Waefeso 5

Waefeso 5

Kuishi katika mwanga

1Kwa hiyo, mwigeni Mungu, maana nyinyi ni watoto wake wapenzi.[#5:1 Mat 5:48. “Mwigeni Mungu”, yamkini katika kusamehe (4:32) na kupenda (5:2).]

2Upendo uongoze maisha yenu kama vile Kristo alivyotupenda, na kwa ajili yetu akajitoa mwenyewe kama tambiko yenye harufu nzuri na sadaka impendezayo Mungu.[#5:2 Maneno ya sehemu ya pili ya aya hii yanagusia kifo cha Yesu Kristo kwa kutumia maneno yaleyale yaliyotumiwa katika A.K. kuhusu kafara; rejea Kut 29:18 na pia taz Fil 4:18; Ebr 10:10.]

3Kwa vile nyinyi ni watu wa Mungu, basi uasherati, uchafu wowote ule au choyo visitajwe kamwe miongoni mwenu.[#5:3 Aya hii karibu ni sambamba na Kol 3:5 ambapo pia vitendo hivyo vitatu visivyofaa vinatajwa.]

4Tena maneno ya aibu, ya upuuzi au ubishi, yote hayo hayafai kwenu; maneno ya kumshukuru Mungu ndiyo yanayofaa.

5Jueni wazi kwamba mwasherati yeyote au mchafu au mchoyo, (ambao ni sawa na kuabudu sanamu), au mtu yeyote wa aina hiyo hataambulia chochote katika ufalme wa Kristo na wa Mungu.[#5:5 Kol 3:5. Mwandishi anaona ulafi ni sawa na kuabudu sanamu kwa vile mtu mlafi nafasi ya Mungu imechukuliwa na hivyo vitu anavyotamani kujishibisha navyo.]

6Msikubali kudanganywa na mtu kwa maneno matupu; maana, kwa sababu ya mambo kama hayo ghadhabu ya Mungu huwajia wote wasiomtii.

7Basi, msishirikiane nao.

8Zamani nyinyi mlikuwa gizani, lakini sasa nyinyi mko katika mwanga kwa kuungana na Bwana. Ishini kama watoto wa mwanga,[#5:8 Yoh 12:35 maelezo.]

9maana matokeo ya mwanga ni wema kamili, uadilifu na ukweli.[#5:9 Baadhi ya hati za kale zina “matokeo ya Roho”.]

10Jaribuni kujua yale yanayompendeza Bwana.

11Msishiriki katika matendo yasiyofaa ya giza, bali yafichueni.

12Mambo yanayotendwa kwa siri ni aibu hata kuyataja.

13Lakini kila kitu kikifichuliwa na mwanga, ukweli wake hudhihirishwa;

14na kila kilichodhihirishwa huwa mwanga. Ndiyo maana Maandiko yasema:

“Amka wewe uliyelala,

fufuka kutoka kwa wafu,

naye Kristo atakuangaza.”

15Basi, muwe waangalifu jinsi mnavyoishi. Msiishi kama wapumbavu, bali kama wenye hekima.

16Tumieni vizuri muda mlio nao maana siku hizi ni mbaya.

17Kwa hiyo, msiwe wapumbavu, bali jaribuni kujua matakwa ya Bwana.

18Acheni kulewa divai maana hiyo itawaangamiza, bali mjazwe Roho Mtakatifu.

19Zungumzeni kwa maneno ya Zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Bwana nyimbo na Zaburi kwa shukrani mioyoni mwenu.

20Mshukuruni Mungu Baba daima kwa ajili ya yote, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo.

Wake na waume

21Kila mmoja amstahi mwenzake kwa sababu ya heshima mliyo nayo kwa Kristo.[#5:21—6:9 Kol 3:18—4:1; 1Pet 2:18-37. Kuanzia 5:21 mpaka 6:9 mwandishi anazungumzia juu ya uhusiano katika familia ya Kikristo: wake na waume (6:5-9); watoto na wazazi (6:1-4); watumwa na mabwana zao (6:5-9). Ni dhahiri kwamba yanayosemwa yanaendana na desturi za wakati huo lakini yamebadilishwa kiasi fulani kutokana na fikra za Kikristo.; #5:21 Kinachosemwa katika aya hii ni muhimu kwa uhusiano wote utakaotajwa katika 5:21—6:9. Muungano kati ya Kristo na Kanisa lake unaipa jumuiya yote ya Wakristo mtazamo mpya kuhusu uhusiano uliopo kati ya tabaka mbalimbali. Katika tafsiri hii, kitenzi “kustahi” yaani kuheshimu, kimetumika kutafsiri neno la Kigiriki ambalo lina maana ya kujiweka chini ya mtu fulani, kumfikiria yeye kwanza. Tafsiri nyingine za Kiswahili zina: Kunyenyekeana.]

22Wake wawatii waume zao kama kumtii Bwana.

23Maana mume anayo mamlaka juu ya mkewe, kama vile Kristo alivyo na mamlaka juu ya kanisa; naye Kristo mwenyewe hulikomboa kanisa, mwili wake.[#5:23-24 Rejea 1Kor 11:3. Hapa picha ya Kanisa kama mwili ambao kichwa chake ni Kristo inatumika pamoja na picha ya Kanisa kama mchumba wa Kristo (rejea aya 23-33). Uhusiano wa Kristo na Kanisa unachukuliwa kama kielelezo kizuri cha uhusiano kati ya mke na mume (aya 25-29). Zaidi ya hayo, inaonekana kwamba mwandishi anataka kuwawekea wafuasi wa Yesu picha ile ile ya Yesu ya kujitoa kwa ajili yao ili iwe ni mwongozo wa uhusiano miongoni mwao.]

24Kama vile kanisa linavyomtii Kristo, vivyo hivyo, wake wawatii waume zao katika mambo yote.

25Nanyi waume, wapendeni wake zenu kama Kristo alivyolipenda kanisa, akajitoa mwenyewe sadaka kwa ajili yake.

26Alifanya hivyo ili kwa neno lake, aliweke wakfu kwa Mungu, baada ya kulifanya safi kwa kuliosha katika maji,[#5:26 Hapa kuna matumizi ya maneno ambayo ni vigumu kufuata. Kadiri ya wafafanuzi wa Maandiko kuna matumizi ya mfano kutokana na desturi ya huko Mashariki ya Kati wakati huo ambapo bibi arusi alifanywa safi kwa ajili ya bwana arusi. Kwa hivyo maneno “baada ya kulifanya safi kwa kuliosha katika maji” ni maneno ya kimfano, kuonesha jinsi Yesu anavyoliweka wakfu kanisa lake na kulitakasa kwa neno lake (rejea Yoh 15:3). Taz pia Tito 3:5; 1Pet 3:21.]

27kusudi ajipatie kanisa lililo takatifu na safi kabisa, kanisa lisilo na doa, kasoro au chochote cha namna hiyo.

28Basi, waume wanapaswa kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. (

29Hakuna mtu yeyote auchukiaye mwili wake; badala ya kuuchukia, huulisha na kuuvika. Ndivyo naye Kristo anavyolitunza kanisa,

30maana sisi ni viungo vya mwili wake).

31“Kwa sababu hiyo, mwanamume atamwacha baba yake na mama yake, ataungana na mkewe, nao wawili watakuwa mwili mmoja.”

32Kuna ukweli uliofichika katika maneno haya, nami naona kwamba yamhusu Kristo na kanisa lake.

33Lakini yanawahusu nyinyi pia: kila mume lazima ampende mkewe kama nafsi yake mwenyewe, naye mke anapaswa kumstahi mumewe.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania