The chat will start when you send the first message.
1Kulipopambazuka, makuhani wakuu walifanya shauri pamoja na wazee, waalimu wa sheria na Baraza lote, wakamfunga Yesu pingu, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato.[#15:1 Yaani Halmashauri kuu ya Wayahudi.; #15:1 Pilato alikuwa mkuu au gavana wa Kiroma katika Yudea, Samaria na Idumea mnamo 26-36 B.K.]
2Pilato akamwuliza Yesu, “Je, wewe ni Mfalme wa Wayahudi?” Yesu akajibu, “Wewe umesema.”[#15:2 Jina la sifa ambalo wale wataalamu wa nyota walilitumia pia kumtambulisha nalo Yesu (Mat 2:2). Huenda baadhi ya Wayahudi walifikiri Yesu alikuwa yule “Masiha” ambaye walikuwa wanamngojea.; #15:2 Jibu ambalo ni kama kitendawili. Laweza kueleweka: “Ndivyo ulivyosema”, au “Wewe ndiwe uliyesema hivyo”. Rejea Mat 27:11.]
3Makuhani wakuu wakamshtaki Yesu mambo mengi.
4Pilato akamwuliza tena Yesu, “Je, hujibu neno? Tazama wanavyotoa mashtaka mengi juu yako.”
5Lakini Yesu hakujibu neno, hata Pilato akashangaa.[#15:5 Isa 53:7; Marko 14:60-61; Luka 23:9.]
6Kila wakati wa sikukuu ya Pasaka, Pilato alikuwa na desturi ya kuwafungulia mfungwa mmoja waliyemtaka.
7Basi, kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Baraba, ambaye alikuwa amefungwa pamoja na waasi wengine kwa kusababisha uasi na mauaji.[#15:7 Si yamkini ni uasi upi unaohusika hapa lakini kulikuwa na maasi kadhaa ya Wayahudi dhidi ya Waroma na jambo hilo ni dhahiri katika Luka 13:1; Mate 5:36-37 na katika maandishi ya mwanahistoria Myahudi Yosefu Flavio.]
8Watu wengi wakamwendea Pilato wakamwomba awafanyie kama kawaida yake.
9Pilato akawauliza, “Je, mwataka niwafungulieni Mfalme wa Wayahudi?”
10Alisema hivyo kwa sababu alijua wazi kwamba makuhani wakuu walimkabidhi Yesu kwake kwa sababu ya wivu.
11Lakini makuhani wakuu wakawachochea watu wamwombe Pilato awafungulie Baraba.
12Pilato akawauliza tena, “Basi, sasa mwataka nifanye nini na mtu huyu mnayemwita Mfalme wa Wayahudi?”
13Watu wote wakapaza sauti tena: “Msulubishe!”
14Lakini Pilato akawauliza, “Kwa nini! Amefanya ubaya gani?” Lakini wao wakazidi kupaza sauti, “Msulubishe!”
15Pilato alitaka kuuridhisha huo umati wa watu; basi, akamwachilia Baraba kutoka gerezani. Akaamuru Yesu apigwe viboko, kisha akamtoa asulubiwe.
16Kisha askari walimpeleka Yesu ndani ukumbini, katika ikulu, wakakusanya kikosi kizima cha askari.[#15:16 Pengine “Pretorio”; ikulu ya gavana, upande wa magharibi mwa mji wa Yerusalemu ambapo yafikiriwa kesi ya Yesu ilifanyika hapo (Mat 27:27).; #15:16 Kawaida kikosi kimoja kilikuwa na askari 600. Si dhahiri kama askari wengi namna hiyo walihusika katika kumzomea na kumdhihaki Yesu au ni wachache tu.]
17Wakamvika vazi la rangi ya zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamwekea kichwani.[#15:17 Au: “joho la rangi ya zambarau”. Yamkini hili lilikuwa joho la kijeshi; lakini kuhusu rangi yenyewe ya zambarau hiyo ilikuwa rangi mahsusi ya mavazi ya kifalme (rejea Mat 27:28).; #15:17 Kwa kuiga taji ya wafalme lakini sasa badala ya maua ni miiba.]
