The chat will start when you send the first message.
1Hili ni neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi-Mungu, wakati mfalme Sedekia alipowatuma Pashuri mwana wa Malkia, na kuhani Sefania mwana wa Maaseya, wamwambie Yeremia hivi:[#21:1-2 Kila ilipowezekana, Sedekia, mfalme wa Yuda, alimwendea Yeremia kutaka ushauri wake na kumsihi awaombee watu kwa Mwenyezi-Mungu. Hapa na katika Yer 37:3-10 aliwatuma wajumbe; nyakati nyingine yeye mwenyewe alimwendea Yeremia kwa faragha (Yer 37:17-21; 38:14-28). “Pashuri mwana wa Malkia”: huyo ofisa wa utawala ni Pashuri mwana wa Imeri, ambaye alikuwa kuhani na mkuu wa ulinzi hekaluni (Yer 20:1). Katika Yer 38:1-4 anatajwa miongoni mwa maofisa waliomshitaki nabii Yeremia kuwa ni mhaini, wakataka ahukumiwe kifo. “Sefania mwana wa Maaseya”: Rejea Yer 29:24-32. “Nebukadneza, mfalme wa Babuloni”: Huyu alishambulia Yerusalemu na baada ya mashambulizi marefu aliuteketeza (mwaka 586 K.K.). Rejea Fal 25:1-11; 2Nya 36:17-21.]
2“Tafadhali, tuombee kwa Mwenyezi-Mungu maana Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, anaanza vita dhidi yetu. Labda Mwenyezi-Mungu atatufanyia mwujiza kama afanyavyo mara kwa mara na kumfanya Nebukadneza atuache na kwenda zake.”
3Yeremia akawaambia:
4Nendeni mkamwambie Sedekia kwamba hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli: “Sedekia! Nitakugeuzia wewe mwenyewe silaha unazotumia kupigana na mfalme wa Babuloni na Wakaldayo wanaowazingira nje ya kuta za mji. Nitazikusanya silaha zote katikati ya mji huu.
5Mimi mwenyewe nitapigana nawe kwa mkono ulionyoka na wenye nguvu, kwa hasira, ukali na ghadhabu kubwa.[#21:5 Msemo wa kimfano katika Biblia ambao hutumika kuonesha ulinzi wa Mungu na nguvu yake katika vita. Taz hasa Kumb 4:34; 5:15; 7:19; 11:2; 26:8. Hapa unatumika kuonesha kwamba Mungu anapigana dhidi ya Yuda kwa kulitumia jeshi la Babuloni kama chombo chake cha kuwaadhibu watu wake waovu.]
6Nitawaua wakazi wa mji huu: binadamu na wanyama kadhalika. Watakufa kwa maradhi mabaya sana.
7Mimi Mwenyezi-Mungu nasema kuwa, baadaye wewe Sedekia mfalme wa Yuda, watumishi wako na watu wa mji huu ambao mtaponea maradhi hayo mabaya pamoja na vita na njaa, nitawatia mikononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babuloni na mikononi mwa adui zenu wanaowawinda. Nebukadneza atawaua kwa upanga na wala hatawahurumia au kuwaachilia au kuwasamehe. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
8“Nawe Yeremia utawaambia watu hawa kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Sikilizeni! Mimi nawapeni nafasi ya kuchagua njia ya uhai au njia ya kifo.[#21:8-10 Kadiri ya Yeremia taifa la Yuda halingeweza tena kuepa hukumu ya Mungu ambayo inalikabili kwa sababu ya dhambi zake na ukaidi wake uliozidi mno. (Taz pia Yer 2:23 maelezo; 9:3; 13:23). Babuloni ilikuwa chombo anachotumia Mungu kutekeleza mpango wake (taz Yer 27:6). Wakati huo, kujiweka chini ya mamlaka ya Babuloni ilikuwa kutii matakwa ya Mungu na ni njia moja tu iliyobakia ya kuliokoa taifa na maangamizi yanayokaribia. Lakini wengi wa wananchi waliomsikia Yeremia, hawakuamini hayo; walimwona kuwa mhaini (rejea Yer 38:4).]
9Mtu atakayebaki mjini humu atauawa kwa upanga au kwa njaa au kwa maradhi mabaya. Lakini mtu atakayetoka nje ya mji na kujisalimisha kwa Wakaldayo wanaouzingira mji, ataishi; naam, atayanusurisha maisha yake.
10Nimeamua kuuletea mji huu maafa na sio mema, nasema mimi Mwenyezi-Mungu. Nitautia mikononi mwa mfalme wa Babuloni, naye atauteketeza kwa moto.
11“Utaiambia jamaa ya mfalme wa Yuda: Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu,
12enyi jamaa ya Daudi! Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi:
Tekelezeni haki tangu asubuhi,
na kuwakomboa mikononi mwa wadhalimu
wote walionyang'anywa mali zao.
La sivyo, hasira yangu itachomoza kama moto,
itawaka na wala hakuna atakayeweza kuizima,
kwa sababu ya matendo yenu maovu.
13Tazama, mimi sasa napambana nanyi mnaoishi bondeni,
mnaokaa kwenye mwamba wa tambarare,
nyinyi mnaosema, ‘Nani atathubutu kutushambulia?
Nani awezaye kuingia katika makazi yetu?’
14Nitawaadhibu kadiri ya matendo yenu;
mimi Mwenyezi-Mungu nasema.
Nitawasha moto katika msitu wenu
nao utateketeza kila kitu kinachouzunguka.”