The chat will start when you send the first message.
1Ee Mungu mtetezi wa haki yangu, unijibu niombapo.
Nilipokuwa katika shida, wewe ulinisaidia;
unionee huruma na kusikia sala yangu.
2Jamani, mtaniharibia jina langu mpaka lini?
Mpaka lini mtapenda upuuzi na kusema uongo?
3Jueni kuwa Mwenyezi-Mungu amejiteulia mwaminifu wake.
Mwenyezi-Mungu husikia kila ninapomwomba.
4Tetemekeni kwa hofu na msitende dhambi;
tafakarini vitandani mwenu na kunyamaza.
5Toeni tambiko zilizo sawa,[#4:5 Yaani matoleo au tambiko zisizochanganyika na dhambi (Isa 1:10-17) au zenye kutokana na upendo na kumjua Mungu kikweli (Hos 6:6; Amo 5:21-25).]
na kumtumainia Mwenyezi-Mungu.
6Wengi husema: “Laiti tungepata tena fanaka!
Utuangalie kwa wema, ee Mwenyezi-Mungu!”
7Lakini mimi umenijalia furaha kubwa moyoni,
kuliko ya hao walio na divai na ngano kwa wingi.
8Nalala na kupata usingizi kwa amani;
ee Mwenyezi-Mungu, wewe peke yako waniweka salama.