Zaburi 3

Zaburi 3

Kuomba msaada asubuhi

1Ee Mwenyezi-Mungu, tazama walivyo wengi adui zangu,

ni wengi mno hao wanaonishambulia.

2Wengi wanasema juu yangu,

“Hatapata msaada kwa Mungu.”

3Lakini wewe ee Mwenyezi-Mungu u ngao yangu kila upande;[#3:3 Silaha ya kujikinga iliyotengenezwa kwa chuma au ngozi iliyopakwa mafuta. Neno hili linatumika hapa kama mfano wa ulinzi wa Mungu (ling Mwa 15:1).]

kwako napata fahari na ushindi wangu.

4Nakulilia kwa sauti, ee Mungu,

nawe wanisikiliza kutoka mlima wako mtakatifu.

5Nalala na kupata usingizi,

naamka tena maana wewe ee Mwenyezi-Mungu wanitegemeza.

6Sitayaogopa maelfu ya watu,

wanaonizingira kila upande.

7Uje ee Mwenyezi-Mungu!

Niokoe ee Mungu wangu!

Wewe wawavunja mataya maadui zangu wote;

wawavunja meno waovu wasinidhuru.

8Mwenyezi-Mungu ndiwe uokoaye;

uwape baraka watu wako.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania