Nehemia 6

Nehemia 6

Njama za kumwangamiza Nehemia

1Kisha Sanbalati, Tobia, Geshemu, Mwarabu na adui zetu wengine, waliposikia kuwa tumemaliza ujenzi wa ukuta na kwamba hakuna mapengo yoyote (ingawa tulikuwa bado hatujaweka milango ya malango),

2Sanbalati na Geshemu walituma ujumbe kwangu wakisema, “Na tukutane kwenye kijiji kimojawapo cha tambarare ya Ono.” Lakini walikusudia kunidhuru.[#6:2 Mji huu na tambarare yake ulikuwa katika eneo la kaskazini-magharibi kabisa ya nchi ya Yuda, na hivyo ni sehemu ya mbali zaidi kabla ya kuacha nchi ya Yuda.]

3Basi, nikawapelekea wajumbe, nikisema, “Kazi ninayoifanya ni muhimu sana. Hivyo siwezi kuja kwenu ili kazi isije ikasimama.”

4Waliendelea kunitaka niende kwao mara nne, lakini nikawapa jibu lilelile.

5Mara ya tano, Sanbalati akanitumia barua ya hadhara kwa njia ya mjumbe wake.

6Na barua yenyewe iliandikwa ifuatavyo:

“Kuna habari zilizoenezwa miongoni mwa mataifa jirani, na Geshemu anathibitisha habari hizi, kuwa wewe pamoja na Wayahudi wenzako mnakusudia kuasi. Hii ndiyo sababu mnaujenga upya ukuta. Kulingana na habari hizo, wewe unakusudia kuwa mfalme wao.

7Ili kuthibitisha wazo lako, umejiwekea manabii mjini Yerusalemu ili watangaze kuwa ‘Kuna mfalme katika nchi ya Yuda’. Taarifa hii ataarifiwa mfalme Artashasta. Hivyo nashauri wewe na mimi tukutane na kuzungumzia jambo hili.”

8Nami nikampelekea ujumbe: “Hakuna jambo kama hilo. Habari hizo umezibuni wewe mwenyewe.”

9Walifanya hivyo ili kututisha wakifikiri: “Hawataendelea na kazi, kwa hiyo, hakuna litakalotendeka.” Nikamwomba Mungu wangu nikisema, “Lakini sasa, ee Mungu, nakuomba unipe nguvu.”

10Nilipokwenda nyumbani kwa Shemaya, mwana wa Delaya mwana wa Mehetabeli, ambaye hakuruhusiwa kutoka nyumbani, aliniambia, “Twende tukutane katika nyumba ya Mungu na milango yake tuifunge kwa sababu leo usiku wanakuja kukuua.”[#6:10 Lawi 9:1-22; Ebr 9:6-7. Maneno “Katika nyumba ya Mungu” yamkini yanamaanisha lile eneo takatifu kabisa ambalo ni kuhani mkuu peke yake aliruhusiwa kuingia.]

11Lakini mimi nikajiuliza moyoni, “Je, mtu kama mimi, ana haja ya kukimbia? Mtu kama mimi anahitaji kuingia hekaluni kusudi apate kuishi? Kamwe sitaingia hekaluni.”[#6:11-19 Ingawa upinzani dhidi ya ujenzi wa ukuta wa Yerusalemu ulikoma baada ya kazi hiyo kukamilika bado tishio dhidi ya Nehemia liliendelea.]

12Kwa bahati nzuri, niling'amua kuwa alikuwa hajatumwa na Mungu, bali alikuwa amekodishwa na Tobia na Sanbalati atangaze mabaya dhidi yangu.

13Alikuwa amekodishwa kunitishia nami nifanye dhambi. Na kwa njia hii wangepata mwanya wa kuniharibia jina langu ili kushusha hadhi yangu.[#6:13 Yaani, kwa vile Nehemia hakuwa kuhani ingekuwa makosa kwake kuingia ndani hekaluni.]

14Nikamwomba Mungu nikisema, “Ee Mungu, kumbuka yote waliyotenda Tobia na Sanbalati, hata yule Noadia, nabii mwanamke, na manabii wengine waliotaka kunifanya niogope.”[#6:14 Hili ni ombi la tatu la kulaani (taz 4:4-5 maelezo).]

Kazi inakamilika

15Basi, ukuta ulikamilika siku ya ishirini na tano ya mwezi wa Eluli; nayo ilichukua muda wa siku hamsini na mbili.[#6:15 Huu ni mwezi wa sita katika kalenda ya Wayahudi (yapata tangu katikati ya mwezi Agosti mpaka katikati ya mwezi Septemba kadiri ya kalenda yetu).]

16Maadui zetu katika mataifa jirani, waliposikia kuwa kazi tumeimaliza, waliogopa na kuona aibu sana; kwani walijua hakika kuwa kazi hii ilikamilika kwa msaada wa Mungu wetu.

17Wakati huu wote, viongozi wa Wayahudi walikuwa wakiandikiana na Tobia.

18Wengi miongoni mwa Wayahudi walishirikiana naye kutokana na kiapo chao kwani alikuwa mkwe wa Shekania, mwana wa Ara. Zaidi ya yote, Yehohanani, mwanawe, alikuwa amemwoa binti Meshulamu, mwana wa Berekia.

19Pia wakanisimulia matendo mema ya Tobia, na habari zangu wakawa wanampelekea. Naye akawa ananiandikia barua ili kunitisha.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania