Isaya 7

Isaya 7

Ujumbe kwa mfalme Ahazi

1Wakati mfalme Ahazi mwana wa Yothamu na mjukuu wa Uzia, alipokuwa anatawala Yuda, Resini, mfalme wa Aramu, na Peka mwana wa Remalia, mfalme wa Israeli, waliushambulia mji wa Yerusalemu, lakini hawakuweza kuuteka.[#7:1 Ahazi alitawala Yuda kuanzia mwaka 736 mpaka 716 K.K. Rejea 2Fal 16:5; 2Nya 28:5-6. Taz pia Isa 1:1.]

2Mfalme wa Yuda alipopata habari kwamba Waashuru wanashirikiana na Waisraeli, yeye pamoja na watu wote wa Yuda waliogopa na kutetemeka kama miti inayotikiswa na upepo.[#7:2 Kiebrania hapa tuna “Efraimu” ambalo ni jina lingine la kutaja utawala wa kusini, yaani Yuda (ndivyo pia katika aya 5,8,9,17; taz pia Hosea 4:17-18).]

3Mwenyezi-Mungu akamwambia Isaya, “Mchukue mwanao, Shearyashubu, uende kukutana na mfalme Ahazi. Utamkuta barabarani mahali wanapofanyia kazi watengenezaji nguo, mwisho wa mfereji uletao maji kutoka bwawa la juu.[#7:3 Kuweko hapo kwa mtoto wa nabii ni muhimu: “Shearyashubu” maana yake ni “watakaobaki warudi” (Isa 4:2-6; 10:21). Jina hilo la kimfano aghalabu lingeweza kumtaarifu mfalme Ahazi kwamba Mungu hataacha kutekeleza ahadi aliyotoa ya kuendeleza utawala wa ukoo wa Daudi (2Sam 7:1-16) hata katika mazingira kama hayo ambayo yanamkabili mfalme.; #7:3 Huenda mfalme alikuwa huko kukagua hali ya mfereji huo ambao ulikuwa muhimu sana hasa wakati wa vita kwa kuwapatia maji wakazi wa Yerusalemu; mazingira yenyewe ya tishio la kushambuliwa yalihitaji jambo la namna hiyo (taz pia Isa 8:6-7 na 30:2 ambapo karibu mazingira hayohayo yanahusika).]

4Mwambie awe macho, atulie na asiogope wala asife moyo, kwa sababu ya hasira kali ya mfalme Resini wa Ashuru, na ya mwana wa Remalia. Hao wawili ni kama tu moshi wa kuni zinazozimika.[#7:4 Lugha hii ya mfano (Kiebrania: “kijinga cha moto kinachofuka moshi”) inamaanisha kwamba nguvu za Ashuru na Israeli zinaishia.]

5Waashuru, kadhalika na Peka pamoja na jeshi la Efraimu wamefanya mpango mbaya dhidi yako. Wamesema,

6‘Twende kuivamia nchi ya Yuda, tuwatie watu hofu, tuitwae nchi na kumtawaza mwana wa Tabeeli awe mfalme wao.’[#7:6 Si dhahiri ni nani hasa huyo anayetajwa hapa.]

7“Lakini mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi:

Jambo hilo halitafaulu kamwe.

8-9Kwani mji mkuu wa Aramu ni Damasko,

na huyo Resini ni mkuu wa Damasko tu.

Mji mkuu wa Efraimu ni Samaria,

na mwana wa Remalia ni mkuu wa Samaria tu.

Mnamo miaka sitini na mitano utawala wa Efraimu utavunjwa;

Efraimu halitakuwa taifa tena.

Kama hutaamini hutaimarika.”

Ishara ya Emanueli

10Tena Mwenyezi-Mungu akamwambia Ahazi,

11“Mwombe Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, akupe ishara; iwe ni kutoka chini kuzimu au juu mbinguni.”[#7:11 Taz pia Isa 8:18; 20:3; 37:30; 38:7-8 ambapo matumizi ya neno hilo yanamaanisha “jambo au tukio lenye kuonesha dhahiri kwamba tukio au kitu kingine kitatendeka.”]

12Ahazi akajibu, “Sitaomba ishara! Sitaki kumjaribu Mwenyezi-Mungu.”[#7:12 Kumb 6:16. Kutokana na jibu la Isaya katika aya ifuatayo ni dhahiri kwamba maneno ya Ahazi ni kisingizio.]

13Basi, Isaya akamjibu, “Sikiliza basi, enyi watu wa ukoo wa Daudi! Je, haitoshi kuwachosha watu hata sasa mnataka kumchosha Mungu wangu pia?[#7:13 Kiebrania “nyumba ya Daudi”. Hapa nabii anaelekeza ujumbe wake moja kwa moja kwa mfalme Ahazi ambaye ni mtawala wa jadi wa ukoo wa Daudi.]

14Haya basi, Bwana mwenyewe atawapa ishara: msichana atachukua mimba, atajifungua mtoto wa kiume na kumwita jina lake Emanueli.[#7:14 Kiebrania neno linalotumiwa hapa ni “alma” neno ambalo katika mazingira mengine laweza kumaanisha “bikira” au “mwanamwali” kwa lugha ya zamani kidogo ya Kiswahili (rejea Mwa 24:43; Kut 2:8; Zab 68:25; Wim 6:8). Neno “bikira” ambalo latumiwa mara nyingine ni sawa na neno “parthenos” la tafsiri ya Septuajinta ya mwaka wapata 200 K.K. ambayo ilitumiwa sana na Wakristo wa kwanza. Mathayo 1:23 alielewa neno hilo kuwa na maana ya “bikira” na akalitumia barabara kuhusu Maria mama yake Yesu.; #7:14 Jina hili katika Kiebrania lamaanisha “Mungu (yuko) pamoja nasi”, jina ambalo hapa latilia tena mkazo ulinzi wake Mungu juu ya utawala wa jadi wa ukoo wa Daudi na pia ulinzi wa Waisraeli.]

15Atakula siagi na asali mpaka atakapojua kukataa mabaya na kuchagua mema.[#7:15 Labda matumizi ya mfano kama rejeo kwa nyakati za Waisraeli walipokuwa jangwani. Katika Kumb 32:13-14, sehemu ya utenzi wa Mose, “asali na siagi” ni mojawapo ya mambo ambayo Mwenyezi-Mungu aliwapa Waisraeli kule jangwani. Kwa kufanya hivyo alijionesha kwao kuwa Mungu Mkuu (aya ya 3). Kwa hiyo yawezekana kwamba wazo lililopo hapa ni lilelile la kusisitiza kwamba Mungu atawalea watu wake kama pale awali. Rejea pia aya 21 ambapo watakaosalia watajaliwa mema. Hali yenyewe itakuwa ngumu lakini mpango wa Mungu kwa ajili ya watu wake utaendelea.]

16Maana, kabla mtoto huyo hajajua kukataa maovu na kuchagua mema, nchi za wafalme hao wawili unaowaogopa zitakuwa mahame.

17Mwenyezi-Mungu atakuletea wewe pamoja na watu wako na jamii yote ya kifalme siku za taabu kuliko zile zote zilizowahi kutokea tangu wakati watu wa Efraimu walipojitenga na Yuda; yaani, atawaleteeni mfalme wa Ashuru.”[#7:17 Mnamo mwaka 732 Ashuru iliivamia Siria na utawala wa kaskazini yaani Israeli. Taz jinsi Ahazi alivyotenda kuhusu mfalme wa Ashuru katika 2Fal 16:5-18. Mwishowe hata utawala wa Yuda pia nao ulivamiwa na Waashuru (2Fal 18:13-37; Isa 8:6-8; 36:1).]

18Wakati huo, Mwenyezi-Mungu atawapigia mruzi watu wa Misri waje kama nzi toka vijito vya mto Nili; na watu wa Ashuru waje kama nyuki kutoka nchi yao.[#7:18 Tishio kubwa hapa kwa utawala wa Yuda sio Misri ila ni Ashuru.; #7:18-25 Hapa tuna utabiri wa mambo manne ambayo yameunganishwa na utabiri wa aya ya 17; utabiri wote unaanza na maneno “wakati huo” (aya 18,20,21,23).]

19Watakuja makundi kwa makundi na kuyajaza mabonde yaliyopasukapasuka, mapango miambani, miiba, vichaka vyote na malisho yote.

20Wakati huo, Bwana atakopa wembe kutoka ng'ambo ya mto Eufrate, yaani mfalme wa Ashuru. Atawanyoa vichwa vyenu, miili yenu na kukatilia mbali pia ndevu zenu.[#7:20 Mto Eufrate ulikuwa katika nchi ya Ashuru eneo ambalo sasa ni nchi ya Iraki.; #7:20 Kunyolewa kichwa ndevu na mwili ilikuwa kitendo cha dharau na cha kuabisha sana (taz 2Sam 10:4-5).]

21Wakati huo, mtu atafuga ng'ombe mmoja mchanga na kondoo wawili;

22nao watatoa maziwa kwa wingi hata aweze kula siagi. Watu watakaosalia katika nchi watakula siagi na asali.

23Wakati huo, kila mahali palipokuwa na mashamba ya mizabibu kwa maelfu ya thamani ya fedha 1,000 kwa kipimo cha hekalu yatakuwa mbigili na miiba mitupu.

24Watu watakwenda huko kuwinda kwa pinde na mishale, maana nchi yote itakuwa imejaa mbigili na miiba.

25Nayo milima yote iliyokuwa ikilimwa itakuwa imejaa mbigili na miiba, hata hakuna mtu atakayejaribu kwenda huko, badala yake itakuwa malisho ya ng'ombe na kondoo.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania