The chat will start when you send the first message.
1Wakati huo, umati mkubwa wa watu ulikusanyika tena, na hawakuwa na chakula. Basi, Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia,
2“Nawaonea huruma watu hawa kwa sababu wamekuwa nami kwa siku tatu, wala hawana chakula.
3Nikiwaacha waende nyumbani wakiwa na njaa watazimia njiani, maana baadhi yao wametoka mbali.”
4Wanafunzi wake wakamwuliza, “Hapa nyikani itapatikana wapi mikate ya kuwashibisha watu hawa wote?”
5Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakamjibu, “Saba.”
6Basi, akawaamuru watu wakae chini. Akaitwaa ile mikate saba, akamshukuru Mungu, akaimega, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu, nao wakawagawia.
7Walikuwa pia na visamaki vichache. Yesu akavibariki, akaamuru vigawiwe watu vilevile.[#8:7 Kulingana na desturi ya Kiyahudi aliye mkubwa katika jamii au wakati wa chakula alichukua mkate na kusema: “Shukrani kwako e Bwana, Mungu wetu, mtawala wa ulimwengu unayezalisha mkate wa dunia”, na waliopo waliitikia “Amina”. Kisha aligawa mkate.]
8Watu wakala, wakashiba. Wakakusanya makombo wakajaza vikapu saba.
9Nao waliokula walikuwa watu wapatao 4,000. Yesu akawaaga,
10na mara akapanda mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda wilaya ya Dalmanutha.[#8:10 Mahali ambapo hapajulikani sasa ila kwa kukisia ni upande wa magharibi wa ziwa Galilaya. Baadhi ya hati zina “Magadani” na nyingine “Magdala” (taz Mat 15:39).]
11Mafarisayo walikuja, wakaanza kujadiliana na Yesu. Kwa kumjaribu, wakamtaka afanye ishara kutoka mbinguni.[#8:11 Mat 12:38; Luka 11:16; Yoh 6:30. “Kutoka mbinguni”: Yaani kutoka kwa Mungu; taz Mat 16:1. Hapa ni dhahiri kwamba lengo la ishara hiyo ni kuonesha kwamba Yesu anayo idhini kutoka kwa Mungu.]
12Yesu akahuzunika rohoni, akasema, “Mbona kizazi hiki kinataka ishara? Kweli nawaambieni, kizazi hiki hakitapewa ishara yoyote.”
13Basi, akawaacha, akapanda tena mashua, akaanza safari kwenda ng'ambo ya pili ya ziwa.
14Wanafunzi walikuwa wamesahau kuchukua mikate; walikuwa na mkate mmoja tu katika mashua.
15Yesu akawaonya, “Angalieni sana! Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode.”[#8:15 Kitu ambacho kikiwekwa katika donge la kutengeneza mkate hulipenya na kulifanya lichache na kuumuka. Chachu inatumika hapa kama mfano wa uovu uliofichika ambao hupotosha kwa siri (taz pia 1Kor 5:6; Gal 5:9).]
16Wanafunzi wakaanza kujadiliana wao kwa wao, “Anasema hivyo kwa kuwa hatuna mikate.”
17Yesu alitambua hayo, akawaambia, “Mbona mnajadiliana juu ya kutokuwa na mikate? Je, bado hamjafahamu, wala hamjaelewa? Je, mioyo yenu ni mizito?
18Je, mnayo macho na hamwoni? Mnayo masikio na hamsikii? Je, hamkumbuki[#8:18 Mara nyingi manabii waliwakaripia Waisraeli kwamba ni watu waliokuwa vipofu na viziwi rohoni (Yer 5:21; Eze 12:2; rejea Marko 4:12).]
19wakati ule nilipoimega ile mikate mitano na kuwapa watu 5,000? Mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki.” Wakamjibu, “Kumi na viwili.”
20“Na nilipoimega ile mikate saba na kuwapa watu 4,000, mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki?” Wakamjibu, “Saba.”
21Basi, akawaambia, “Na bado hamjaelewa?”
22Yesu alifika Bethsaida pamoja na wanafunzi wake. Huko watu wakamletea kipofu, wakamwomba amguse.
23Yesu akamshika huyo kipofu mkono, akampeleka nje ya kijiji. Akamtemea mate machoni, akamwekea mikono, akamwuliza, “Je, unaweza kuona kitu?”[#8:23 Labda ambako hakukuwa na watu wengi. Baada ya kumponya anamwambia asirudi mjini (8:26).; #8:23 Taz maelezo ya 7:33. Taz pia Yoh 9:6.]
24Huyo kipofu akatazama, akasema, “Ninawaona watu wanaoonekana kama miti inayotembea.”[#8:24-25 Hatuwezi kuelewa sasa kwa nini kitendo cha kumponya huyo kipofu kinafanyika katika hatua mbili.]
25Kisha Yesu akamwekea tena mikono machoni, naye akakaza macho, uwezo wake wa kuona ukamrudia, akaona kila kitu sawasawa.
26Yesu akamwambia aende zake nyumbani na kumwamuru, “Usirudi kijijini!”[#8:26 Kwa maana ya kumzuia asije akatangaza habari za Yesu; jambo ambalo ni la kawaida katika Injili ya Marko. Baadhi ya hati za kale zinaongeza hapo: “Usimwambie mtu yeyote”.]
27Kisha Yesu na wanafunzi wake walikwenda katika vijiji vya Kaisarea Filipi. Walipokuwa njiani, Yesu aliwauliza wanafunzi wake, “Watu wanasema mimi ni nani?”[#8:27 Mji kaskazini mwa ziwa Galilaya, eneo ambamo kwa wingi waliishi watu wasio Wayahudi. Mji huo ulijengwa na Herode Filipo kwa heshima ya mtawala mkuu wa Waroma yaani Kaisari.]
28Wakamjibu, “Wengine wanasema wewe ni Yohane Mbatizaji, wengine Elia na wengine mmojawapo wa manabii.”[#8:28 Marko 6:14-15; Luka 9:7-8.; #8:28 Rejea 1Fal 17—2Fal 2 Wayahudi walitazamia kurudi kwake kabla ya ile siku ya Bwana (Mal 4:5-6); taz pia Mat 16:14.]
29Naye akawauliza, “Na nyinyi je, mnasema mimi ni nani?” Petro akamjibu, “Wewe ndiwe Kristo.”[#8:29 Rejea Yoh 6:68-69. Kristo ni tafsiri ya Kigiriki ya jina la Kiebrania “Masiha”, maana yake “Aliyepakwa mafuta”, yaani aliyewekwa wakfu na Mungu kwa ajili ya wadhifa au kazi fulani.]
30Kisha Yesu akawaonya wasimwambie mtu yeyote habari zake.[#8:30 Au, akawakaripia. Taz Marko 1:34 maelezo.]
31Yesu alianza kuwafundisha wanafunzi wake kwamba ni lazima Mwana wa Mtu apatwe na mateso mengi na kukataliwa na wazee na makuhani wakuu na waalimu wa sheria. Kwamba atauawa, na baada ya siku tatu atafufuka.[#8:31 Taz 2:10. Hapa mkazo uko katika mateso yake.]
32Yesu aliwaambia jambo hilo waziwazi. Hapo, Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea.
33Lakini Yesu akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro akisema, “Ondoka mbele yangu Shetani! Mawazo yako si ya kimungu ila ni ya kibinadamu.”
34Kisha akauita umati wa watu pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, “Kama mtu yeyote anataka kuwa mfuasi wangu, lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate.[#8:34 Au, ajiache mwenyewe. Taz 14:30-31,72; vilevile Mat 10:38; Luka 14:27.; #8:34 Ulikuwa chombo cha kuwatesa waliotakiwa kuuawa (Taz 15:21,30,32). Taz pia matumizi yake katika Rom 6:2-11; Gal 2:19; 6:14; Kol 3:3-5.]
35Maana mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza, lakini mtu anayepoteza maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Habari Njema, atayaokoa.
36Je, kuna faida gani mtu kuupata ulimwengu wote na kuyapoteza maisha yake?
37Ama mtu atatoa kitu gani badala ya maisha yake?
38Mtu yeyote katika kizazi hiki kiovu na kisicho na uaminifu kwa Mungu, anayenionea aibu mimi na mafundisho yangu, Mwana wa Mtu atamwonea aibu mtu huyo, wakati atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.”[#8:38 Kama vile Mat 12:39.]