The chat will start when you send the first message.
1Mwimbieni Mwenyezi-Mungu wimbo mpya![#96:1 Wimbo mpya unaimbwa kusherehekea matukio mapya, hapa huenda ni lile tukio la kuwarudisha Waisraeli kutoka uhamishoni Babuloni ambako walipelekwa mnamo mwaka 586 K.K.]
Mwimbieni Mwenyezi-Mungu, ulimwengu wote!
2Mwimbieni Mwenyezi-Mungu na kulisifu jina lake.
Tangazeni kila siku matendo yake ya wokovu.
3Yatangazieni mataifa utukufu wake,
waambieni watu wote matendo yake ya ajabu.
4Maana Mwenyezi-Mungu ni mkuu, anasifika sana;
anastahili kuheshimiwa kuliko miungu yote.
5Miungu ya mataifa mengine si kitu;[#96:5 Taz 31:6. Kuabudu miungu mingine kulikatazwa na sheria ya Mungu (Kut 20:4-6; Kumb 5:8-10).]
lakini Mwenyezi-Mungu aliziumba mbingu.
6Utukufu na fahari vyamzunguka;
nguvu na uzuri vyalijaza hekalu lake.
7Mpeni Mwenyezi-Mungu heshima, enyi jamii zote za watu;
naam, kirini utukufu na nguvu yake.
8Lisifuni jina lake tukufu;
leteni tambiko na kuingia hekaluni mwake.
9Mwabuduni Mwenyezi-Mungu katika patakatifu pake;[#96:9 Au, “kwa mavazi ya ibada”. Au, “anapotokea”. Aya 9 ni sawa na Zab 29:2b ambapo zingatia maelezo ya 29:1-2.]
tetemekeni mbele yake ee dunia yote!
10Yaambieni mataifa: “Mwenyezi-Mungu anatawala!
Ameuweka ulimwengu imara, hautatikisika.
Atawahukumu watu kwa haki!”
11Furahini enyi mbingu na dunia!
Bahari na ivume pamoja na vyote vilivyomo!
12Furahini enyi mashamba na vyote vilivyomo!
Ndipo miti yote misituni itaimba kwa furaha,
13mbele ya Mwenyezi-Mungu anayekuja;
naam, anayekuja kuihukumu dunia.
Ataihukumu dunia kwa haki,
na mataifa kwa uaminifu wake.