Marko 16

Marko 16

Kufufuka kwa Yesu

(Mat 28:1-8; Luka 24:1-12; Yoh 20:1-10)

1Baada ya siku ya Sabato, Maria Magdalene, Salome na Maria mama yake Yakobo walinunua manukato ili wakaupake mwili wa Yesu.[#16:1 Yaani baada ya jua kutua siku ya Jumamosi.]

2Basi, alfajiri na mapema siku ya Jumapili, walifika kaburini, jua lilipoanza kuchomoza.

3Nao wakawa wanaambiana, “Nani atakayetuondolea lile jiwe mlangoni mwa kaburi?”

4Lakini walipotazama, waliona jiwe limekwisha ondolewa. (Nalo lilikuwa kubwa mno.)

5Walipoingia kaburini, walimwona kijana mmoja aliyevaa vazi jeupe, ameketi upande wa kulia; wakashangaa sana.[#16:5 Picha kawaida ya kusema juu ya malaika (rejea Mat 28:2).]

6Lakini huyo kijana akawaambia, “Msishangae. Mnamtafuta Yesu wa Nazareti aliyesulubiwa. Amefufuka, hayumo hapa. Tazameni mahali walipokuwa wamemlaza.[#16:6 Taz maelezo ya Mat 2:23.]

7Nendeni mkawaambie wanafunzi wake pamoja na Petro ya kwamba anawatangulieni kule Galilaya. Huko mtamwona kama alivyowaambieni.”[#16:7 Kaskazini mwa Palestina. Taz ramani.; #16:7 Taz 14:28; Mat 26:32; rejea Yoh 21:1-22.]

8Basi, wakatoka pale kaburini mbio, maana walitetemeka kwa hofu na kushangaa. Hawakumwambia mtu yeyote kitu, kwa sababu waliogopa mno.[#16:8 Hapa yaishia Injili ya Marko kama tulivyoipokea kutoka katika hati za mkono za awali kabisa. Hata hivyo aya za 9-20 zimo katika hati nyingi za kale ambazo zatoa muhtasari wa Yesu kuwatokea wanafunzi wake baada ya kufufuka kwake kama inavyotajwa katika Injili nyingine, na kugusia baadhi ya matukio yanayotajwa katika Matendo.; #16:8 Baadhi ya hati za kale humalizia Injili hii na aya hii ya 8.]

Yesu anamtokea Maria Magdalene

(Mat 28:9-10; Yoh 20:11-18)

[

9Yesu alipofufuka mapema Jumapili, alijionesha kwanza kwa Maria Magdalene, ambaye Yesu alikuwa amemtoa pepo wabaya saba.[#16:9-20 Aya hizi hazipo katika hati za awali kabisa na baadhi ya tafsiri za kale.; #16:9 Injili zote nne zinaafikiana kwamba wa kwanza kumwona Yesu baada ya kufufuka kwake alikuwa mwanamke au wanawake (Mat 28:5-9; Luka 24:2-8; Yoh 20:14-16).; #16:9 Rejea Luka 8:2.]

10Maria Magdalene akaenda, akawajulisha wale waliokuwa pamoja na Yesu, na wakati huo walikuwa wanaomboleza na kulia.

11Lakini waliposikia ya kwamba Yesu yu hai na kwamba Maria Magdalene amemwona, hawakuamini.

Yesu anawatokea wanafunzi wawili

(Luka 24:13-35)

12Baadaye Yesu aliwatokea wanafunzi wawili akiwa na sura nyingine. Wanafunzi hao walikuwa wanakwenda shambani.

13Nao pia wakaenda, wakawaambia wenzao. Hata hivyo hawakuamini.

Wanafunzi wanatumwa

(Mat 28:16-20; Luka 24:36-49; Yoh 20:19-23; Mate 1:6-8)

14Mwishowe Yesu aliwatokea wanafunzi kumi na mmoja walipokuwa pamoja mezani. Akawakemea sana kwa sababu ya kutoamini kwao na ukaidi wao, maana hawakuwaamini wale waliokuwa wamemwona baada ya kufufuka.

15Basi, akawaambia, “Nendeni ulimwenguni kote mkahubiri Habari Njema kwa kila mtu.

16Anayeamini na kubatizwa ataokolewa. Asiyeamini atahukumiwa.

17Na ishara hizi zitaandamana na wale wanaoamini: kwa jina langu watatoa pepo na watasema kwa lugha mpya.[#16:17 Taz Mate 2:4; 10:46; 19:6; 1Kor 12:10,28; 13:1; 14:1-6.]

18Wakishika nyoka au wakinywa kitu chochote chenye sumu, hakitawadhuru. Watawawekea wagonjwa mikono, nao watapona.”[#16:18 Rejea Mate 28:3-6.]

Yesu anapaa mbinguni

(Luka 24:50-53; Mate 1:9-11)

19Basi, Bwana Yesu alipokwisha sema nao, akachukuliwa mbinguni, akaketi upande wa kulia wa Mungu.[#16:19 Mahali pa heshima na uwezo (taz 12:36; 14:62).]

20Wanafunzi wakaenda wakihubiri kila mahali. Bwana akafanya kazi pamoja nao na kuimarisha ujumbe huo kwa ishara zilizoandamana nao.][#16:20 Baadhi ya hati za kale zinajumlishia hapa neno “Amina”.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania