The chat will start when you send the first message.
1Anayetafuta yake tu hujitenga na wenzake;
hukasirika akipewa shauri lolote jema.
2Mpumbavu hapendezwi na busara;
kwake cha maana ni maoni yake tu.
3Ajapo mwovu huja pia dharau;
pamoja na aibu huja fedheha.
4Maneno yaweza kuwa chemchemi ya hekima;[#18:4 Kama methali hiyo ikichukuliwa hapa kwa maana iliyoko katika 13:14 ni dhahiri kwamba yanafaa kwa maisha. Sura hii inalipa suala la kuongea nafasi yake: maneno ya mpumbavu (18:6-8,13); nguvu ya maneno (18:20-21).]
yenye kilindi kama bahari, kama kijito kinachobubujika.
5Si vizuri kumpendelea mtu mwovu,[#18:5 Methali hii inahusu maamuzi katika mahakama (taz Meth 17:15; rejea Lawi 19:15; Kumb 1:17; Yobu 13:7-8; Meth 24:23; Isa 5:23).]
na kumnyima haki mtu mwadilifu.
6Maneno ya mpumbavu huleta ugomvi;
kila anachosema husababisha adhabu.
7Kinywa cha mpumbavu humwangamiza mwenyewe;
mdomo wake ni mtego wa kumnasa yeye mwenyewe.
8Maneno ya msengenyaji ni kama kitoweo kitamu;[#18:8 Rejea Meth 26:22. Taz pia 10:8-14 maelezo.]
ambacho hushuka moja kwa moja mpaka tumboni.
9Mtu mvivu kazini mwake
ni ndugu yake mharibifu.
10Jina la Mwenyezi-Mungu ni mnara imara;[#18:10 Mwenyezi-Mungu mara kwa mara husemwa kuwa ni ngome, au mnara wa kuwakinga watu (Zab 18:1-2; 91:2). Lakini matajiri wanafikiri utajiri wao ni usalama wao (Meth 18:11).]
mwadilifu huukimbilia akawa salama.
11Lakini tajiri hudhani mali ni ngome yake;
anafikiri hayo ni ukuta mrefu unaomlinda.
12Majivuno ya moyoni huleta maangamizi,[#18:12 Kuhusu yawapatao wenye tabia hiyo rejea Meth 16:18.]
lakini unyenyekevu huleta heshima.
13Kujibu kabla ya kusikiliza
ni upumbavu na jambo la aibu.
14Roho ya mtu huweza kustahimili ugonjwa,
lakini ukiwa umevunjika moyo, utastahimilije?
15Mtu mwenye akili hujipatia maarifa,
sikio la mwenye busara hutafuta maarifa.
16Zawadi humfungulia mtu milango;
huweza kumfikisha mtu mbele ya mkuu.
17Ajiteteaye kwanza huonekana msema kweli,
mpaka hapo mpinzani wake atakapoanza kumhoji.
18Kura hukomesha ubishi;
huamua kati ya wakuu wanaopingana.
19Ndugu aliyeudhiwa ni mgumu kuliko mji wa ngome;
magomvi hubana kama makufuli ya ngome.
20Maneno ya mtu yaweza kumshibisha;
hutosheka kwa matokeo ya maneno yake.
21Ulimi una nguvu ya kufanya hai na kuua;
wanaopenda kuutumia watakula matunda yake.
22Anayempata mke amepata bahati njema;[#18:22 Kuhusu mke kama zawadi kutoka kwa Mungu taz 19:14b.]
hiyo ni fadhili kutoka kwa Mwenyezi-Mungu.
23Maskini huomba kwa unyenyekevu,
bali tajiri hujibu kwa ukali.
24Marafiki wengi waweza kumwangusha mtu,
lakini wapo marafiki waaminifu kuliko ndugu.