The chat will start when you send the first message.
1Anayekaa chini ya ulinzi wa Mungu Mkuu,[#91:1-13 Aya hizi zote zina wazo moja muhimu: ulinzi na kinga ya Mungu kwa watu wake.]
anayeishi chini ya kivuli cha Mungu Mwenye Nguvu,
2ataweza kumwambia Mwenyezi-Mungu:
“Wewe ni kimbilio langu na ngome yangu;
Mungu wangu, ninayekutumainia!”
3Hakika Mungu atakuokoa katika mtego;
atakukinga na maradhi mabaya.
4Atakufunika kwa mabawa yake,[#91:4 Hapa Mwanazaburi anaeleza juu ya Mungu kwa picha au mfano wa mama ndege anavyowalinda vifaranga vyake; au kwa mfano wa wale viumbe wenye mabawa ambao walikuwa juu ya sanduku la agano na walifikiriwa kuwa ni kiti cha enzi cha Mungu.]
utapata usalama kwake;
mkono wake utakulinda na kukukinga.
5Huna haja ya kuogopa vitisho vya usiku,
wala shambulio la ghafla mchana;
6huna haja ya kuogopa baa lizukalo usiku,
wala maafa yanayotokea mchana.
7Hata watu elfu wakianguka karibu nawe,[#91:7 Hii inaweza kuwa kwa sababu ya ugonjwa au kwa vita.]
naam, elfu kumi kuliani mwako,
lakini wewe baa halitakukaribia.
8Kwa macho yako mwenyewe utaangalia,
na kuona jinsi watu waovu wanavyoadhibiwa.
9Wewe umemfanya Mwenyezi-Mungu kuwa kimbilio lako;
naam, Mungu aliye juu kuwa kinga yako.
10Kwa hiyo, hutapatwa na maafa yoyote;[#91:10 Ahadi ya Mungu siyo kwamba hakutatokea baa lolote, lile kwamba ulinzi na kinga ya Mungu utakuwako daima kama inavyodhihirika katika aya inayofuata.]
nyumba yako haitakaribiwa na baa lolote.
11Maana Mungu atawaamuru malaika zake,[#91:11 Katika Biblia malaika hutumika kama wajumbe na watumishi wa Mungu. Taz pia Malaika katika Fahirisi.]
wakulinde popote uendapo.
12Watakuchukua mikononi mwao,
usije ukajikwaa kwenye jiwe.
13Utakanyaga simba na nyoka,[#91:13 Mara nyingi wanyama hutumiwa kama mfano wa maadui. Taz Luka 10:19 na Zab 34:10.]
utawaponda wana simba na majoka.
14Mungu asema: “Nitamwokoa yule anipendaye;
nitamlinda anayenitambua!
15Akiniita, mimi nitamwitikia;
akiwa taabuni nitakuwa naye;
nitamwokoa na kumpa heshima.
16Nitamridhisha kwa maisha marefu,
nitamjalia wokovu wangu.”