Ufunuo 8

Ufunuo 8

Mhuri wa saba

1Na Mwanakondoo alipouvunja mhuri wa saba, kukawa kimya mbinguni kwa muda wa nusu saa.[#8:1 Uvunjaji wa mhuri wa saba unamalizia sehemu hii iliyoanza katika 4:1; kisa hiki pia kinatayarisha matukio yafuatayo.]

2Kisha, nikawaona wale malaika saba wanaosimama mbele ya Mungu wamepewa tarumbeta saba.[#8:2-6 Ni sehemu inayotayarisha tukio jipya ambalo lahusu malaika saba na tarumbeta zao. Kwa mfano huo wa tarumbeta saba (8:2—11:8) inaoneshwa jinsi Mungu anavyowakomboa watu wake na kuwaadhibu waasi. Kwamba balaa na maangamizi yanaathiri tu sehemu fulani ya dunia, yaonesha kwamba huo si mwisho bado. Baadhi ya mabaa yanayotajwa hapa yanafanana na mengine ya kule Misri katika kitabu cha Kutoka.]

3Malaika mwingine akafika, anachukua chetezo cha dhahabu, akasimama mbele ya madhabahu ya kufukizia ubani. Naye akapewa ubani mwingi autoe sadaka pamoja na sala za watu wote wa Mungu juu ya madhabahu ya dhahabu iliyo mbele ya kiti cha enzi.[#8:3 Tazama maelezo ya 5:8.; #8:3 Ni ileile ya kuchomea ubani; ling Kut 30:1-5.]

4Moshi wa ubani ukapanda juu, pamoja na sala za watu wa Mungu kutoka mikononi mwake huyo malaika aliyekuwa mbele ya Mungu.

5Kisha, malaika akakichukua hicho chetezo, akakijaza moto wa madhabahuni, akakitupa duniani. Kukawa na ngurumo, sauti, umeme na tetemeko la ardhi.

Tarumbeta

6Kisha, wale malaika saba wenye tarumbeta saba wakajiweka tayari kupiga mbiu ya mgambo.

7Malaika wa kwanza akapiga tarumbeta yake. Mchanganyiko wa mvua ya mawe na moto pamoja na damu ukamwagwa juu ya nchi. Theluthi moja ya nchi ikaungua, theluthi moja ya miti ikaungua na majani yote mabichi yakaungua.

8Kisha malaika wa pili akapiga tarumbeta yake. Na kitu kama mlima mkubwa unaowaka moto kikatupwa baharini. Theluthi moja ya bahari ikawa damu,

9theluthi moja ya viumbe vya baharini vikafa, na theluthi moja ya meli zikaharibiwa.

10Kisha, malaika wa tatu akapiga tarumbeta yake. Na nyota kubwa ikiwaka kama bonge la moto ikaanguka kutoka mbinguni na kutua juu ya theluthi moja ya mito na chemchemi za maji.[#8:10-11 Yer 9:15; 23:15. “Uchungu”: Neno hili linatafsiri jina la mmea fulani ambao unasifika kwa mwonjo wake mchungu sana (taz Meth 5:4 na Ombo 3:15); nalo latumika hapa kama mfano wa jadi wa kueleza maumivu, dhuluma na uchungu.]

11(Nyota hiyo inaitwa “Uchungu.”) Basi, theluthi moja ya maji yakawa machungu; watu wengi wakafa kutokana na maji hayo, kwa sababu yaligeuka kuwa machungu.

12Kisha, malaika wa nne akapiga tarumbeta yake. Ndipo theluthi moja ya jua, ya mwezi na ya nyota ikapata pigo; hata mwangaza ukapoteza theluthi moja ya mng'ao wake. Theluthi moja ya mchana ikakosa mwanga, hali kadhalika na theluthi moja ya usiku.[#8:12 Pigo la giza ni kama lile la Kut 10:21-23; taz pia Isa 13:10; Eze 32:7; Yoe 2:10,31; 3:15.]

13Kisha, nikatazama, nikasikia tai akiruka juu kabisa angani, anasema kwa sauti kubwa, “Ole, ole, ole kwa wanaoishi duniani wakati malaika watatu waliobaki watakapopiga tarumbeta zao!”[#8:13 Hapa anatumiwa kama ndege aletaye kifo na uharibifu.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania