The chat will start when you send the first message.
1Sikilizeni! Hekima anaita!
Busara anapaza sauti yake!
2Juu penye mwinuko karibu na njia,
katika njia panda ndipo alipojiweka.
3Karibu na malango ya kuingilia mjini,[#8:1-3 Mafungu hayo ya maneno yanataja mahali ambapo katika mazingira ya kale ya mwandishi ndiko kulikokuwa na mkusanyo wa watu wengi. Kwa maneno hayo mwandishi bila shaka alitaka kusema kwamba mwito wa Hekima ni kwa watu wote. Neno “Busara” (aya 1b) ni neno lingine sambamba na hekima; maneno mengine yanayotumika mara nyingi kwa maana hiyohiyo ni: ujuzi, maarifa, akili, utambuzi, n.k.]
mahali wanapoingia watu anaita kwa sauti:
4“Enyi watu wote, nawaita nyinyi!
Wito wangu ni kwa ajili ya binadamu.
5Enyi wajinga, jifunzeni kuwa na akili;
sikilizeni kwa makini enyi wapumbavu.
6Sikilizeni maana nitakachosema ni jambo muhimu;
midomoni mwangu mtatoka mambo ya adili.
7Kinywa changu kitatamka kweli tupu;
uovu ni chukizo midomoni mwangu.
8Kinywa changu kitatamka maneno ya kweli,
udanganyifu ni haramu midomoni mwangu.
9Kwa mtu mwelewa kila kitu ni wazi,
kwa mwenye maarifa yote ni sawa.
10Chagua mafundisho yangu badala ya fedha;[#8:10 Kuwa na hekima ni bora kupita utajiri wote wa kidunia (taz pia 2:4; 3:14-15; 8:19; Yobu 28:15-19).]
na maarifa badala ya dhahabu safi.
11“Mimi Hekima nina thamani kuliko johari;
chochote unachotamani hakiwezi kulingana nami.
12Mimi Hekima ninao ujuzi;
ninayo maarifa na busara.
13Kumcha Mwenyezi-Mungu ni kuchukia uovu.[#8:13 Taz 1:7 maelezo.]
Nachukia kiburi, majivuno na maisha mabaya;
nachukia na lugha mbaya.
14Nina uwezo wa kushauri na nina hekima.
Ninao ujuzi na nina nguvu.
15Kwa msaada wangu wafalme hutawala,[#8:15-16 Watawala ambao husikiliza hekima hutawala kwa haki na uaminifu. Mfalme au mtawala mwenye hekima ndiye aliyekuwa mtawala bora (Isa 9:6,7; 11:1-5). Wazo hili linakumbusha ombi la mfalme Solomoni apewe hekima (1Fal 3:6-9; 2Nya 1:8-10).]
watawala huamua yaliyo ya haki.
16Kwa msaada wangu viongozi hutawala,
wakuu na watawala halali.
17Nawapenda wale wanaonipenda;
wanaonitafuta kwa bidii hunipata.
18Utajiri na heshima viko kwangu,
mali ya kudumu na fanaka.
19Matunda yangu ni mazuri kuliko dhahabu safi,
faida yangu yashinda ile ya fedha bora.
20Natembea katika njia ya uadilifu;
ninafuata njia za haki.
21Mimi huwatajirisha wanaonipenda,
huzijaza tele hazina zao wanipendao.
22“Mwenyezi-Mungu aliniumba mwanzoni mwa kazi yake,
zama za zama kabla ya kuwako kitu chochote.
23Nilifanywa mwanzoni mwa nyakati,
nilikuwako kabla ya dunia kuanza.
24Nilizaliwa kabla ya vilindi vya bahari,
kabla ya chemchemi zibubujikazo maji.
25Kabla ya milima haijaumbwa,
na vilima kusimamishwa mahali pake,
mimi nilikuwako tayari.
26Kabla Mungu hajaumba dunia na mashamba yake,
wala chembe za kwanza za mavumbi ya dunia.
27Nilikuwako wakati alipoziweka mbingu,
wakati alipopiga duara juu ya bahari;
28wakati alipoimarisha mawingu mbinguni,
alipozifanya imara chemchemi za bahari;
29wakati alipoiwekea bahari mpaka wake,
maji yake yasije yakavunja amri yake;
wakati alipoiweka misingi ya dunia.
30Nilikuwa pamoja naye kama fundi stadi,[#8:30 Au, “kama mtoto mdogo”. Wengine wanafikiri “fundi stadi” ni kisifa cha Mungu na katika tafsiri wana: “Nilikuwa pamoja na yeye aliye fundi stadi”.]
nilikuwa furaha yake kila siku,
nikishangilia mbele yake daima,
31nikifurahia dunia na wakazi wake,
na kupendezwa kuwa pamoja na wanadamu.
32“Sasa basi wanangu, nisikilizeni:
heri wale wanaofuata njia zangu.
33Sikilizeni mafunzo mpate hekima,
wala msiyakatae.
34Heri mtu anayenisikiliza,
anayekaa kila siku mlangoni pangu,
anayekesha karibu na milango yangu.
35Anayenipata mimi amepata uhai,
amepata upendeleo kwa Mwenyezi-Mungu.
36Asiyenipata anajidhuru mwenyewe;
wote wanaonichukia wanapenda kifo.”