Waefeso 6

Waefeso 6

Watoto na wazazi wao

1Enyi watoto, watiini wazazi wenu Kikristo maana hili ni jambo jema.

2“Waheshimu Baba na mama yako,” hii ndiyo amri ya kwanza ambayo imeongezewa ahadi, yaani,

3“Upate fanaka na kuishi miaka mingi duniani.”

4Nanyi akina baba, msiwachukize watoto wenu ila waleeni katika nidhamu na mafundisho ya Kikristo.[#6:4 Kol 3:21]

Watumwa na wakuu wao

5Enyi watumwa, watiini mabwana zenu hapa duniani kwa hofu na kutetemeka; fanyeni hivyo kwa unyofu wa moyo kana kwamba mnamtumikia Kristo.[#6:5 Maneno yanayotumika katika Biblia kwa maana ya kuwa na uangalifu au bidii; rejea 2Kor 7:15; Fil 2:12.]

6Fanyeni hivyo si tu wakati wanapowatazama ili mjipendekeze kwao, bali tumikieni kwa moyo kama atakavyo Mungu kwa sababu nyinyi ni watumishi wa Kristo.

7Muwe radhi kutumikia kwa ajili ya Bwana na si kwa ajili ya watu.

8Kumbukeni kwamba kila mtu mwenye kutenda mema, awe mtumwa au mtu huru, atapokea tuzo lake kutoka kwa Bwana.

9Nanyi mnaotumikiwa, watendeeni vivyo hivyo watumwa wenu, na acheni kutumia vitisho. Kumbukeni kwamba nyinyi pia kama vile wao, mnaye Bwana yuleyule mbinguni, naye hatendi kwa ubaguzi.[#6:9 Kumb 10:17; Mate 10:34; Rom 2:11; Kol 3:25. Katika jamii za kale na hata nyakati za A.J. watumwa hawakuwa na hadhi yoyote katika jumuiya; lakini kwa vile Kikristo wote ni sawa mbele ya Mungu na kwa kuwa Wakristo wote ni watumishi (au watumwa) wa Kristo (aya ya 6), Paulo anawahimiza wanaotumikiwa na watumwa wawatendee hao watumwa kwa haki. Taz Kol 3:22 maelezo.]

Vita vya kiroho

10Hatimaye, nawatakeni muwe imara katika kuungana na Bwana na kwa msaada wa nguvu yake kuu.[#6:10-20 Sehemu hii ya mwisho kabla ya salamu za mwisho katika 6:21-22, inahusu maisha ya Kikristo ambayo yanaelezwa kwa kutumia picha ya vita ambavyo kila Mkristo anapaswa kujiandaa kwavyo na kuwa tayari. Maelezo ya silaha za Kikristo yanatolewa katika aya 11 mpaka 17, hali katika 18 mpaka 20 Mwandishi anazungumzia juu ya sala kwa ajili ya watu wote wa Mungu na kwa ajili yake mwenyewe.]

11Vaeni silaha anazowapeni Mungu mpate kuzipinga mbinu mbaya za Ibilisi.[#6:11 2Kor 10:4; 1Pet 4:1; taz 1Tim 1:18-20 maelezo. Picha ya silaha hapa imechukuliwa kutoka silaha za Waroma wa nyakati hizo. Hapa, Mungu ndiye anayewagawia Wakristo silaha hizo. Rejea pia Rom 13:12; 1Thes 5:8. Tafsiri hii, kwa namna ilivyowekwa, inaonesha kwamba vita vya Mkristo ni dhidi ya jeshi ovu (au pepo wabaya) la mbingu ambalo ndio hao wanaoitwa pia kwa majina matatu: watawala, wakuu, na wenye nguvu (taz Efe 1:21-22 maelezo). Na kuhusu “mbingu”, taz 1:3 maelezo.]

12Maana vita vyetu si vita kati yetu na binadamu, bali ni vita dhidi ya jeshi ovu la ulimwengu wa roho; tunapigana na watawala, wakuu na wenye nguvu, wanaomiliki ulimwengu huu wa giza.

13Kwa sababu hiyo, vaeni silaha za Mungu ili siku ile itakapofika mweze kuyapinga mashambulio ya adui; na mkisha pigana mpaka mwisho, mtakuwa bado imara.

14Basi, kaeni tayari. Ukweli na uwe kama mkanda kiunoni mwenu, uadilifu uwe kama vazi la kujikinga kifuani,[#6:14 Yobu 29:14; Isa 59:17; rejea 1Thes 5:8. Matumizi ya mkanda wa kujifunga kiunoni hapa ni picha ya askari aliye tayari kabisa na kwa Mkristo mkanda huo ni ishara ya ukweli.]

15na hamu ya kutangaza Habari Njema ya amani iwe kama viatu miguuni mwenu.[#6:15 Isa 52:7; Rom 10:15. Askari wa Kiroma alivaa viatu vya buti ambavyo viliimarisha miguu alipotembea. Picha hiyo Mwandishi anaitumia kwa kusema kwamba Habari Njema ya Kristo ndiyo itakayowaimarisha Wakristo katika vita hivyo na hawatalegealegea. Kutokana na picha hiyo, yawezekana kutafsiri: “Mjiweke tayari na kuwa imara katika kutangaza Habari Njema”.]

16Zaidi ya hayo yote, imani iwe daima kama ngao mikononi mwenu, iwawezeshe kuizima mishale ya moto ya yule Mwovu.

17Upokeeni wokovu kama kofia yenu ya chuma, na neno la Mungu kama upanga mnaopewa na Roho Mtakatifu.[#6:17 Isa 59:17; 1Thes 5:8.]

18Salini daima, mkiomba msaada wa Mungu. Salini kila wakati kwa nguvu ya Roho. Kesheni bila kuchoka mkisali kwa ajili ya watu wote wa Mungu.

19Niombeeni nami pia ili niongeapo Mungu anijalie cha kusema, niweze kuwajulisha watu fumbo la Injili kwa uthabiti.[#6:19 Au “siri”. Taz Efe 1:9 maelezo.]

20Mimi ni balozi kwa ajili ya Injili hiyo ingawa sasa niko kifungoni. Ombeni, basi, ili niweze kuwa hodari katika kuitangaza kama inipasavyo.

Salamu za mwisho

21Tukiko, ndugu yetu mpenzi na mtumishi mwaminifu katika kuungana na Bwana, atawapeni habari zangu zote mpate kujua ninachofanya.[#6:21 Mate 20:4; 2Tim 4:12; Tito 3:12; taz Kol 4:7 maelezo.]

22Namtuma kwenu awapeni habari zetu mpate kuwa na moyo.

23Ninawatakieni nyinyi ndugu amani, upendo na imani kutoka kwa Mungu Baba na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo.

24Nawatakia neema ya Mungu wote wanaompenda Bwana wetu Yesu Kristo kwa mapendo yasiyo na mwisho.[#6:24 Hati nyingine za kale zina neno “Amina” mwishoni mwa barua hii.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania