The chat will start when you send the first message.
1Watu wa Israeli walipotoka Misri,
wazawa wa Yakobo walipotoka ugenini,
2Yuda ikawa maskani ya Mungu,[#114:2 Au, “Yuda ikawa patakatifu pake”. Mungu alimteua Mose kuwatoa watu wake Misri, akawaongoza wakaingia katika nchi ya Kanaani. Baadaye, Mungu alichagua Yerusalemu, mji wa Yuda, kuwa makao yake; hivyo, kwa maneno mengine kabila la Yuda lilikuwa maskani yake Mungu.]
Israeli ikawa milki yake.
3Bahari iliona hayo ikakimbia;
mto Yordani ukaacha kutiririka!
4Milima ilirukaruka kama kondoo dume;
vilima vikaruka kama wanakondoo!
5Ee bahari, imekuwaje hata ukakimbia?
Nawe Yordani, kwa nini ukaacha kutiririka?
6Enyi milima, mbona mliruka kama kondoo dume?
Nanyi vilima, mmerukaje kama wanakondoo?
7Tetemeka, ee dunia mbele yake Mwenyezi-Mungu;
tetemeka mbele ya Mungu wa Yakobo,
8anayeugusa mwamba ukawa bwawa la maji,
nayo majabali yakawa chemchemi za maji!