The chat will start when you send the first message.
1Siku hiyohiyo, mfalme Ahasuero alimkabidhi malkia Esta mali yote ya Hamani, adui ya Wayahudi. Esta akamjulisha mfalme kwamba Mordekai ni jamaa yake. Basi, tangu wakati huo, Mordekai akaruhusiwa kumwona mfalme.
2Mfalme akaivua pete yake ya mhuri aliyokuwa amemnyang'anya Hamani, akampa Mordekai. Esta naye akampa Mordekai mamlaka juu ya mali ya Hamani.
3Kisha Esta akazungumza tena na mfalme; akajitupa chini, miguuni pa mfalme, huku analia, akamsihi mfalme aukomeshe mpango mbaya ambao Hamani, wa uzao wa Agagi, alikuwa amepanga dhidi ya Wayahudi.
4Mfalme akamnyoshea Esta fimbo yake ya dhahabu, naye Esta akasimama na kusema,
5“Ukipenda, ewe mfalme, na kama unanijali na ukiona inafaa, tafadhali, toa tangazo la kufutilia mbali mipango ambayo Hamani alikuwa ameamuru itekelezwe. Mipango hiyo ni ile ya mwana wa Hamedatha, mzaliwa wa Agagi, aliyopanga ili kuwaangamiza Wayahudi wote katika mikoa yote.
6Maana, ninawezaje kuvumilia kuona watu wangu wanaangamizwa na jamaa zangu wanauawa?”
7Mfalme Ahasuero akawaambia malkia Esta na Mordekai, yule Myahudi, “Tazameni! Nimempa Esta mali yake Hamani, naye wamekwisha mnyonga kwa sababu ya njama zake dhidi ya Wayahudi.[#8:7-8 Sasa kwa vile mfalme hangeweza yeye mwenyewe kutangua agizo lililotolewa la kuwaangamiza Wayahudi, anawapa uwezo Mordekai na Esta wa kuandika agizo lingine la kubatilisha lile la kwanza.]
8Mwaweza kuwaandikia Wayahudi lolote mpendalo. Tena mwaweza kuandika kwa jina langu na kutumia mhuri wa kifalme, kwa sababu tangazo ambalo limetolewa kwa jina la mfalme na kupigwa mhuri wa mfalme, haliwezi kubatilishwa.”
9Basi, mnamo siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa tatu uitwao Siwani, Mordekai aliwaita makatibu wote wa mfalme, akawaagiza waandike barua kwa Wayahudi na wakuu, watawala na maofisa wa mikoa yote 127, kuanzia India mpaka Kushi. Nyaraka hizo ziliandikwa kwa kila mkoa katika lugha yake na hati yake ya maandishi, hali kadhalika kwa Wayahudi.
10Mordekai alikuwa ameandika nyaraka hizo kwa jina la mfalme Ahasuero, akazipiga mhuri kwa pete ya mfalme. Na waliozipeleka walikuwa matarishi waliopanda farasi wenye nguvu waendao kasi.
11Kwa njia ya nyaraka hizi mfalme aliwaruhusu Wayahudi katika kila mji kukusanyika ili kuyalinda maisha yao. Walikuwa na ruhusa ya kuharibu, kuua bila huruma na kuangamiza kundi lolote la watu au mkoa, lenye kuwashambulia kwa silaha pamoja na wanawake na watoto wao, na kuziteka nyara mali zao.
12Jambo hili lingefanyika katika mikoa yote ya mfalme Ahasuero, mnamo siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, yaani Adari.[#8:11-12 Tarehe hiyo ni sawa na siku moja kabla ya kutekelezwa yale maangamizi dhidi ya Wayahudi (taz 3:7; B:6).]