo mara nyingine adhabu iliwapata hata watu wengine wa familia (Yos 7:24-25). Taz 2Fal 14:6; 2Nya 25:4; Yer 31:29-30; Eze 18:1-20.]
17“Msipotoshe haki za wageni na yatima. Wala msichukue vazi la mjane kuwa rehani.[#24:17-18 Taz 10:18-19 ambapo yahusu yatima na wajane. Taz pia Kut 23:9; Lawi 19:33-34; Kumb 27:19.]
18Kumbukeni kwamba nyinyi mlikuwa watumwa nchini Misri, na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, akawakomboa kutoka huko. Kwa hiyo ninawapeni amri hiyo.
19“Mnapovuna mavuno yenu shambani na kusahau masuke mengine humo, msirudi kuyachukua, ila waachieni wageni, yatima na wajane, ili Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu awabariki katika kazi zenu zote.[#24:19-21 Waisraeli wanaambiwa wasirudi kuokota chochote kilichobaki. Mabaki ya shambani yalitakiwa yaachwe kwa ajili ya maskini ili wao waokote, wale. Taz pia Lawi 19:9-10; 23:22; Rut 2:2-7.]
20Mkipukutisha mizeituni yenu kuvuna matunda, msirudi kupukutisha tena vitawi vyake, ila waachieni wageni, yatima na wajane.
21Mnapochuma zabibu, msirudi kuokota zabibu zilizobaki ila waachieni wageni, yatima na wajane.
22Mtakumbuka kuwa nyinyi mlikuwa watumwa nchini Misri; kwa hiyo ninawapeni amri hii.