18Wakaanza kumsalimu, “Shikamoo Mfalme wa Wayahudi!”[#15:18 Taz maelezo ya aya ya 2.]
19Wakampiga kichwani kwa mwanzi, wakamtemea mate; wakampigia magoti na kumsujudia.[#15:19 Ishara ya dharau na chuki (Hes 12:14; Kumb 25:9; Yobu 30:10; Isa 50:6).]
20Baada ya kumdhihaki, walimvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka kumsulubisha.
21Walipokuwa njiani, walikutana na mtu mmoja aitwaye Simoni, mwenyeji wa Kurene. Yeye alikuwa baba yao Aleksanda na Rufo, na wakati huo alikuwa akitoka shambani. Basi, wakamlazimisha achukue msalaba wa Yesu.[#15:21 Mat 27:32 na Luka 23:26. Kule kumtambulisha zaidi kama baba yao Aleksanda na Rufo kunaonesha aghalabu kwamba hao watoto wake wawili walikuwa maarufu au walijulikana katika jumuiya ya kwanza ya Wakristo.; #15:21 Ulikuwa mji wa Kigiriki, kaskazini mwa Afrika, sasa ni eneo la Libia.; #15:21 Kwa maneno hayo yawezekana kuona hapa kwamba kutokana na mapigo aliyoyapata Yesu, sasa alikuwa amedhoofika na kuchoka mno.]
22Kisha wakampeleka Yesu mpaka mahali palipoitwa Golgotha, maana yake, mahali pa Fuvu la Kichwa.[#15:22 Neno la Kiaramu lenye maana ya “fuvu” la kichwa.]
23Wakampa divai iliyochanganywa na manemane, lakini yeye alikataa kunywa.[#15:23 Yasemekana ilikuwa kawaida mhalifu aliyepelekwa kuuawa kupewa divai iliyochanganywa na dawa fulani kumpunguzia maumivu yake.]
24Basi, wakamsulubisha, wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura waamue nani angepata nini.[#15:24 Taz Zab 22:18.]
25Ilikuwa saa tatu asubuhi walipomsulubisha.
26Na shtaka dhidi yake lilikuwa limeandikwa, “Mfalme wa Wayahudi.”[#15:26 Taz maelezo ya aya 2.]
27Pamoja naye waliwasulubisha wanyang'anyi wawili, mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto.[#15:27 Baadhi ya hati za kale zina aya 28. “Hapo yakatimia Maandiko Matakatifu yaliyosemwa aliwekwa kundi moja na wahalifu” (Taz Isa 53:12; Luka 22:37).]
29Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana, wakitikisa vichwa vyao na kusema, “Aha! Wewe mwenye kuvunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu![#15:29 Kuonesha dharau au matukano (Taz Yobu 16:4; Zab 22:7; 44:14; 109:25; Isa 37:22; Yer 18:16; 48:27; Sira 12:17-18; 13:7).; #15:29 Marko 14:58; Yoh 2:19; Mate 6:14.]
30Sasa, shuka msalabani ujiokoe mwenyewe!”
31Nao makuhani wakuu pamoja na waalimu wa sheria walimdhihaki wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi!
32Ati yeye ni Kristo, Mfalme wa Israeli! Basi, na ashuke kutoka msalabani ili tuone na kuamini.” Hata watu wale waliosulubiwa pamoja naye walimtukana.
33Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa giza likaikumba nchi yote.[#15:33 Kuhusu “giza”, rejea Amo 8:9. “Nchi yote” labda yahusu nchi yote ya Israeli lakini yaweza kufafanuliwa kwa maana ya “dunia yote.”]
34Saa tisa alasiri Yesu akalia kwa sauti kubwa, akasema, “Eloi, Eloi, lema sabakthani?” Maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”[#15:34 Ni Kiaramu cha Zab 22:1. Rejea maelezo ya Mat 27:46.]
35Baadhi ya watu waliosimama pale waliposikia hivyo, walisema, “Sikiliza! Anamwita Elia.”[#15:35 Kadiri ya A.K. (2Fal 2:9-12) Elia alichukuliwa mbinguni akiwa hai, na iliaminika miongoni mwa Wayahudi kwamba angekuja tena kuwasaidia wakati wa shida. Maneno “Eloi” na neno “Elia” kimatamshi yanafanana. Mal 4:5-6; taz maelezo ya Mat 27:47]
36Mtu mmoja akakimbia, akaichovya sifongo katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe akisema, “Hebu tuone kama Elia atakuja kumteremsha msalabani!”[#15:36 Labda divai hafifu. Labda kitendo hicho hapo awali kilikuwa cha huruma kwa mtu aliyekuwa anateseka lakini kimefafanuliwa baadaye kama cha ukatili kadiri ya Zab 69:21 “Nilipokuwa na kiu walinipa siki.”]
37Yesu akapaza sauti kubwa, akakata roho.
38Basi, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu mpaka chini.[#15:38 Pazia linalotajwa hapa ni lile lililotenga Mahali Patakatifu na Mahali Patakatifu Kabisa hekaluni (Kut 26:31-33; 40:21), ambapo ilifikiriwa kuwa makazi ya Mungu hapa duniani. Maelezo zaidi, taz Ebr 9:8; 10:19 ambapo mwandishi anaelewa kitendo hicho kuwa ni fursa ya binadamu wote kumwendea Mungu bila kizuizi.]
39Jemadari mmoja aliyekuwa amesimama mbele yake alipoona kwamba Yesu alikata roho namna hiyo, akasema, “Kweli mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu!”[#15:39 Katika jeshi la Kiroma jemadari alikuwa mkuu wa kikosi cha askari mia moja.; #15:39 Baadhi ya hati za kale zina: alilia na kukata roho.; #15:39 Kwa tamko hilo ambalo limesemwa na mtu asiye Myahudi; Injili imefikia kilele chake.]
40Walikuwako pia wanawake waliotazama kwa mbali, miongoni mwao akiwa Maria Magdalene, Salome, na Maria mama wa kina Yakobo mdogo na Yose.[#15:40 Magdalene yaani “wa Magdala”, mji ulio upande wa magharibi wa ziwa Galilaya.; #15:40 Bila shaka hao Yakobo na Yose walikuwa watu waliojulikana kwa jumuiya changa ya Wakristo.]
41Hawa walimfuata Yesu alipokuwa Galilaya na kumtumikia. Kulikuwa na wanawake wengine wengi waliokuja Yerusalemu pamoja naye.[#15:41 Luka 8:2 maelezo.]
42Wakati wa jioni ulikuwa umekwisha fika. Hiyo ilikuwa siku ya Maandalio, yaani siku inayotangulia Sabato.
43Hapo akaja Yosefu mwenyeji wa Arimathaya, mjumbe wa Baraza Kuu, aliyeheshimika sana. Yeye pia alikuwa anatazamia kuja kwa ufalme wa Mungu. Basi, alimwendea Pilato bila woga, akaomba apewe mwili wa Yesu.[#15:43 Mahali penyewe hapajulikani, lakini baadhi ya wataalamu wa mambo ya Biblia wanahisi ni katika sehemu ya kilima yapata kilomita 15 mashariki mwa Yopa.; #15:43 Ilikuwa desturi ya Waroma kuacha mwili wa mhalifu aliyesulubiwa msalabani mpaka uoze, lakini iliwezekana kuwaruhusu jamaa za aliyesulubiwa kuondoa maiti.]
44Pilato alishangaa kusikia kwamba Yesu alikuwa amekwisha kufa. Basi, akamwita jemadari, akamwuliza kama Yesu alikuwa amekufa kitambo.
45Pilato alipoarifiwa na huyo jemadari kwamba Yesu alikuwa amekwisha kufa, akamruhusu Yosefu kuuchukua mwili wake.
46Hapo Yosefu akanunua sanda ya kitani, akauteremsha chini huo mwili, akauzungushia sanda. Akauweka katika kaburi lililokuwa limechongwa mwambani, kisha akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango.[#15:46 Taz Mat 27:60 maelezo.]
47Nao Maria Magdalene na Maria mama yake Yose walipaona hapo alipolazwa.