Kutoka 18

Kutoka 18

Yethro anamtembelea Mose

(Kumb 1:9-18)

1Yethro, kuhani wa Midiani, baba mkwe wa Mose, alisikia juu ya mambo yote ambayo Mwenyezi-Mungu alimtendea Mose na Waisraeli alipowatoa katika nchi ya Misri.

2Kwa hiyo Yethro, akiwa na Sipora, mkewe Mose, ambaye Mose alikuwa amemrudisha kwa baba yake, alimwendea Mose,

3pamoja na watoto wawili wa Mose. Mtoto wa kwanza aliitwa Gershomu. Mose alimpa jina hili kwa vile alisema, “Nimekimbilia katika nchi ya kigeni.”[#18:2-3 Inaonekana kwamba wakati Mose alipokwenda Misri kukabiliana na Farao aliiacha familia yake chini ya ulinzi wa babamkwe wake, Yethro; na sasa, baada ya matatizo ya Misri kupita, Yethro anamkabidhi tena hao watoto wake (aya 5). Kuhusu jina “Gershomu” taz Kut 2:22.]

4Wa pili aliitwa Eliezeri, kwa vile Mose alisema, “Mungu wa baba yangu ndiye aliyenisaidia nisiuawe na Farao.”[#18:4 Kiebrania “Eli” maana yake “Mungu wangu” na “ezer”, maana yake “msaada”; kwa hiyo jina lote lina maana ya “Mungu wangu ni msaada wangu”.]

5Yethro, mkwewe Mose, alikuja pamoja na binti yake, yaani mkewe Mose, pamoja na watoto, akamkuta Mose jangwani alikokuwa amepiga kambi kwenye mlima wa Mungu.[#18:5 Yaani, Zipora (taz 2:15-22).; #18:5 Yaani, Gershomu (taz 2:22) na Eliezeri (taz 18:4).; #18:5 Yaani, Sinai au Horebu. Taz Kut 3:1 maelezo.]

6Mose alipoambiwa kuwa baba mkwe wake pamoja na mkewe na wanawe wawili wanakuja,

7alitoka kwenda kumlaki baba mkwe wake, akamwinamia na kumbusu. Wakasalimiana, kisha wakaingia hemani.[#18:7 Katika Mashariki ya Kati ya Kale, kama ilivyo katika jamii nyingi hapa Afrika, watu walikuwa na desturi zao za kuonesha heshima: mtu akikutana na fulani ambaye anampita kwa umri, au mfalme au mtu mwenye madaraka, n.k., ilimbidi amsalimu kwa kuinama.]

8Mose akamweleza mkwewe mambo yote Mwenyezi-Mungu aliyomtenda Farao na Wamisri kwa ajili ya Waisraeli. Alimwambia pia juu ya shida zote zilizowapata safarini na jinsi Mwenyezi-Mungu alivyowaokoa.

9Yethro akafurahishwa na yote aliyotenda Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya Waisraeli, kwa kuwaokoa mikononi mwa Wamisri.

10Yethro akasema, “Na atukuzwe Mwenyezi-Mungu ambaye amewaokoa mikononi mwa Wamisri na kutoka utumwa wa Farao.

11Sasa najua kwamba Mwenyezi-Mungu ni mkuu kuliko miungu yote, kwani amewakomboa watu hawa mikononi mwa Wamisri ambao waliwatendea ujeuri.”

12Hapo Yethro, baba mkwe wa Mose, akamtolea Mungu sadaka za kuteketezwa na tambiko. Naye Aroni akaja pamoja na wazee wa Israeli ili kula chakula pamoja na Yethro, mbele ya Mwenyezi-Mungu.[#18:12 Inaonekana kwamba Waisraeli na watu wa huko Media, eneo la Afrika kaskazini na sehemu ya Uarabuni hawakuwa tu na uhusiano wa kitamaduni (taz k.m. harusi ya Mose Kut 2:21), bali walikuwa pia na uhusiano wa kidini. Hapa Yethro anamshirikisha Mose katika karamu ya kafara ambayo alimtambikia Mungu. Suala gumu hapa ni kwamba alikuwa “Mungu” yupi kwa vile Yethro hakuwa Mwisraeli. Mungu anayetajwa hapa yaelekea ni Mwenyezi-Mungu. Sadaka hapa yawezekana ni ya wanyama ambao waliteketezwa kwa moto. (Ling 20:24; Lawi 12:6,8).]

Kuteuliwa kwa waamuzi

(Kumb 1:9-18)

13Kesho yake, Mose aliketi kuamua matatizo ya Waisraeli, nao wakasimama wakiwa wamemzunguka, tangu asubuhi mpaka jioni.[#18:13 Katika Mashariki ya Kati ya Kale ilikuwa kawaida kwa yeyote aliyefanya kazi kama hakimu kukaa anapoamua mashauri. (Ling 1Fal 1:30,35,37,47; Zab 93:2; 82:1; Isa 6:1; Ufu 5:11).]

14Yethro, baba mkwe wa Mose, alipoyaona mambo yote ambayo Mose aliwafanyia Waisraeli, alimwuliza, “Kwa nini unawafanyia watu mambo haya? Mbona unaketi peke yako huku watu wamekuzunguka tangu asubuhi mpaka jioni?”

15Mose akamjibu mkwewe, “Kwa sababu watu huja kwangu kuuliza matakwa ya Mungu.

16Wakiwa na ugomvi wowote ule wao huja kwangu nami huamua kati ya mtu na mwenzake, na kuwafunza amri za Mungu na maamuzi yake.”

17Basi, Yethro akamwambia Mose, “Unavyofanya si vizuri!

18Utajidhuru mwenyewe na hawa watu kwa uchovu, kwani hii ni kazi ngumu usiyoweza kuifanya peke yako.

19Sikiliza shauri langu kwako, na Mungu awe pamoja nawe. Wewe utawawakilisha watu mbele ya Mungu na kumletea Mungu matatizo yao.

20Hali kadhalika utawafundisha amri na maamuzi ya Mungu na kuwaonesha jinsi inavyowapasa kuishi na kufanya.

21Lakini kuhusu mambo mengine, chagua miongoni mwa watu wote, watu wanaostahili, watu wanaomcha Mungu, waaminifu na wanaochukia kuhongwa. Wape hao mamlaka, wawe na jukumu la kuwasimamia watu katika makundi ya watu elfu, mia, hamsini na kumikumi.[#18:21 Tafsiri nyingine: Walio na uwezo au wazoefu. Jambo la kuwa na viongozi wanaofaa ni jambo muhimu katika Biblia hata kuanzia wakati huo wa kale, na uovu wa viongozi walanguzi na wapotovu ulikemewa na Mungu kwa njia ya manabii wake (taz 23:6-8; Kumb 10:17; 16:19; Isa 33:15; Eze 16:33; 22:12; Amo 5:12; Mika 3:11; 7:3).]

22Hao ndio watakaokuwa na vikao kila siku kutatua matatizo ya watu. Matatizo magumu watakuletea wewe, lakini yale madogomadogo watayaamua wenyewe. Kwa njia hiyo utaweza kurahisisha kazi yako kwa vile watashirikiana nawe katika jukumu hilo.

23Ukifanya hivyo, na kama ndivyo atakavyo Mungu, utaweza kustahimili na watu hawa wote wataweza kurudi makwao kwa amani.”

24Mose alilisikiliza shauri hilo la mkwewe na kufanya kama alivyoshauriwa.

25Basi, akawateua watu wenye uwezo kati ya Waisraeli, akawafanya kuwa viongozi wa makundi ya watu elfu, watu mia, watu hamsini na watu kumikumi.

26Nao wakawa wanaamua matatizo ya watu kila wakati. Matatizo magumu walimletea Mose, lakini yale madogomadogo waliyatatua wao wenyewe.

27Baada ya kufanya hivyo, Mose na mkwewe wakaagana naye Yethro akarudi nchini kwake.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania