The chat will start when you send the first message.
1Basi, mfalme Hezekia aliposikia habari hiyo alirarua mavazi yake, akavaa vazi la gunia, akaingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.[#37:1 Kufanya hivyo ni kuonesha kilio au ombolezo. Mavazi ya gunia yalimfanya aliyeyavaa kujisikia mateso kwa vile yalikuwa yenye kuwasha kiasi. Vilevile Wayahudi walijirashia majivu au vumbi kwa lengo hilo hilo.]
2Aliwaamuru Eliakimu, mkuu wa ikulu, Shebna, katibu, na wazee wa makuhani, wamwendee nabii Isaya mwana wa Amozi, wakiwa wamevaa mavazi ya magunia.
3Nao wakamwambia Isaya, “Hezekia anasema hivi, ‘Leo ni siku ya huzuni, siku ya kukemewa, na ya dharau. Sisi tumekuwa kama mama anayetaka kujifungua mtoto, lakini hana nguvu ya kumzaa.
4Inawezekana kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wako alisikia maneno ya mkuu wa matowashi ambaye ametumwa na mfalme wa Ashuru, bwana wake, ili kumtukana Mungu aliye hai, naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wako atapinga maneno aliyoyasikia; kwa hiyo waombee watu waliobaki.’”
5Basi, hao watumishi wa mfalme Hezekia walipokwisha fika kwa Isaya,
6yeye akawaambia, “Mwambieni bwana wenu kwamba Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Usiogope kwa sababu ya maneno ya watumishi wa mfalme wa Ashuru uliyoyasikia, maneno ambayo wameyasema kunidharau.
7Tazama nitamfanya mfalme asikie uvumi halafu atarudi katika nchi yake, na huko nitamfanya auawe kwa upanga.’”[#37:7 Huenda yahusu uvumi wa fujo miongoni mwa watu wake nchini (rejea aya 28).]
8Kisha yule mkuu wa matowashi aliposikia kwamba mfalme wa Ashuru alikuwa ameondoka Lakishi, aliondoka na kumkuta akishambulia mji wa Libna.
9Halafu aliposikia habari kwamba Tirhaka mfalme wa Kushi anakuja kupigana naye, alituma wajumbe kwa Hezekia, akisema,[#37:9 Huyo alikuwa wa ukoo wa kifalme wa ishirini na tano (Isa 18:1-7 maelezo). Alitawala wakati mmoja na ndugu yake nchini Misri yapata mwaka 690 K.K. na kama mfalme tangu mwaka 685-664 K.K.]
10“Mwambieni Hezekia mfalme wa Yuda: ‘Usikubali Mungu wako unayemtegemea akudanganye kwa kukuahidi kwamba Yerusalemu hautatekwa na mfalme wa Ashuru.
11Wewe umekwisha sikia jinsi wafalme wa Ashuru walivyozitenda nchi nyingine na kuziangamiza kabisa. Je, unadhani wewe utaokoka?
12Je, miungu ya mataifa iliokoa Gozani, Harani, Resefu na Waedeni waliokaa Telasari, mataifa ambayo wazee wangu waliyaangamiza?[#37:12 Nchi na watu wanaotajwa katika aya hii walikuwa wenyeji wa Mesopotamia.]
13Wako wapi wafalme wa Hamathi, Arpadi, Sefarvaimu, Hena na Iva?’”
14Mfalme Hezekia alipokea barua kutoka kwa wajumbe na kuisoma. Kisha akaenda na kuingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, akaiweka mbele ya Mwenyezi-Mungu.
15Halafu akamwomba Mwenyezi-Mungu akisema;
16“Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, unayeketi katika kiti cha enzi juu ya viumbe wenye mabawa. Wewe ndiwe uliyeumba mbingu na dunia.[#37:16 Taz Kut 25:52. Kiebrania ni “kerubimu” (Mwa 2:24 maelezo). Viumbe hivyo vilionesha ukuu wa kimungu. Viumbe viwili vyenye mabawa vilivyokuwa juu ya sanduku la agano vilikuwa ishara ya kiti cha enzi cha Mungu asiyeonekana.]
17Ee, Mwenyezi-Mungu, fumbua macho uone, tega sikio lako, uyasikie matusi yote ambayo Senakeribu amepeleka na kukutukana wewe Mungu uliye hai.
18Ee Mwenyezi-Mungu, ni kweli kwamba wafalme wa Ashuru wameangamiza mataifa yote na nchi zao.
19Waliweza kuitupa miungu yao motoni, kwa sababu haikuwa miungu kweli bali sanamu za miti au mawe zilizochongwa na mikono ya watu.
20Sasa ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, utuokoe makuchani mwa Senakeribu, ili falme zote za dunia zijue kwamba wewe peke yako ndiwe uliye Mwenyezi-Mungu.”
21Kisha Isaya mwana na Amozi, alituma ujumbe kwa Hezekia akisema, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli: Kwa kuwa umeniomba kuhusu Senakeribu mfalme wa Ashuru,
22basi huu ndio ujumbe wangu kuhusu huyo mfalme:
Mji wa Siyoni, naam, Yerusalemu,
unakudharau na kukutukana.
Yerusalemu, mji mzuri
unakutikisia kichwa kwa dhihaka.
23Wewe umemtukana nani?
Umemkashifu nani?
Umethubutu kumbeza nani kwa majivuno?
Ni mimi Mungu, Mtakatifu wa Israeli!
24Umewatumia watumishi wako kunidhihaki mimi Bwana;
wewe umesema, ‘Kwa magari yangu mengi ya vita,
nimekwea vilele vya milima,
mpaka kilele cha Lebanoni.
Nimeangusha mierezi yake mirefu,
na misonobari mizurimizuri.
Nimevifikia vilele vyake
na ndani ya misitu yake mikubwa.
25Nimechimba visima na kunywa maji yake,
na nilikausha vijito vya Misri
kwa nyayo za miguu yangu.’
26“Je, hujasikia ewe Senakeribu kwamba
nilipanga jambo hili tangu zamani?
Ninachotekeleza sasa nilikipanga zamani.
Nilikuweka uifanye miji yenye ngome
kuwa rundo la magofu.
27Wakazi wake wakiwa wameishiwa nguvu,
wametishika na kufadhaika.
Wamekuwa kama mimea shambani,
kama nyasi changa shambani,
kama majani yaotayo juu ya paa
au kama ngano kabla hazijakomaa
ambazo hunyauka upepo mkavu uvumapo.
28Lakini, nakujua wewe Senakeribu;
najua kila unachofanya na kuacha kufanya;
najua mipango yako dhidi yangu.
29Kwa vile umefanya mipango dhidi yangu
na nimeusikia ufidhuli wako,
nitatia ndoana yangu puani mwako,
na lijamu yangu kinywani mwako.
Nitakurudisha njia ileile uliyojia.”
30“Na hii ndiyo itakuwa ishara kwako Hezekia: Mwaka huu na mwaka ujao mtakula kinachomea chenyewe bila kupandwa. Lakini katika mwaka wa tatu mtapanda na kuvuna mavuno; mtapanda mizabibu na kula matunda yake.
31Wale watakaobaki katika ukoo wa Yuda wataongezeka na kuwa wengi kama vile mti unavyotoa mizizi yake udongoni na kuzaa matunda juu.[#37:30-32 Taz Isa 4:2-6 maelezo.]
32Maana kutakuwa na watu watakaosalia huko Yerusalemu; naam, huko mlimani Siyoni kutakuwako watu wachache watakaosalimika.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi amedhamiria kukamilisha hayo.
33Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya mfalme wa Ashuru: “Hataingia katika mji huu, wala kuupiga mshale wala kuingia kwa ngao wala kuuzingira.
34Atarudi kwa njia ileile aliyojia na wala hataingia katika mji huu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimetamka hayo.
35Naam, kwa ajili ya heshima yangu mimi na kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi nitaulinda na kuuokoa mji huu.”[#37:35 Rejea ahadi ya Mungu kwa Daudi katika 2Sam 7:1-16.]
36Basi, wakati wa usiku malaika wa Mwenyezi-Mungu aliingia kambini mwa Waashuru na kuwaua watu 185,000. Halafu kulipopambazuka watu hao wote walionekana wakiwa maiti.
37Kisha Senakeribu mfalme wa Ashuru akaondoka, akaenda kwake, akakaa Ninewi.[#37:37-38 “Senakeribu” aliuawa mwaka 681 K.K. “Ararat” ni eneo ambalo kwa sasa ni nchi ya Armenia na sehemu ya Uturuki. “Esar-hadoni” alikuwa mfalme wa Ashuru na Babuloni kati ya mwaka 681 na 669 K.K.]
38Siku moja, wakati Senakeribu alipokuwa akiabudu katika nyumba ya Nisroki mungu wake, wanawe wawili, Adrameleki na Sharezeri, walimuua kwa upanga, halafu wakakimbilia nchini Ararati. Naye Esar-hadoni, mwanawe, akatawala badala yake.