Methali 3

Methali 3

Mawaidha kwa vijana

1Mwanangu, usiyasahau mafundisho yangu,

bali kwa moyo wako uzishike amri zangu.

2Maana yatakupa wingi wa siku,

maisha marefu na fanaka kwa wingi.

3Utii na uaminifu visitengane nawe.

Vifunge shingoni mwako;

viandike moyoni mwako.

4Hivyo utakubalika na kusifika,

mbele ya Mungu na mbele ya wanadamu.

5Mtumaini Mwenyezi-Mungu kwa moyo wako wote,

wala usitegemee akili zako mwenyewe.

6Umtambue Mungu katika kila ufanyalo,

naye atazinyosha njia zako.

7Usijione wewe mwenyewe kuwa mwenye hekima;[#3:7 Onyo la namna hiyohiyo liko katika Rom 12:16. Taz pia mstari wa pili wa sura 2:5. Lengo la onyo ni kukwepa kufikiri kwamba una hekima na kusahau kwamba hekima yatoka kwa Mungu.]

mche Mwenyezi-Mungu na kujiepusha na uovu.

8Hiyo itakuwa dawa mwilini mwako,

na kiburudisho mifupani mwako.

9Mheshimu Mwenyezi-Mungu kwa mali yako,

na kwa malimbuko ya mazao yako yote.

10Hapo ghala zako zitajaa nafaka,

na mapipa yako yatafurika divai mpya.

11Mwanangu, usidharau adhabu ya Mwenyezi-Mungu,[#3:11 Mungu anapotuadhibu ili kuturudi ni kwa faida yetu (Yobu 5:17; Rev 3:19). Aya hii imenukuliwa katika Ebr 12:5-6 kulingana na tafsiri ya Kigiriki ya Septuajinta (LXX).]

wala usiudhike kwa maonyo yake;

12maana Mwenyezi-Mungu humwonya yule ampendaye,

kama baba amwonyavyo mwanawe mpenzi.

13Heri mtu anayegundua hekima,

mtu yule anayepata ufahamu.

14Hekima ni bora kuliko fedha,[#3:14-18 Aya hizi ni utenzi ambao unasema kwa kifupi faida zinazotokana na Hekima: maisha marefu, utajiri, heshima, usalama na furaha. Mti wa uhai hutumika katika Biblia kama mfano wa baraka za Mwenyezi-Mungu (Mwa 2:9; Ufu 22:2).]

ina faida kuliko dhahabu.

15Hekima ina thamani kuliko johari,

hamna unachotamani kiwezacho kulingana nayo.

16Kwa mkono wake wa kulia Hekima atakupa maisha marefu;

kwa mkono wake wa kushoto atakupa mali na heshima.

17Njia zake ni za kupendeza,

zote zaelekea kwenye amani.

18Hekima ni mti wa uhai kwa wote wampatao;

wana heri wote wanaoshikamana naye.

19Kwa hekima Mwenyezi-Mungu aliweka misingi ya dunia,[#3:19 Katika 8:24 tunaambiwa kuwa Hekima alikuwako na Mungu tangu mwanzo kabla ya kuumbwa ulimwengu (taz 28:24-26). Wazo kwamba Hekima alikuwa pamoja na Mungu lakini alikuwa tofauti na Mungu huenda lilichangia wazo lingine la Ukristo la kumwona Kristo kuwa ni mwana wa Mungu ambaye naye pia alikuwa pamoja na Mungu tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu (Yoh 1:1-3; Kol 1:15-17). Rejea pia Ufu 3:14.]

kwa akili aliziimarisha mbingu.

20Kwa maarifa yake vilindi vilipasuka,[#3:20 Watu wa kale waliamini kwamba dunia ilikuwa bapa na sio mviringo kama tujuavyo leo, na chini ya dunia kulikuwa maji mengi sana na juu ya anga ambalo lilifikiriwa kuwa kama bakuli kubwa sana lilofudikizwa kulikuwa na maji pia. Mvua na theluji vilianguka kutoka huko wakati Mungu alipofungua madirisha yake (Mwa 7:1; Zab 78:23).]

na mawingu yakadondosha umande.

21Mwanangu, zingatia hekima safi na busara;

usiviache vitoweke machoni pako,

22navyo vitakuwa uhai nafsini mwako,

na pambo zuri shingoni mwako.

23Hapo utaweza kwenda zako kwa usalama,

wala mguu wako hautajikwaa.

24Ukiketi hutakuwa na hofu;

ukilala utapata usingizi mtamu.

25Usiogope juu ya tishio la ghafla,

wala shambulio kutoka kwa waovu,

26Maana Mwenyezi-Mungu ndiye atakayekutegemeza;

atakuepusha usije ukanaswa mtegoni.

27Usimnyime mtu anayehitaji msaada,[#3:27 Katika 3:27-32 mwandishi anatilia mkazo umuhimu wa kuwa na uhusiano mwema na watu wengine. Mtu mwenye hekima huwatendea wengine mema (Gal 6:10; 1Yoh 3:17-18).]

ikiwa unao uwezo wa kufanya hivyo.

28Usimwambie jirani yako aende zake hadi kesho,

hali wewe waweza kumpa anachohitaji leo.

29Usipange maovu dhidi ya jirani yako,

anayeishi karibu nawe bila wasiwasi.

30Usigombane na mtu bila sababu

ikiwa hajakudhuru kwa lolote.

31Usimwonee wivu mtu mkatili,

wala usiige mwenendo wake.

32Maana waovu ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu;

lakini yeye huwafanya marafiki zake wale walio wanyofu.

33Mwenyezi-Mungu huapiza nyumba za waovu,

lakini huyabariki makao ya waadilifu.

34Yeye huwadharau wenye dharau,

lakini huwafadhili wanyenyekevu.

35Wenye hekima watavuna heshima,

lakini wapumbavu watapata fedheha.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania