Ufunuo 2

Ufunuo 2

Ujumbe kwa Efeso

1“Kwa malaika wa kanisa la Efeso andika: “Mimi nishikaye zile nyota saba katika mkono wangu wa kulia na ambaye hutembea katikati ya vinara saba vya taa vya dhahabu, nasema hivi:[#2:1 Mji maarufu kupita yote katika Asia Ndogo nyakati hizo. Tazama pia utangulizi, barua kwa Waefeso (Mate 18:19—19:41; 20:17-38 na pia 1Tim 1:3-4).]

2Najua mambo yako yote; najua bidii yako na uvumilivu wako. Najua kwamba huwezi kuwavumilia watu waovu, na kwamba umewapima wale wanaojisemea kuwa mitume na kumbe sio, ukagundua kwamba ni waongo.

3Wewe unayo saburi, umestahimili taabu nyingi kwa ajili ya jina langu, wala hukuvunjika moyo.

4Lakini ninalo jambo moja dhidi yako: wewe hunipendi tena sasa kama pale awali.

5Basi, pakumbuke pale ulipokuwa kabla ya kuanguka, ukatubu na kufanya kama ulivyofanya pale awali. La sivyo, naja kwako na kukiondoa kinara chako cha taa mahali pake.[#2:5 Lugha ya picha yenye maana ya kukomesha uhai wa kanisa kusema kuondolea mbali umaarufu wake hapa duniani na hata mbinguni.]

6Lakini nakusifu juu ya kitu kimoja: wewe unayachukia wanayoyatenda Wanikolai kama ninavyoyachukia mimi.[#2:6 Kundi la watu ambao hatuna habari zao zaidi. Taz 2:15 maelezo.]

7“Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho anayoyaambia makanisa!

“Mshindi nitamjalia kula matunda ya mti wa uhai ulioko ndani ya bustani ya Mungu.

Ujumbe kwa Smurna

8“Kwa malaika wa kanisa la Smurna andika:[#2:8 Mji wa pwani kaskazini mwa Efeso, siku hizi unaitwa Izmir.]

“Mimi niliye wa kwanza na wa mwisho, ambaye nilikufa na kuishi tena, nasema hivi:

9Najua taabu zako; najua pia umaskini wako, ingawaje kwa kweli wewe ni tajiri; najua kashfa walizokufanyia wale wanaojiita Wayahudi lakini si Wayahudi wa kweli, bali ni kundi lake Shetani.[#2:9 Ni vigumu kujua kwa hakika watu hao ni kina nani. Lakini tazama pia Rom 2:28-29.]

10Usiogope hata kidogo yale ambayo itakulazimu kuteseka. Sikiliza! Ibilisi anataka kuwajaribu kwa kuwatia baadhi yenu gerezani; nanyi mtapata dhiki kwa muda wa siku kumi. Muwe waaminifu hata mpaka kufa, nami nitawapeni taji ya uhai.[#2:10 Picha au mfano wa kusema kwa “muda mfupi” (taz Dan 1:12,14).; #2:10 Yaani, uhai kama zawadi au nishani ya ushindi. (Hapo kale, katika michezo ya mashindano, wanariadha walioshinda walivikwa taji).]

11“Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho anayoyaambia makanisa!

“Mshindi hataumizwa na kifo cha pili.

Ujumbe kwa Pergamumu

12“Kwa malaika wa kanisa la Pergamumu andika:[#2:12 Mji huu ulikuwa maarufu, ni kitovu cha ibada mbalimbali kwa miungu na aghalabu ibada kwa Mtawala Mkuu wa Roma ambaye kwa heshima yake hekalu lake lilijengwa humo yapata mwaka wa 29 K.K.]

“Mimi niliye na upanga mkali wenye makali kuwili nasema hivi:

13Najua unakoishi: Wewe unaishi kwenye makao makuu ya Shetani! Lakini bado unashikilia jina langu; hukuikana imani yako kwangu hata siku zile Antipa, shahidi wangu mwaminifu, alipouawa pale mahali anapoishi Shetani.[#2:13 Au: Pale Shetani alipo na kiti chake cha enzi. Msemo kidogo wa kutatanisha, lakini huenda mwandishi aliona Pergamumu kuwa mahali ambapo utawala wa Shetani ulipamba hasa kwa wingi wa ibada za miungu wa uwongo. Baadhi wanafikiri mwandishi anagusia ibada iliyofanywa kwa Mtawala Mkuu wa Roma au ibada kwa mungu Zeu.; #2:13 Hatuna habari nyingine juu ya huyu Antipa.]

14Lakini ninayo machache dhidi yako: baadhi yenu ni wafuasi wa Balaamu aliyemfundisha Balaki kuwatega wana wa Israeli wale vyakula vilivyotambikiwa sanamu na kufanya uzinzi.[#2:14 Tazama Hes 22:24-25.; #2:14 1Kor 8:7-13; 10:20-21.; #2:14 Kumwacha Mungu wa kweli na kufuata miungu ya uwongo kunasemwa katika Biblia mara nyingi kama kukosa uaminifu na hivyo “uzinzi” (Kut 34:15; Isa 1:21; Eze 16:23; Hos 1:2; Ufu 17).]

15Vivyo hivyo, wako pia miongoni mwenu watu wanaofuata mafundisho ya Wanikolai.[#2:15 Tazama maelezo ya 2:6. Labda haohao ndio walioshikilia mafundisho ya Balaamu anayetajwa katika aya ya 14. Aghalabu jina Nikolao kwa Kigiriki laweza kuchukuliwa kama tafsiri ya Balaamu yaani “Mla watu” au “Mmeza watu”.]

16Basi, tubu. La sivyo, nitakuja kwako upesi na kupigana na watu hao kwa upanga utokao kinywani mwangu.

17“Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho anayoyaambia makanisa!

“Mshindi nitampa ile mana iliyofichika. Nitampa pia jiwe jeupe lililoandikwa jina jipya ambalo hakuna mtu aliyelijua isipokuwa tu wale wanaolipokea.

Ujumbe kwa Thuatira

18“Kwa malaika wa kanisa la Thuatira andika hivi:[#2:18 Mji kusini-mashariki mwa Pergamumu ambao ulisifika kwa biashara yake (Mate 16:14).]

“Huu ndio ujumbe wa Mwana wa Mungu, ambaye macho yake yametameta kama moto, na miguu yake inang'aa kama shaba iliyosuguliwa.

19Najua mambo yako yote. Najua upendo wako, imani yako, utumishi wako na uvumilivu wako. Wewe unafanya vizuri zaidi sasa kuliko pale awali.

20Lakini nina jambo moja dhidi yako: wewe unamvumilia yule mwanamke Yezebeli anayejiita nabii, anayefundisha na kuwapotosha watumishi wangu wafanye uzinzi na kula vyakula vilivyotambikiwa sanamu.[#2:20 Jina la mkewe mfalme Ahabu ambaye alihimiza na kupamba ibada ya mungu wa uongo huko nchini Israeli (1Fal 16:31-33). Hapa yamkini jina hilo latumiwa kama mfano.]

21Nimempa muda wa kutubu, lakini hataki kuachana na uzinzi wake.[#2:21 Uzinzi wa Yezebeli ulihusika na kuchanganya ibada ya mungu Baali na ile ya Mwenyezi-Mungu.]

22Sikiliza! Sasa namtupa kitandani ambapo yeye pamoja na wote waliofanya uzinzi naye watapatwa na mateso makali, kama wasipotubu matendo yao mabaya waliyotenda naye.[#2:22 Yaani wote waliofuata mafundisho yake.]

23Tena nitawaua wafuasi wake, ili makanisa yote yatambue kwamba mimi ndiye ninayechunguza mioyo na fikira za watu.[#2:23 Au: Watoto wake. Hao ni wale wanaofuata mafundisho yake.; #2:23 Zab 7:9; Yer 17:10. Yesu hupatiliza sio tu uzinzi bali pia mawazo mabaya (Mat 5:27-30).]

24“Lakini nyinyi wengine mlioko huko Thuatira ambao hamfuati mafundisho yake Yezebeli na ambao hamkujifunza kile wanachokiita Siri ya Shetani, nawaambieni kwamba sitawapeni mzigo mwingine.[#2:24 Mafundisho ya siri ya Shetani. Angalia pia 1Kor 2:10.]

25Lazima mzingatie yale mliyo nayo sasa mpaka nitakapokuja.

26“Mshindi na mwenye kuzingatia mpaka mwisho mambo ninayotaka, nitampa mamlaka juu ya watu wa mataifa:

27atawaongoza kwa fimbo ya chuma na kuwavunjavunja kama vyombo vya udongo.[#2:27 Tazama Zab 2:8-9; maneno ambayo yanatumiwa kwa Yesu Kristo (taz Ufu 12:5).]

28Mimi pia nimepokea mamlaka hayo kutoka kwa Baba yangu. Tena nitampa nyota ya asubuhi.[#2:28 Maneno hayo yanatumiwa katika 22:16 kuhusu Kristo. Mshindi, atashiriki sifa zake Yesu Kristo. Nyota hiyo huashiria mwisho wa usiku na mwanzo wa mchana. Ni ishara ya ushindi na mamlaka.]

29“Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa!

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania