The chat will start when you send the first message.
1Ilikuwa siku mbili tu kabla ya sikukuu ya Pasaka na ya mikate isiyotiwa chachu. Makuhani wakuu na waalimu wa sheria walikuwa wakitafuta njia ya kumtia Yesu nguvuni kwa hila, wamuue.[#14:1 Sikukuu ya Wayahudi ya kukumbuka kukombolewa utumwani Misri (Kut 12:1-27; Kumb 16:1-8). Sikukuu hiyo iliadhimishwa siku moja tu lakini mara baada ya siku hiyo, sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu iliadhimishwa kwa muda wa siku saba.]
2Lakini walisema, “Tusimtie nguvuni wakati wa sikukuu, watu wasije wakafanya ghasia.”[#14:2 Taz Mat 26:5 maelezo.]
3Yesu alikuwa Bethania, nyumbani kwa Simoni Mkoma. Alipokuwa mezani kula chakula, mama mmoja aliyekuwa na chupa ya alabasta yenye marashi ya nardo safi ya thamani kubwa alikuja, akaivunja hiyo chupa, akammiminia Yesu marashi hayo kichwani.[#14:3 Taz Mat 26:6 maelezo.; #14:3 Jina la jiwe laini ambalo lilitumika kutengenezea vyombo kama chupa n.k., vya kuhifadhi vitu majimaji kama mafuta.; #14:3 Mafuta yaliyotengenezwa kutoka mmea mmoja wa jina hilo.]
4Baadhi ya watu waliokuwa hapo walikasirika, wakajisemea, “Kwa nini kupoteza ovyo marashi haya?
5Yangaliweza kuuzwa kwa fedha kiasi cha dinari 300, wakapewa maskini!” Wakamkemea huyo mama.[#14:5 Hiyo ni kiasi kikubwa sana cha fedha kwa vile dinari moja tu ilikuwa ni mshahara wa kutwa wa kibarua.]
6Lakini Yesu akawaambia, “Mwacheni; kwa nini mnamsumbua? Amenitendea jambo jema.
7Maskini mnao daima pamoja nanyi; mnaweza kuwasaidia wakati wowote mnaopenda. Lakini mimi sitakuwapo pamoja nanyi daima.
8Yeye amefanya alivyoweza; ameupaka mwili wangu marashi kuutayarisha kwa mazishi.[#14:8 Wayahudi walitumia mafuta yenye marashi au manukato kwa kutayarisha miili kabla ya kuizika. Katika mila na desturi za Wayahudi kuzikwa vizuri lilikuwa jambo muhimu na la maana zaidi kupita hata kusaidia maskini.]
9Nawaambieni kweli, popote ulimwenguni Habari Njema itakapohubiriwa, kitendo hiki alichofanya kitatajwa kwa kumkumbuka yeye.”
10Kisha Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili, alikwenda kwa makuhani wakuu ili kumsaliti Yesu.
11Makuhani wakuu waliposikia habari hizo, walifurahi, wakamwahidi kumpa fedha. Basi, Yuda akaanza kutafuta nafasi ya kumsaliti.
12Siku ya kwanza ya sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, wakati ambapo mwanakondoo wa Pasaka huchinjwa, wanafunzi wake walimwuliza, “Wataka tukuandalie wapi karamu ya Pasaka?”
13Basi Yesu akawatuma wawili wa wanafunzi wake akiwaambia, “Nendeni mjini, na humo mtakutana na mwanamume mmoja anayebeba mtungi wa maji. Mfuateni[#14:13 Taz Luka 22:10-11 maelezo.]
14mpaka katika nyumba atakayoingia, mkamwambie mwenye nyumba, ‘Mwalimu anasema: wapi chumba changu ambamo nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?’
15Naye atawaonesha chumba kikubwa ghorofani kilichotayarishwa na kupambwa. Tuandalieni humo.”
16Wanafunzi wakaondoka, wakaenda mjini, wakakuta kila kitu sawa kama Yesu alivyokuwa amewaambia. Wakaandaa karamu ya Pasaka.
17Ilipokuwa jioni, Yesu alifika pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili.
18Walipokuwa mezani wakila, Yesu alisema, “Kweli nawaambieni, mmoja wenu anayekula pamoja nami, atanisaliti.”[#14:18 Zaburi 41:9. Kula pamoja ni ishara ya washiriki kuwa marafiki.]
19Hapo wanafunzi wake wakaanza kuhuzunika, wakamwuliza mmojammoja, “Je, ni mimi?”
20Yesu akawaambia, “Ni mmoja wenu nyinyi kumi na wawili, anayechovya mkate pamoja nami katika bakuli.[#14:20 Yoh 13:18; rejea Zab 41:9. Taz pia Mat 26:23 maelezo.]
21Kweli Mwana wa Mtu anakwenda zake kama Maandiko Matakatifu yanavyosema juu yake; lakini, ole wake mtu yule anayemsaliti Mwana wa Mtu! Ingalikuwa afadhali kwa mtu huyo kama hangalizaliwa!”[#14:21 Mahali penyewe katika Biblia hapatajwi moja kwa moja lakini utenzi wa Mtumishi wa Bwana katika Isa 52:13—53:12 waweza kuhusika.; #14:21 Taz maelezo katika 2:10; 8:31.]
22Walipokuwa wanakula, Yesu alitwaa mkate, akashukuru, akaumega na kuwapa wanafunzi wake akisema, “Twaeni; huu ni mwili wangu.”[#14:22 Licha ya sehemu sambamba katika Injili, taz pia Yoh 6:51-58.]
23Kisha akatwaa kikombe cha divai, akamshukuru Mungu, akawapa; wote wakanywa kutoka kikombe hicho.
24Akawaambia, “Hii ni damu yangu inayothibitisha agano la Mungu, damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi.[#14:24 Kut 24:6-8; Yer 31:31-34; Zek 9:11; Luka 22:20 maelezo; rejea Ebr 9:11—10:18.]
25Kweli nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka siku ile nitakapoinywa upya katika ufalme wa Mungu.”[#14:25 Taz k.m. Mat 8:11 maelezo, na Luka 13:29. Picha ya karamu hutumika kuelezea wokovu ujao na ufalme wa Mungu (rejea Isa 25:6 na Ufu 19:9).]
26Kisha wakaimba wimbo, wakaondoka, wakaenda katika mlima wa Mizeituni.[#14:26 Karamu ya Pasaka kwa desturi ilimalizika kwa wimbo wa Zaburi ya 115 au 118.]
27Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Nyinyi nyote mtakuwa na mashaka nami; maana Maandiko Matakatifu yasema:
‘Nitampiga mchungaji,
nao kondoo watatawanyika.’
28Lakini nikisha fufuka, nitawatangulieni kule Galilaya.”[#14:28 Mat 28:7,10,16; Marko 16:7; rejea Yoh 21:1.]
29Petro akamwambia “Hata kama wote watakuwa na mashaka nawe na kukuacha, mimi sitakukana kamwe!”
30Yesu akamwambia, “Kweli nakuambia, usiku huu, kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.”[#14:30 Kabla ya kipindi au mkesha wa pili wa usiku. Taz Mat 26:75 maelezo.]
31Lakini Petro akasisitiza, “Hata kama ni lazima nife pamoja nawe, sitakuacha kamwe.” Wanafunzi wote pia wakasema vivyo hivyo.
32Basi, wakafika katika bustani iliyoitwa Gethsemane. Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa wakati mimi nasali.”[#14:32 Bustani karibu na Yerusalemu kwenye tambarare ya Mlima wa Mizeituni (rejea Yoh 18:1).]
33Kisha akawachukua Petro, Yakobo na Yohane; akaanza kufadhaika sana na kuhangaika.
34Akawaambia, “Nina huzuni kubwa moyoni hata karibu kufa. Kaeni hapa na kukesha.”[#14:34 Yoh 12:27; rejea Zab 42:5,11; 43:5.]
35Akaenda mbele kidogo, akajitupa chini kifudifudi, akasali kwamba, kama ingewezekana, asiipitie saa hiyo ya mateso.
36Akasema, “Baba yangu, kwako mambo yote yanawezekana. Uniondolee kikombe hiki; lakini isiwe kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe.”[#14:36 Maneno yanayotafsiri neno la Kiaramu “Aba” ambalo ni neno walilotumia watoto kuwaita baba zao (taz pia Rom 8:15; Gal 4:6).; #14:36 Katika A.K. neno “kikombe” lilitumiwa mara kwa mara kimfano kwa maana ya adhabu au kisasi (Isa 51:17; Yer 49:12; Eze 23:32). Hapa kikombe ni mfano wa mateso, na tafsiri hii imesema wazi hivyo, (taz pia Mat 26:39).]
37Kisha akarudi kwa wanafunzi wale watatu, akawakuta wamelala. Basi, akamwuliza Petro, “Simoni, je, umelala? Hukuweza kukesha hata saa moja?”
38Kisha akawaambia, “Kesheni na kusali ili msije mkaingia katika majaribu. Roho inataka, lakini mwili ni dhaifu.”[#14:38 Taz Sira 2:1; Mat 6:13; Luka 11:4; Yak 1:2; 1Pet 1:6; Ufu 2:10; 3:10.; #14:38 Tofauti baina ya roho (nguvu ya Mungu) na mwili (nguvu za kibinadamu) ni jambo ambalo lapatikana pia katika A.K. (k.m. Isa 31:3), na katika A.J. kama vile Rom 8:1-17, wazo la tofauti kati ya roho na mwili linaendelezwa.]
39Akaenda kusali tena akirudia maneno yaleyale.
40Kisha akarudi tena, akawakuta wamelala. Macho yao yalikuwa yamebanwa na usingizi. Hawakujua la kumjibu.
41Alipowajia mara ya tatu aliwaambia, “Mnalala bado na kupumzika? Sasa imetosha! Saa imefika! Mwana wa Mtu anakabidhiwa kwa watu waovu.
42Amkeni, twende zetu. Tazameni, yule atakayenisaliti amekaribia.”
43Yesu alipokuwa bado anasema, Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili, akafika pamoja na umati wa watu wenye mapanga na marungu. Watu hao walikuwa wametumwa na makuhani wakuu, waalimu wa sheria na wazee.
44Msaliti Yuda alikuwa amewapa ishara: “Yule nitakayembusu ndiye; mkamateni na kumpeleka chini ya ulinzi.”
45Yuda alipofika tu, alimwendea Yesu moja kwa moja, akamwambia, “Mwalimu!” Kisha akambusu.[#14:45 Kwa desturi ya Wayahudi kubusu hapa ni ishara ya heshima ambayo aghalabu mwanafunzi alimpa mwalimu wake; taz Mat 26:48-49.]
46Basi, hao watu wakamkamata Yesu, wakamtia nguvuni.
47Mmoja wa wale waliokuwa wamesimama hapo pamoja na Yesu, akachomoa upanga wake, akampiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio.[#14:47 Katika Yoh 18:10 huyo anatajwa wazi kuwa ni Simoni Petro.]
48Yesu akawaambia, “Je, mmekuja na mapanga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyang'anyi?
49Kila siku nilikuwa pamoja nanyi nikifundisha hekaluni, wala hamkunikamata. Lakini sasa lazima Maandiko Matakatifu yatimie.”[#14:49 Luka 19:47; 21:37; Yoh 18:20.]
50Hapo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia.
51Kulikuwa na kijana mmoja aliyekuwa anamfuata Yesu akiwa amevaa shuka. Nao wakajaribu kumkamata.[#14:51-52 Tukio hili linatajwa na Marko peke yake.]
52Lakini yeye akaponyoka, akaiachilia ile shuka, akakimbia uchi.
53Basi, wakampeleka Yesu kwa kuhani mkuu ambapo makuhani wakuu wote, wazee na waalimu wa sheria walikuwa wamekutanika.[#14:53 Kikao hicho bila shaka kilikuwa kikao cha Baraza kuu la Wayahudi (taz aya 55; Mat 26:57).]
54Petro alimfuata Yesu kwa mbali, akaingia ndani ya ua wa kuhani mkuu, akaketi pamoja na walinzi akiota moto.
55Makuhani wakuu na Baraza lote wakatafuta ushahidi wa kumshtaki Yesu wapate kumwua, lakini hawakuupata.
56Watu wengi walitoa ushahidi wa uongo juu ya Yesu, lakini ushahidi wao haukupatana.
57Kisha wengine walisimama, wakatoa ushahidi wa uongo wakisema:
58“Tulimsikia mtu huyu akisema, ‘Nitaliharibu hekalu hili lililojengwa kwa mikono, na kwa siku tatu nitajenga lingine lisilojengwa kwa mikono.’”[#14:58 Marko 15:29; rejea Yoh 2:19-22.]
59Lakini hata hivyo, ushahidi wao haukupatana.
60Basi, kuhani mkuu akasimama katikati yao, akamwuliza Yesu, “Je, hujibu neno? Watu hawa wanashuhudia nini dhidi yako?”
61Lakini yeye akakaa kimya; hakusema hata neno moja. Kuhani mkuu akamwuliza tena, “Je, wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu Mtukufu?”
62Yesu akajibu, “Naam, mimi ndiye. Tena, mtamwona Mwana wa Mtu amekaa upande wa kulia wa yule Bwana Mwenye Nguvu, akija katika mawingu ya mbinguni.”[#14:62 Upande wa kulia ni mahali pa heshima.; #14:62 Jina la sifa la kumtaja Mungu.; #14:62 Dan 7:13; rejea pia Mate 1:9-10.]
63Hapo kuhani mkuu akararua joho lake, akasema, “Tuna haja gani tena ya mashahidi?[#14:63 Ishara ya chukizo, kuonesha kwamba tamko la Yesu ni kufuru na jambo lisilokubaliwa.]
64Mmesikia kufuru yake! Nyinyi mwaonaje?” Wote wakaamua kwamba anastahili kuuawa.
65Basi, baadhi yao wakaanza kumtemea mate, wakamfunika uso, wakampiga na kumwambia, “Bashiri ni nani amekupiga!” Hata watumishi wakamchukua, wakampiga makofi.
66Petro alipokuwa bado chini uani, mmoja wa watumishi wa kike wa kuhani mkuu alikuja.
67Alipomwona Petro akiota moto, alimtazama, akamwambia, “Hata wewe ulikuwa pamoja na Yesu Mnazareti.”
68Lakini Petro akakana, “Sijui, wala sielewi unayosema!” Kisha Petro akaondoka, akaenda nje uani. Hapo jogoo akawika.
69Yule mtumishi alipomwona tena Petro, akaanza tena kuwaambia watu waliokuwa wamesimama hapo, “Mtu huyu ni mmoja wao.”
70Petro akakana tena. Baadaye kidogo, watu waliokuwa wamesimama hapo wakamwambia Petro, “Hakika wewe ni mmoja wao, maana wewe ni Mgalilaya.”
71Lakini Petro akaanza kulaani na kuapa akisema, “Mimi simjui mtu huyu mnayesema habari zake.”
72Hapo jogoo akawika mara ya pili. Basi, Petro akakumbuka jinsi Yesu alivyokuwa amemwambia: “Kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.” Petro akabubujika machozi.