Zaburi 34

Zaburi 34

Sifa kwa wema wa Mungu

1Nitamtukuza Mwenyezi-Mungu nyakati zote,

sitaacha kamwe kuzitamka sifa zake.

2Mimi nitaona fahari juu ya Mwenyezi-Mungu,

wanyonge wasikie na kufurahi.

3Mtukuzeni Mwenyezi-Mungu pamoja nami,

sote pamoja tulisifu jina lake.

4Nilimwomba Mwenyezi-Mungu naye akanijibu,

na kuniondoa katika hofu zangu zote.

5Mgeukieni Mungu mpate kufurahi;

nanyi hamtaaibishwa kamwe.

6Maskini alimlilia Mwenyezi-Mungu, naye akamsikia,[#34:6 Watunzi wa Zaburi hujitaja mara kwa mara kama “wapole” au “maskini” kutokana na hali ya kutaka kunyenyekea mbele ya Mungu. Taz 37:11.]

na kumwokoa katika taabu zake zote.

7Malaika wa Mwenyezi-Mungu huwalinda wote wamchao,

na kuwaokoa katika hatari.

8Jaribuni mwone Mwenyezi-Mungu alivyo mwema.

Heri mtu anayekimbilia usalama kwake.

9Mcheni Mwenyezi-Mungu enyi watakatifu wake;

maana wenye kumcha hawatindikiwi na kitu.

10Hata wanasimba hutindikiwa na kuona njaa;[#34:10 Katika kitabu cha Zaburi mara nyingine wanyamapori wakali hutumiwa kama mfano wa maadui za watu wa Mungu. Taz pia 10:9-10; 22:12-13.]

lakini wanaomtafuta Mwenyezi-Mungu hawakosi chochote chema.

11Njoni enyi vijana mkanisikilize,

nami nitawafundisha kumcha Mwenyezi-Mungu.

12Je, watamani kufurahia maisha,

kuishi maisha marefu na kufurahia mema?

13Basi, acha kusema mabaya,

na kuepa kusema uongo.

14Jiepushe na uovu, utende mema;

utafute amani na kuizingatia.

15Mwenyezi-Mungu huwaangalia waadilifu,

na kusikiliza malalamiko yao;

16lakini huwapinga watu watendao maovu,

awafutilie mbali kutoka duniani.

17Waadilifu wakimlilia Mwenyezi-Mungu yeye huwasikia,

na kuwaokoa katika taabu zao zote.

18Mwenyezi-Mungu yu karibu na waliokufa moyo;

huwaokoa wote waliokata tamaa kabisa.

19Mateso ya mwadilifu ni mengi,

lakini Mwenyezi-Mungu humwokoa kutoka yote.

20Huvilinda viungo vya mwili wake wote,

hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.

21Ubaya huwaletea waovu kifo;

wanaowachukia waadilifu wataadhibiwa.

22Mwenyezi-Mungu huokoa maisha ya watumishi wake,

wote wanaomkimbilia hawataadhibiwa.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania