The chat will start when you send the first message.
1Divai huleta dhihaka na kileo huleta ugomvi;
yeyote anayevutiwa navyo hana hekima.
2Ghadhabu kali ya mfalme ni kama simba angurumaye;[#20:2 Si dhahiri kama msemo huu unasema hivyo kwa jumla bila kugusia kwamba ni hasira halali au la. Katika 19:12; 20:8,26,28 inahusu mfalme aliye mwema.]
anayemkasirisha anayahatarisha maisha yake.
3Ni jambo la heshima kuepa ugomvi;
wapumbavu ndio wanaogombana.
4Mvivu halimi wakati wa kulima;
wakati wa mavuno atatafuta asipate chochote.
5Fikira za mtu zimefichika kama kilindi cha maji;
lakini mtu mwenye busara ajua kuzichota humo.
6Watu wengi hujivunia kuwa wema,
lakini mwaminifu wa kweli apatikana wapi?
7Mtu mwadilifu akiishi kwa unyofu;
watoto wake atakaowaacha watabarikiwa.
8Mfalme mwema aketipo kutoa hukumu,
huupepeta uovu wote kwa macho yake.
9Nani athubutuye kusema: “Nimeutakasa moyo wangu;
mimi nimetakasika dhambi yangu?”
10Mizani ya udanganyifu na vipimo vya udanganyifu,
vyote ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu.
11Hata mtoto hujulikana kwa matendo yake,
kama tabia yake ni njema na aminifu.
12Sikio lisikialo na jicho lionalo,
yote mawili kayafanya Mwenyezi-Mungu.
13Usipende kulala tu usije ukawa maskini;
uwe macho nawe utakuwa na chakula kingi.
14“Hakifai, hakifai”, mnunuzi hulalamika,
lakini akiondoka hujisifu amepunguziwa bei.
15Kuna dhahabu na wingi wa mawe ya thamani kubwa;
lakini cha thamani kubwa zaidi ni maneno ya busara!
16Mtu akiahidi mbele yako kumdhamini mgeni,
chukua nguo yake;
mfanye awajibike kwa kuwadhamini wageni.
17Chakula kipatikanacho kwa udanganyifu ni kitamu,
lakini baadaye huwa kama mchanga kinywani.
18Mipango mizuri hufanyika kwa kushauriana;
ukitaka kuanza vita lazima kutafakari kwanza.
19Mpiga domo hafichi siri,
kwa hiyo mwepe mtu wa kuropoka.
20Anayemlaani baba yake au mama yake,[#20:20 Taz 10:13; 14:3; 19:29.]
mwanga wa uhai wake utazimwa kama taa gizani.
21Mali iliyopatikana kwa haraka mwanzoni,
haitakuwa ya heri mwishoni.
22Usiseme, “Nitalipiza ubaya niliotendewa.”
Mtegemee Mwenyezi-Mungu naye atakusaidia.
23Mizani ya udanganyifu ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu,
na vipimo visivyo halali ni kitu kibaya.
24Hatua za mtu huongozwa na Mwenyezi-Mungu;
awezaje binadamu kujua njia ya kwenda?
25Ni hatari kusema kwa mzaha “Usiahidi kumpa Mungu kitu bila kufikiri,
la sivyo utaanza kusikitika baada ya nadhiri yako.”
26Mfalme mwenye busara huwapepeta waovu;
huwaadhibu bila huruma.
27Dhamiri ya mtu ni taa ya Mwenyezi-Mungu;
huchunguza nafsi yake mtu mpaka ndani kabisa.
28Wema na uaminifu humkinga mfalme;
utawala wake huimarishwa kwa uadilifu.
29Fahari ya vijana ni nguvu zao,
uzuri wa vikongwe ni mvi za uzee.
30Mapigo yanayoumiza ni dawa ya kuondoa uovu;
viboko husafisha nafsi mpaka ndani kabisa.