Isaya 63

Isaya 63

Mungu awaadhibu maadui za watu wake

1Ni nani huyu ajaye kutoka Edomu,[#63:1 Hiyo ilikuwa nchi mpakani mwa nchi ya Yuda upande wa kusini, mji wake mkuu ulikuwa Bosra, yapata kilomita 30 kusini-mashariki ya Bahari ya Chumvi (rejea Isa 34:6; Yer 49:13,22; Amo 1:12). Kulikuwa na uhasama wa jadi kati ya Waisraeli na Waedomu, uhasama ambao ulikithiri hasa wakati wa uhamisho wa Waisreli (Zab 137:7; Ombo 4:21-22). Hapa nchi hiyo inatajwa kuwakilisha maadui wote wa Waisraeli “Edomu … Bosra”: Msomaji atatambua kwamba majina haya mawili yanatumika pia kwa lengo fulani la muundo wa kimaandishi. “Edomu” linafanana na jina la Kiebrania lenye maana ya “ekundu” (adom). Tena, jina “Bosra” linakumbusha picha ya “mvunazabibu” (bozer).]

anayefika kutoka Bosra na mavazi ya madoa mekundu?

Ni nani huyo aliyevaa mavazi ya fahari,

anatembea kwa nguvu zake kubwa?

Ni mimi Mwenyezi-Mungu

ninayetangaza ushindi wangu;

nami ni mwenye nguvu ya kuokoa.

2Lakini mbona nguo yako ni nyekundu,

nyekundu kama ya mtu anayekamua zabibu?

3“Naam, nimekamua zabibu peke yangu,[#63:3 Rejea Ombo 1:15; Yoe 3:13; Ufu 14:20; 19:15. “Nguo zangu zimejaa madoa ya damu yao …”: Rejea Ufu 19:13.]

wala hakuna mtu aliyekuja kunisaidia.

Nimeyakanyaga mataifa kwa hasira yangu,

niliyapondaponda kwa ghadhabu yangu.

Nguo zangu zimejaa madoa ya damu yao,

imeyachafua kabisa mavazi yangu.

4Niliamua kuwa siku ya kulipiza kisasi imefika;

wakati wa kuwakomboa watu wangu umefika.

5Nilitazama na hapakuwa na wa kunisaidia;

nilishangaa hapakuwa na wa kuniunga mkono.

Lakini nilijipatia ushindi kwa mkono wangu,

ghadhabu yangu ilinihimiza.

6Kwa hasira yangu niliwaponda watu,

niliwalewesha kwa ghadhabu yangu;

damu yao niliimwaga chini ardhini.”

Wema wa Mungu kwa Israeli

7Nitasimulia fadhili za Mwenyezi-Mungu;

nitataja matendo yake yote yastahiliyo sifa,

kwa sababu ya yote aliyotutendea,

wema wake mkuu aliowapa Waisraeli kwa huruma yake,

kadiri ya wingi wa fadhili zake.

8Maana alisema juu yao:

“Hakika, hawa ni watu wangu;

watoto wangu ambao hawatanidanganya.”

Basi yeye akawa Mwokozi wao.

9Katika taabu zao zote,

hakumtuma mjumbe mwingine kuwasaidia,

ila yeye mwenyewe alikuja kuwaokoa.

kwa upendo na huruma yake aliwakomboa.

Aliwabeba na kuwachukua tangu zamani.

10Lakini wao walikuwa wakaidi,

wakaihuzunisha roho yake takatifu.

Basi, Mungu akageuka, akawa adui yao;

yeye mwenyewe akapigana nao.

11Ndipo walipokumbuka siku za zamani,

wakati wa Mose mtumishi wa Mwenyezi-Mungu.

Wakauliza, “Yuko wapi sasa Mwenyezi-Mungu,

aliyewaokoa wachungaji wa kundi lake baharini?

Yuko wapi yule aliyeiweka roho yake takatifu kati yao,

12ambaye kwa mkono wake wenye nguvu

alifanya maajabu kwa njia ya Mose,

akapasua bahari na kuwaongoza watu wake,

na kujipatia jina la milele?

13Aliwaongoza katikati ya vilindi vya bahari,

wakapita humo kama farasi bila kujikwaa.

14Kama ng'ombe wapelekwavyo malishoni bondeni,

ndivyo roho ya Mungu ilivyowapumzisha watu wake.

Ndivyo ee Mungu ulivyowaongoza watu wako,

nawe ukajipatia jina tukufu.”

Sala ya kuomba msaada

15Ututazame kutoka mbinguni ee Mungu, uone,

utuangalie kutoka makao yako matakatifu na matukufu.

Iko wapi bidii yako kwa ajili yetu na nguvu yako?

Usiache kutuonesha upendo wako.

16Maana wewe ndiwe Baba yetu;

Abrahamu, mzee wetu, hatujali,

naye Israeli hatutambui;

lakini wewe, ee Mwenyezi-Mungu, ni Baba yetu.

Wewe umeitwa tangu kale: “Mkombozi wetu.”

17Ee Mwenyezi-Mungu, mbona unatukosesha njia zako?

Mbona unatufanya kuwa wakaidi hata tusikuogope?

Rudi ee Mungu kwa ajili ya watumishi wako,

makabila ambayo daima yalikuwa mali yako.

18Kwa kitambo tu sisi watakatifu wako tulimiliki nchi,

lakini maadui zetu wakaja wakaharibu maskani yako.

19Tumekuwa kama watu ambao hujawatawala kamwe,

kama watu ambao hawakujulikana kwa jina lako.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania