Isaya 39

Isaya 39

Wajumbe kutoka Babuloni

(2 Fal 20:12-19)

1Wakati huo, mfalme Merodak-baladani mwana wa Baladani, mfalme wa Babuloni, aliposikia kwamba Hezekia alikuwa ameugua na sasa amepona, alimtumia ujumbe pamoja na zawadi.[#39:1-2 Taz 2Fal 20:12. Mfalme huyu alitawala huko Babuloni tangu mwaka 721 hadi 710 K.K. Huenda kufika kwa wajumbe wake Yerusalemu kulikuwa na shabaha ya kumwomba mfalme Hezekia msaada dhidi ya Ashuru. Jina “Merodak-baladani” ni Kiebrania cha jina la Kibabuloni “Marduk-apalidini” maana yake ni “Marduki” (mungu) amepata mtoto.]

2Basi, Hezekia aliwakaribisha na kuwaonesha nyumba ya hazina: fedha, dhahabu, viungo vya kukolezea chakula, mafuta ya thamani, vifaa vyake vyote vya kijeshi na vitu vyote vilivyokuwamo katika bohari zake. Hakuna chochote katika ikulu yake au katika nchi yake ambacho hakuwaonesha.

3Ndipo nabii Isaya alipokwenda kwa mfalme Hezekia na kumwuliza, “Watu hawa wamesema nini? Na, wamekujia kutoka wapi?” Naye Hezekia akamjibu “Wamenijia kutoka nchi ya mbali, huko Babuloni.”

4Halafu Isaya akamwuliza, “Wameona nini katika ikulu yako?” Hezekia akamjibu, “Wameona yote yaliyomo katika ikulu yangu. Hakuna chochote katika bohari zangu ambacho sikuwaonesha.”

5Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la Mwenyezi-Mungu wa majeshi:[#39:5-7 Baadhi ya wafafanuzi wa Maandiko Matakatifu wanahusisha tangazo hili na kuwekwa jela kwa Manase, mwanawe Hezekia, kule Babuloni, tukio linalosimuliwa katika 2Nya 33:10-13; lakini lawezekana linahusu kuchukuliwa Waisraeli wengi uhamishoni chini ya mfalme Nebukadneza (2Fal 24:10—25:17).]

6Tazama, siku zinakuja ambapo vyote vilivyomo nyumbani mwako na vitu vyote walivyokusanya wazee wako hadi leo, vitapelekwa mpaka Babuloni. Hakuna kitu chochote kitakachobaki; ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu.

7Tena baadhi ya watoto wako mwenyewe wa kiume watapelekwa mateka nao watakuwa matowashi katika ikulu ya mfalme wa Babuloni.”

8Naye Hezekia akamwambia Isaya, “Neno la Mwenyezi-Mungu ulilosema ni sawa.” Alisema hivyo kwani alifikiri, “Kutakuwa na amani na usalama muda wote niishipo.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania