The chat will start when you send the first message.
1Siku zile Yohane Mbatizaji alitokea, akaanza kuhubiri katika jangwa la Yudea:[#3:1 Injili zote nne zinaafikiana kwa jumla juu ya kuhusisha mwanzo wa kazi yake Yesu na mahubiri ya Yohane Mbatizaji (rejea Marko 1:1-14; Luka 3:1-22; Yoh 1:19-36). Yohane Mbatizaji ni mjumbe yule aliyetangazwa na nabii Isaya (3:3); anatajwa kuwa mkuu kuliko watumishi wote wa Mungu wa hapo awali (11:7-11); anatajwa pia kuwa Elia ambaye angefika siku ile ya mwisho ya hukumu (Mal 3:1; 4:5; Mat 11:13-14; 17:10-13).; #3:1 Yapata mwaka 27 B.K. karibu miaka 30 tangu matukio ya sura ya pili (Luka 3:1-3).; #3:1 Sehemu iliyokaliwa na watu wachache sana; sehemu yenyewe ilikuwa kusini mwa Yerusalemu kuelekea mji Hebroni hadi Bahari ya Chumvi.]
2“Tubuni, maana ufalme wa mbinguni umekaribia.”[#3:2 Neno lenyewe ni tafsiri ya neno la Kigiriki “metanoite” nalo lina maana ya kubadilisha mwenendo mbaya, kuacha maisha mabaya na kuishi maisha mema. Neno la kawaida lililotumika katika Kiebrania kuelezea jambo hilo ni “shub”, nalo lamaanisha “kurudi”, yaani kumrudia Mungu.; #3:2 Kufuatana na desturi ya Wayahudi ya kutotamka jina la Mungu, Mathayo anapendelea kusema “Ufalme wa mbinguni” badala ya “Ufalme wa Mungu” maneno ambayo yanatumiwa na wale waandishi wengine wa Injili. Ufalme wa mbinguni wa Mungu, ni utawala wa Mungu kati ya watu.]
3Huyu Yohane ndiye yule ambaye nabii Isaya alinena juu yake aliposema:
“Sauti ya mtu anaita jangwani:
‘Mtayarishieni Bwana njia yake,
nyosheni barabara zake.’”
4Yohane alivaa vazi lililoshonwa kwa manyoya ya ngamia, na ukanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni.
5Basi, watu kutoka Yerusalemu, kutoka pande zote za Yudea na sehemu zote za kandokando ya mto Yordani, walimwendea,
6wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani.[#3:6 Ibada yenyewe ya kutumia maji ilikuwa ishara ya kutakaswa rohoni na kujiweka tayari kwa hukumu ya Mungu.]
7Lakini alipowaona Mafarisayo wengi na Masadukayo wanamjia ili awabatize, aliwaambia, “Enyi kizazi cha nyoka! Ni nani aliyewadokezea muikimbie ghadhabu inayokuja?[#3:7 “Mafarisayo” walikuwa kikundi cha Wayahudi ambao walisisitiza sana kuzingatia sheria na mapokeo ya Wayahudi mara nyingine kwa unafiki. “Masadukayo” kwa upande mwingine walikuwa zaidi hasa wanasiasa na walihitilafiana na Mafarisayo kwa vile walikana kuweko ufufuo wa wafu, roho na malaika (taz Mate 23:8).; #3:7 Msemo wa kukaripia, sawa na kusema kwa mfano: “wajeuri wabaya kama nyoka”.; #3:7 Hapa inamaanisha “hukumu”.]
8Onesheni kwa vitendo kwamba mmetubu.
9Msifikiri na kujisemea, ‘Baba yetu ni Abrahamu!’ Nawaambieni hakika, Mungu anaweza kuyafanya mawe haya yawe watoto wa Abrahamu.[#3:9 Ling na Yoh 8:33-39. Waisraeli walifikiri kwamba kule kuwa na Abrahamu kama mzee wao kwa nasaba kuliwafanya wawe watu wa Mungu, lakini nasaba ya kiroho ndilo jambo muhimu zaidi (Rom 9:6-8; Gal 3:9).]
10Basi, shoka liko tayari kwenye mizizi ya miti; hivyo, kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni.
11Mimi ninawabatizeni kwa maji kuonesha mmetubu. Lakini anayekuja baada yangu ana nguvu kuliko mimi, nami sistahili hata kubeba viatu vyake. Yeye atawabatizeni kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.[#3:11 “Roho Mtakatifu” ni zawadi ya Mungu kwa watu wake (Yoe 2:28-29; Mate 2:16-18); “moto” watumika hapa kama ishara ya adhabu na uteketezaji wa wakosefu wasiotubu (18:9).]
12Yeye anashika mkononi chombo cha kupuria nafaka, ili aipure nafaka yake; akusanye ngano yake ghalani, na makapi ayachome kwa moto usiozimika.”[#3:12 Aya yenyewe ina lengo la kuonesha “hukumu”; (taz Isa 17:5; Yer 13:24; Amosi 4:12-13).]
13Wakati huo Yesu alitoka Galilaya akafika katika mto Yordani, akamwendea Yohane ili abatizwe naye.
14Lakini Yohane alijaribu kumzuia akisema, “Je, wewe unakuja kwangu? Mimi hasa ndiye ninayehitaji kubatizwa nawe.”
15Lakini Yesu akamjibu, “Acha tu iwe hivyo kwa sasa, maana ndivyo inavyofaa tuyatekeleze yale yote Mungu anayotaka.” Hapo Yohane akakubali.[#3:15 Au, “uadilifu wote” (rejea Mat 5:6,10,20; 6:33).]
16Mara tu Yesu alipokwisha batizwa, alitoka majini; na kumbe mbingu zikafunguka, akaona Roho wa Mungu akishuka kama njiwa na kutua juu yake.
17Sauti kutoka mbinguni ikasema, “Huyu ndiye Mwanangu mpendwa, nimependezwa naye.”[#3:17 Inawezekana pia kuelewa maneno hayo kwa maana ya “Mwanangu wa pekee”. Ling na Zab 2:7; Isa 42:1. Maneno hayo kutoka mbinguni yanamdhihirisha Yesu kuwa Mtumishi wa Mungu (Isa 42:1; 52:13-53:12 ambapo yahusu Mtumishi wa Mwenyezi-Mungu anayeteseka), Mwana wa pekee wa Mungu (Zab 2:7; ling Mwa 22:2). Taz pia Mat 12:18; 17:5; Marko 1:11.]