Kumbukumbu la Sheria 26

Matoleo ya mavuno

1“Baada ya kufika na kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anawapa iwe yenu na kuishi huko,[#26:1-11 Kisehemu hiki kinashughulikia malimbuko au mavuno ya kwanza ya shambani. Kama vile wazaliwa wa kwanza, mavuno ya kwanza yalipaswa kuwekwa wakfu kwa Mungu. Matoleo ya mavuno ya kwanza (aya 2-3) katika sikukuu ya mavuno yaliandamana na kutangaza imani yao (aya 5-9) ambayo iliwakumbusha matendo makuu aliyofanya Mungu kwa jili yao tangu walipotoka Misri hadi walipoingia nchini Kanaani (taz Kumb 6:20-25; Yos 24:13). Haisemwi kama tukio hilo la kutolea mavuno ya kwanza lilifanyika kwa mwaka au kila wakati wa mavuno ya kwanza.]

2baadhi ya malimbuko ya mazao utakayovuna katika nchi anayokupa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, utayachukua katika kikapu mpaka pale mahali ambapo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amepachagua pawe makao yake.

3Utamwendea kuhani anayehudumu wakati huo, na kumwambia, ‘Leo ninakiri mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, kuwa nimeingia katika nchi aliyowaapia wazee wetu kuwa atatupa.’[#26:3 Makuhani wa Waisraeli walikuwa na majukumu ya kumtolea Mwenyezi-Mungu tambiko zifaazo na kuwafundisha watu juu ya mambo yaliyo safi na yaliyo najisi kidini.]

4“Naye kuhani atakapochukua kikapu hicho mikononi mwako na kukiweka mbele ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako,

5utatamka maneno haya mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako: ‘Baba yangu alikuwa Mwaramu aliyetangatanga huko na huko, kisha akashuka kwenda Misri akaishi huko kama mgeni. Yeye na jamaa yake walikuwa watu wachache tu walipokuwa huko, lakini wakawa taifa kubwa lenye nguvu na watu wengi.[#26:5 Hapa mwandishi anasema juu ya babu wa Waisraeli, yaani Yakobo, ambaye alitangatana kutoka Kanaani hadi Harani na kurudi tena Kanaani (Mwa 27-35) kisha akaenda Misri (Mwa 46:3-7). Alipokuwa Misri, jamaa yake iliongezeka hata wakawa taifa kubwa (Kut 1:1-7).]

6Wamisri walitutendea kwa ukatili wakatutesa na kutulazimisha kufanya kazi ngumu ya watumwa.

7Kisha tukamlilia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wetu, akasikia kilio chetu, na kuyaona mateso yetu, kazi ngumu na dhuluma tulizozipata.

8Basi, Mwenyezi-Mungu akatutoa huko Misri kwa mkono wake wa nguvu ulionyoshwa, kwa vitisho, ishara na maajabu.

9Alituleta hapa na kutupatia nchi hii inayotiririka maziwa na asali.

10Na sasa ninamletea Mwenyezi-Mungu malimbuko ya mazao ya nchi ambayo amenipa.’

“Kisha utaweka kikapu chini, mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, na kuabudu mbele zake.

11Nawe utafurahia mema yote ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, amekujalia wewe na jamaa yako. Nao watafurahi pamoja nawe.

12Kila baada ya miaka mitatu, kila mmoja wenu atatoa sehemu moja ya kumi ya mazao yake yote kwa ajili ya Walawi na wageni, yatima na wajane, ili wapate chakula chote wanachohitaji wanapokuwa katika miji yenu.[#26:12 Si dhahiri miaka hiyo ilihesabiwa namna gani. Wengi wanafikiri ilikuwa ni mwaka wa tatu na wa sita katika mzunguko wa miaka saba (Kumb 16:1-7).; #26:12 Neno linalotafsiriwa kama zaka hapa ni sawa na lile linalotajwa kama moja ya kumi au asilimia kumi ya mapato ya mtu ambayo Waisraeli walitakiwa kumtolea Mungu itumike kama riziki ya Walawi kwani hao hawakuwa na mashamba kama watu wa makabila mengine ya Waisraeli (taz Lawi 27:30; Hes 18:20; 24; Kumb 14:23-29). Zaka hiyo iliwafaa pia wasiobahatika kama vile yatima, wajane na wageni walioishi miongoni mwao.]

13Kisha utasema mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, hivi: ‘Nimelitoa nyumbani kwangu fungu takatifu, nikawapa Walawi, wageni, yatima na wajane, kama ulivyoniamuru nifanye. Sijavunja amri zako wala sijasahau.

14Sikula zaka yoyote nilipokuwa ninaomboleza; sikuitoa nje ya nyumba yangu nilipokuwa najisi na sikutoa zaka hiyo kwa wafu. Nimekutii ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu; nimefanya kila kitu ulichoamuru.[#26:14 Mambo yanayotajwa hapa: kutambika chakula na kwa jumla ibada kwa wale waliokufa ni desturi ambazo zimetapakaa karibu katika tamaduni zote ulimwenguni. Rejea k.m. Kumb 18:11; 1Sam 28:3-24.]

15Uangalie chini kutoka makao yako matakatifu mbinguni, uwabariki watu wako Israeli na nchi uliyotupatia kama ulivyowaapia wazee wetu; nchi inayotiririka maziwa na asali.’

Watu wa Mwenyezi-Mungu

16“Leo hii, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anawaamuru kuyashika masharti na maagizo haya. Muwe waangalifu kuyatekeleza kwa moyo wote na roho yote.

17Leo hii mmekiri Mwenyezi-Mungu, kuwa Mungu wenu, na kwamba mtafuata njia zake na kushika masharti, amri zake na maagizo yake na kutii sauti yake.

18Naye Mwenyezi-Mungu ametamka rasmi leo hii kwamba nyinyi ni watu wake yeye mwenyewe kama alivyowaahidi na kwamba mnatakiwa kushika amri zake zote.[#26:16-18 Kisehemu hiki kinamalizia sehemu iliyoanza na sura 12 (linganisha 12:1 na 26:16), sehemu ambayo inasisitiza sana kutii sheria ya Mungu na kwamba taifa la Israeli ni mali yake Mwenyezi-Mungu. Kinachosemwa katika aya 17-18 kinahusu watu wa Israeli: ninyi mmekiri Mwenyezi-Mungu kuwa Mungu wenu (aya 17), na kwa upande mwingine Mwenyezi-Mungu anawafanya Waisraeli kuwa watu walio mali yake mwenyewe (aya 18). Kwa hiyo, lile agano au mkataba kati ya Mungu na watu wa Israeli umeratibishwa. Rejea Kut 24:7. Kutokana na hayo watu watatii maagizo na masharti ya Mungu siyo kwa sababu ni wajibu bali matokeo ya upendo na baraka walizopata kutoka kwake. Katika 27:9 Mose anawatangazia watu kwamba wamekuwa watu wake Mwenyezi-Mungu.]

19Atawafanyieni nyinyi kuwa taifa kubwa kuliko mataifa yote aliyoyaumba. Nanyi mtalitetea jina lake, sifa yake na heshima yake. Nyinyi mtakuwa watu wake, walio mali yake, kama alivyoahidi.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania