The chat will start when you send the first message.
1Waisraeli walitenda tena uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, naye akawaacha watawaliwe na Wafilisti kwa miaka arubaini.[#13:1-25 Hapa inaanza hadithi ya Samsoni ambaye ni shujaa wa kijiji chake na ambaye aliwalipiza kisasi Wafilisti. Samsoni anajulikana kwa nguvu zake za ajabu na mambo mengine kuhusu tabia yake yanaelezwa katika 14-16.; #13:1 Samsoni anahusika sana na Wafilisti karibu kila wakati wa maisha yake. Hao walikuwa adui wakubwa wa Waisraeli tangu wakati wa kuingia Kanaani mpaka wakati wa Daudi. Katika Yos 13:3 miji au maeneo matano ya watawala wa Wafilisti inatajwa.]
2Kulikuwa na mtu mmoja huko Sora, wa kabila la Dani, jina lake Manoa. Mke wake alikuwa tasa.[#13:2 Mji wa kale wa Kanaani yapata kilomita 20 magharibi ya Yerusalemu. Kadiri ya Yos 19:41 mji huu ulikuwa kwanza wa eneo la Dani lakini baadaye ukawa sehemu ya kabila la Yuda (Yos 15:33).; #13:2 Kwamba mke wa Manoa (baba yake Samsoni) alikuwa tasa, mwandishi anataka kusema kwamba kuzaliwa kwa Samsoni kulitokana na uwezo wa Mungu mwenyewe.]
3Siku moja, malaika wa Mwenyezi-Mungu akamtokea huyo mwanamke, akamwambia, “Wewe ni tasa, huna watoto. Lakini utapata mimba na kumzaa mtoto wa kiume.
4Kwa hiyo uwe mwangalifu, usinywe divai au kileo wala usile kitu chochote kilicho najisi,
5kwa maana utachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume. Nywele za mtoto huyo kamwe zisinyolewe, maana atakuwa amewekwa wakfu kwa Mungu tangu kuzaliwa kwake. Naye ataanza kuwakomboa Waisraeli mikononi mwa Wafilisti.”[#13:5 Masharti na majukumu yanayotajwa hapa (taz 4-5) kwa kawaida yahusu mtu aliyewekwa wakfu kwa Mungu kwa nadhiri fulani (taz Hes 6:1-8). Maneno “aliyewekwa wakfu kwa Mungu” Kiebrania ni “aliye mnadhiri wa Mungu”.]
6Mwanamke huyo akaenda kumwambia mume wake, “Mtu wa Mungu ambaye sura yake ilikuwa kama ya malaika wa Mungu alinijia. Sikumwuliza alikotoka wala hakuniambia jina lake.
7Lakini aliniambia kwamba nitachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume. Aliniamuru nisinywe divai au kileo wala kula chochote kilicho najisi, maana mtoto huyo atakuwa amewekwa wakfu kwa Mungu tangu kuzaliwa kwake mpaka atakapokufa.”
8Kisha Manoa akamwomba Mwenyezi-Mungu, akisema, “Nakuomba ee Mwenyezi-Mungu, umtume tena yule mtu wako uliyemtuma ili atufundishe mambo tunayopaswa kumtendea huyo mtoto atakayezaliwa.”
9Mwenyezi-Mungu akalisikia ombi la Manoa, na yule malaika wa Mungu akamwendea tena yule mwanamke alipokuwa ameketi shambani. Lakini mumewe, Manoa, hakuwa pamoja naye.
10Mwanamke akakimbia upesi, akamwambia mumewe, “Tazama! yule mtu aliyenijia siku ile amenitokea tena.”
11Manoa akafuatana naye mpaka kwa mtu huyo, akamwuliza, “Je, wewe ni yule mtu aliyezungumza na mwanamke huyu?” Yule mtu akamjibu, “Ni mimi.”
12Kisha Manoa akasema, “Sasa maneno yako yatakapotimia ni mambo gani tutakayofuata kwa ajili ya huyo mtoto? Tutafanya nini kwa ajili yake?”
13Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Manoa, “Mkeo atapaswa kushika yote niliyomwambia:
14asionje mazao yoyote ya mzabibu, wala asinywe divai au kileo wala kula chochote kilicho najisi. Yote niliyomwamuru, ayafuate.”
15Manoa akamwambia huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu, “Tafadhali, ukae kidogo tukutayarishie mwanambuzi.”[#13:15 Kumwandalia mgeni chakula ilikuwa ishara mahsusi ya ukarimu. Taz pia Mwa 18:1-8; Amu 6:19-22.]
16Yule malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Manoa, “Hata kama mkinilazimisha kukaa sitakula chakula chenu. Lakini kama ukipenda, tayarisha sadaka ya kuteketezwa, mtolee Mwenyezi-Mungu.” Manoa hakujua kuwa huyo alikuwa malaika wa Mwenyezi-Mungu.
17Basi, Manoa akamwambia huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu, “Tuambie jina lako ili tukuheshimu wakati maneno yako yatakapotimia.”
18Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Kwa nini unataka kujua jina langu, kwa kuwa jina langu ni la ajabu?”
19Hapo Manoa akatayarisha mwanambuzi na tambiko, akaviweka juu ya mwamba amtolee Mwenyezi-Mungu afanyaye maajabu.[#13:19 Bila shaka yahusu mahali maalumu pa kumtambikia Mungu. Waisraeli walimtambika Mungu kwa kumtolea wanyama fulanifulani, nafaka, matunda na viungo vya harufu nzuri, ili kumshukuru, kumwomba msamaha au kulipa kwa ajili ya mikosi mbalimbali ya watu.]
20Basi, wakati Manoa na mkewe walipokuwa wanatazama miali ya moto ikipanda juu mbinguni kutoka madhabahuni, walimwona malaika katika miali hiyo akipanda kwenda mbinguni. Basi Manoa na mkewe wakasujudu.
21Manoa akajua kuwa huyo alikuwa malaika wa Mwenyezi-Mungu. Malaika hakumtokea tena Manoa na mkewe.
22Basi, Manoa akamwambia mkewe, “Hakika tutakufa, maana tumemwona Mungu.”[#13:22 Taz 6:22 maelezo.]
23Lakini mkewe akamjibu, “Kama Mwenyezi-Mungu angetaka kutuua hangepokea sadaka yetu ya kuteketezwa na ya nafaka; wala hangetuonesha mambo hayo wala kutuambia maagizo.”
24Kisha mkewe Manoa akajifungua mtoto wa kiume, naye Manoa akampa jina Samsoni. Mtoto huyo akakua naye Mwenyezi-Mungu akambariki.[#13:24 Jina hili linafanana na jina la Kiebrania “shemesh” maana yake: “jua”. Yapata kilomita 3 kusini ya mji wa Sora alikozaliwa Samsoni (Amu 13:2), kuna mji maarufu uitwao “Beth-shemeshi” yaani: “nyumba ya jua”.]
25Roho ya Mwenyezi-Mungu ikaanza kumsukuma akiwa huko Mahane-dani, kati ya Sora na Eshtaoli.