Zaburi 113

Zaburi 113

Sifa kwa Mungu mtukufu

1Msifuni Mwenyezi-Mungu!

Enyi watumishi wa Mwenyezi-Mungu, lisifuni jina lake!

2Jina lake litukuzwe,

sasa na hata milele.

3Kutoka mashariki na hata magharibi,[#113:3 Manaeno yanayotumika kusema ulimwenguni kote (50:1; Mal 1:11).]

litukuzwe jina la Mwenyezi-Mungu!

4Mwenyezi-Mungu atawala juu ya mataifa yote,

utukufu wake wafika juu ya mbingu.

5Nani aliye kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu?

Yeye ameketi juu kabisa;

6lakini anatazama chini,

azione mbingu na dunia.

7Humwinua fukara kutoka mavumbini;[#113:7 neno linalotumiwa kimfano na linamaanisha hali duni ya kukandamizwa. Taz msemo wa namna hiyo hiyo katika 1Sam 2:4-8; Luka 1:46-53.]

humnyanyua maskini kutoka unyonge wake,

8na kumweka pamoja na wakuu;

pamoja na wakuu wa watu wake.

9Humjalia mwanamke tasa furaha nyumbani kwake;

humfurahisha kwa kumjalia watoto.

Msifuni Mwenyezi-Mungu!

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania