The chat will start when you send the first message.
1Agano la kwanza lilikuwa na taratibu zake za ibada na maskani takatifu ya duniani.
2Palitengenezwa hema ambayo sehemu yake ya nje iliitwa Mahali Patakatifu. Humo mlikuwa na kinara cha taa, meza na mikate iliyowekwa mbele ya Mungu.[#9:2 Yaani hema ya mkutano kule jangwani. (Tazama Ebr 8:2 na rejea maelezo katika Kut 26:1-36).; #9:2 Kut 25:31-40.; #9:2 Kut 25:23-30]
3Nyuma ya pazia la pili, kulikuwa na hema iliyoitwa Mahali Patakatifu sana.
4Humo mlikuwa na madhabahu ya dhahabu kwa ajili ya kufukizia ubani, na sanduku la agano, ambalo lilikuwa limepakwa dhahabu pande zote, na ndani yake mlikuwa na chungu cha dhahabu kilichokuwa na mana, fimbo ya Aroni iliyokuwa imechanua majani, na vile vibao viwili vya mawe vilivyoandikwa agano.[#9:4 Kut 25:10-16.; #9:4 Kut 16:33.; #9:4 Hes 17:8-10.; #9:4 Kut 25:16; Kumb 10:3-5.]
5Juu ya hilo sanduku kulikuwa na viumbe wenye mabawa, na mabawa yao yalitanda juu ya kiti cha rehema. Lakini sasa hatuwezi kusema kinaganaga juu ya mambo hayo.[#9:5 Au, neno kwa neno: Kerubimu. Picha za viumbe wenye mabawa ambao hapa walitumika kama walinzi (Kut 25:18). Rejea Mwa 3:24; 1Fal 6:23-29; Zab 18:10.; #9:5 Tafsiri nyingine: “Mahali ambapo dhambi huondolewa”. Kut 25:17-22; taz Rom 3:25 maelezo.]
6Mipango hiyo ilitekelezwa, kisha ikawa desturi kwa makuhani kuingia kila siku katika hema ya nje kutoa huduma zao.
7Lakini kuhani mkuu peke yake ndiye anayeingia katika lile hema la pili; naye hufanya hivyo mara moja tu kwa mwaka, na huwa amechukua damu ambayo anamtolea Mungu kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya makosa ya watu.[#9:7 Yahusu ibada ya Siku ya Msamaha au Siku ya Malipizi ambayo yaelezwa kinaganaga katika Lawi 16.]
8Kutokana na taratibu hizo Roho Mtakatifu anafundisha wazi kwamba wakati ile hema ya nje ingali ipo imesimama, njia ya kuingia Mahali Patakatifu sana haijafunguliwa.
9Jambo hili ni mfano wa nyakati za sasa, ambapo zawadi na tambiko zinatolewa lakini haziwezi kuifanya dhamiri za wanaoabudu kuwa kamilifu,
10kwani haya yote yanahusika na vyakula, vinywaji na taratibu mbalimbali za kutawadha. Yote hayo ni maagizo ya njenje tu; na nguvu yake hukoma wakati Mungu atakaporekebisha vitu vyote.
11Lakini Kristo amekwisha fika, akiwa kuhani mkuu wa mambo yaliyo mema, ambayo sasa yamekwisha fika. Yeye anatoa huduma zake katika hema iliyo bora na kamilifu zaidi, isiyofanywa kwa mikono ya watu, yaani isiyo ya ulimwengu huu ulioumbwa.
12Yeye aliingia Mahali Patakatifu mara moja tu, akiwa amechukua, sio damu ya mbuzi na ng'ombe, bali amechukua damu yake yeye mwenyewe, akatupatia ukombozi wa milele.
13Watu waliokuwa najisi kidini waliweza kutakasika na kuwa safi waliponyunyiziwa damu ya mbuzi na ya ng'ombe pamoja na majivu ya ndama.[#9:13 Lawi 16:15-16.; #9:13 Hes 19:9,17-19.]
14Lakini, kwa damu ya Kristo, mambo makuu zaidi hufanyika! Kwa nguvu ya Roho wa milele, Kristo alijitolea mwenyewe tambiko kamilifu kwa Mungu. Damu yake itatutakasa dhamiri zetu kutokana na matendo yaletayo kifo, ili tupate kumtumikia Mungu aliye hai.[#9:14 Hes 28:3; 1Pet 1:18-19.; #9:14 1Yoh 1:7; Ufu 1:5; 7:14.]
15Hivyo yeye ni mpatanishi wa agano jipya ambamo wale walioitwa na Mungu wanaweza kupokea baraka za milele walizoahidiwa. Kifo chake huwakomboa watu kutoka yale makosa waliyofanya wakati wa lile agano la kale.[#9:15 Taz Ebr 8:6 maelezo. Neno “Agano” na “Wosia” katika aya ifuatayo (16) ni tafsiri ya neno lile lile la Kigiriki; katika aya 15-20 mwandishi anachukua fursa ya maana hizo mbili (wosia ukiwa unahusu kifo) kuonesha kwamba wokovu sasa unapatikana kwa sababu ya kifo cha Yesu Kristo.]
16Kwa kawaida wosia hutambuliwa tu kama kifo cha yule aliyeufanya huo wosia kimethibitishwa.
17Wosia hauwezi kutekelezwa mpaka kumetokea kifo, kwani wosia hauna maana ikiwa mwenye kuufanya bado anaishi.
18Ndiyo maana hata lile agano la kwanza halikuwekwa bila damu kumwagwa.[#9:18 Yaani, kwa kuuawa kwa wanyama wa tambiko.]
19Kwanza Mose aliwatangazia watu wote amri zote kama ilivyokuwa katika sheria; kisha akachukua damu ya ndama pamoja na maji, na kwa majani ya mti wa husopo na pamba nyekundu, akakinyunyizia kile kitabu cha sheria na watu wote.[#9:19-20 Husopo na pamba nyekundu - vitu ambavyo kutokana na utamaduni wa kidini wa Wayahudi vilitumika katika ibada ya kutawadha (Kut 12:22; Lawi 14:4-6; Hes 19:6,18); tazama Yoh 19:29 ambapo majani ya mti huohuo yanatumika aghalabu kama kifano, kukumbusha kwamba hapo kuna tukio la umwagaji damu lenye kutakasa.]
20Mose alisema: “Hii ni damu inayothibitisha agano mliloamriwa na Mungu mlitii.”[#9:20 Kut 24:6-8; Ebr 10:29; 13:20; rejea Mat 26:28 na sehemu nyingine sambamba katika Injili na 1Kor 11:25.]
21Vilevile Mose aliinyunyizia damu ile hema na vyombo vya ibada.
22Naam, kadiri ya sheria karibu kila kitu chaweza kutakaswa kwa damu, na dhambi nazo zaondolewa tu ikiwa damu imemwagwa.[#9:22 Taz 9:20 na rejea Lawi 5:10,16,18; 17:11.]
23Vitu hivi ambavyo ni mfano tu wa mambo halisi ya mbinguni, vililazimika kutakaswa kwa namna hiyo. Lakini vitu vya mbinguni huhitaji tambiko iliyo bora zaidi.[#9:23 Au, “kopi”: Tazama Ebr 8:3-5.; #9:23 Taz Ebr 7:19 maelezo.]
24Maana Kristo hakuingia Mahali Patakatifu palipojengwa kwa mikono ya watu, ambapo ni mfano tu wa kile kilicho halisi. Yeye aliingia mbinguni kwenyewe ambako sasa anasimama mbele ya Mungu kwa ajili yetu.[#9:24 Ebr 7:25. Rejea Yoh 17:20-26 ambapo Yesu anasema yeye mwenyewe anachukua nafasi ya mwombezi: “Nawaombea …” (Rom 8:34; 1Yoh 2:1).]
25Kuhani mkuu wa Wayahudi huingia Mahali Patakatifu kila mwaka akiwa na damu ya mnyama; lakini Kristo hakuingia humo ili ajitoe mwenyewe mara nyingi,[#9:25 Rejea aya ya 7.]
26maana ingalikuwa hivyo, Kristo angalipaswa kuteswa mara nyingi tangu kuumbwa ulimwengu. Lakini sasa, nyakati hizi zinapokaribia mwisho wake, yeye ametokea mara moja tu kuondoa dhambi kwa kujitoa yeye mwenyewe tambiko.
27Basi, kama vile kila mtu hufa mara moja tu, kisha husimama mbele ya hukumu ya Mungu,
28vivyo hivyo Kristo naye alijitoa tambiko mara moja tu kwa ajili ya kuziondoa dhambi za wengi. Atakapotokea mara ya pili, si kwa ajili ya kupambana na dhambi, bali ni kwa ajili ya kuwaokoa wale wanaomngojea.