Zaburi 19

Zaburi 19

Utukufu wa Mungu katika viumbe

1Mbingu zatangaza utukufu wa Mungu;[#19 Kwa Zaburi hii mtunzi wake anamsifu Mwenyezi-Mungu kwa sababu ya matendo yake mawili: maumbile (aya 1-6), na sheria yake (aya 7-11).]

anga ladhihirisha kazi ya mikono yake.

2Mchana waupasha habari mchana ufuatao,

usiku waufahamisha usiku ufuatao.

3Hamna msemo au maneno yanayotumika;

wala hakuna sauti inayosikika;

4hata hivyo, sauti yao yaenea duniani kote,

na maneno yao yafika kingo za ulimwengu.

Mungu ameliwekea jua makao yake angani;

5nalo hutoka kama bwana arusi chumbani mwake,

lafurahi kama shujaa aliye tayari kushindana.

6Lachomoza toka upande mmoja,

na kuzunguka hadi upande mwingine;

hakuna kiwezacho kuliepa joto lake.

Sheria ya Mungu

7Sheria ya Mwenyezi-Mungu ni kamilifu,

humpa mtu uhai mpya;

masharti ya Mwenyezi-Mungu ni thabiti,

huwapa hekima wasio na makuu.

8Kanuni za Mwenyezi-Mungu ni sawa,

huufurahisha moyo;

amri ya Mwenyezi-Mungu ni safi,

humwelimisha mtu.

9Kumcha Mwenyezi-Mungu ni jambo jema,

na la kudumu milele;

maagizo ya Mwenyezi-Mungu ni sawa,

yote ni ya haki kabisa.

10Yatamanika kuliko dhahabu;

kuliko dhahabu safi kabisa.

Ni matamu kuliko asali;

kuliko asali safi kabisa.

11Yanifunza mimi mtumishi wako;

kuyafuata kwaniletea tuzo kubwa.

12Lakini nani aonaye makosa yake mwenyewe?

Ee Mungu, niepushe na makosa nisiyoyajua.

13Unikinge mimi mtumishi wako na makosa ya makusudi,

usikubali hayo yanitawale.

Hapo nitakuwa mkamilifu,

wala sitakuwa na hatia ya kosa kubwa.

14Maneno ya kinywa changu, na mawazo ya moyo wangu,

yakubalike mbele yako, ee Mwenyezi-Mungu,

mwamba wangu na mkombozi wangu!

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania