Tito 3

Tito 3

Maisha ya Kikristo

1Wakumbushe watu kuwastahi watawala na wenye mamlaka, kuwatii na kuwa tayari kwa kila namna kutenda mambo yote mema.[#3:1 Kuhusu uhusiano baina ya waumini au Wakristo na maisha ya raia, taz 1Tim 2:1-4 maelezo, na rejea Rom 13:1-7; 1Pet 2:13-17.; #3:1 Tito 3:8,14; rejea Efe 4:28.]

2Waambie wasimtukane mtu yeyote; bali waishi kwa amani na masikilizano, wawe daima wapole kwa kila mtu.

3Maana, wakati mmoja sisi tulikuwa wapumbavu, wakaidi na wapotovu. Tulikuwa watumwa wa tamaa na anasa za kila aina. Tuliishi maisha ya uovu na wivu; watu walituchukia nasi tukachukiana.[#3:3-7 Sehemu hii kama ile ya Tito 2:11-14 inatumia maeneno ambayo yalikuwa ya kawaida katika mapokeo.]

4Lakini wakati wema na upendo wa Mungu, Mwokozi wetu ulipofunuliwa,[#3:4 Taz Tito 1:3 maelezo.]

5alituokoa si kwa sababu ya jambo lolote jema tulilotenda sisi, bali kwa sababu ya huruma yake, kwa njia ya Roho Mtakatifu anayetujalia tuzaliwe upya na kuwa na maisha mapya kwa kutuosha kwa maji.[#3:5 Rejea 2Tim 1:9 na pia Kumb 9:18; Rom 3:27-28; 4:25; Gal 2:16; Efe 2:8-9.; #3:5 Rejea Rom 6:3-4; 2Kor 5:17.]

6Mungu alitumiminia Roho Mtakatifu bila kipimo kwa njia ya Yesu Kristo, Mwokozi wetu,[#3:6 Au, “Alitumiminia … kwa wingi”. Taz Yoeli 2:28; tazama pia Mate 2:17.]

7ili kwa neema yake tupate kukubaliwa kuwa waadilifu na kuupokea uhai wa milele tunaotumainia.[#3:7 Rejea Rom 3:24. “Tupate kukubaliwa kuwa waadilifu”: Taz Rom 1:17 maelezo.]

8Jambo hili ni kweli.[#3:8 Au, “Neno hili ni kweli”. Yahusu yote yaliyosemwa katika aya zilizotangulia (aya ya 3-7) ambazo zina baadhi ya mawazo ya msingi ya imani ya Wakristo.]

Ninakutaka uyatilie mkazo mambo haya, ili wale wanaomwamini Mungu wawe na hamu ya kuutumia wakati wao katika kutenda mema, yaani mambo mazuri na ya kuwafaa watu.

9Lakini jiepushe na ubishi wa kipumbavu, ugomvi na mabishano juu ya sheria. Mambo hayo hayana faida yoyote na ni ya bure tu.[#3:9 Taz 1Tim 1:4, na rejea 1Tim 4:7; 6:20; Tito 1:14. “Sheria”: Yaani, vitabu vitano vya kwanza vya A.K.]

10Mtu anayesababisha mafarakano mpe onyo la kwanza na la pili, kisha achana naye.[#3:10 Rejea Mat 18:15-17; 2Thes 3:14. “Mtu anayesababisha mafarakano”: Rom 16:17; 1Kor 1:10; Yuda 19.]

11Wajua kwamba mtu wa namna hiyo amepotoka kabisa, na dhambi zake zathibitisha kwamba amekosea.

Mawaidha ya mwisho

12Baada ya kumtuma kwako Artema au Tukiko, fanya bidii kuja Nikopoli unione, maana nimeamua kukaa huko wakati wa majira ya baridi.[#3:12 Anatajwa hapa tu.; #3:12 Mate 20:4; Efe 6:21-22; Kol 4:7-8; 2Tim 4:12.; #3:12 Labda mji wa pwani ya magharibi ya Ugiriki kaskazini-mashariki mwa Korintho.]

13Jitahidi kumsaidia mwanasheria Zena na Apolo ili waweze kuanza ziara zao, na uhakikishe kwamba wana kila kitu wanachohitaji.[#3:13 Anatajwa hapa tu.; #3:13 Mate 18:24; 1Kor 3:5-6; 16:12.]

14Ni lazima watu wetu wajifunze kuutumia wakati wao katika kutenda mema ili wasaidie katika mahitaji ya kweli, na maisha yao yawe ya kufaa.[#3:14 Mate 20:35; Efe 4:28.]

15Watu wote walio pamoja nami wanakusalimu. Wasalimu rafiki zetu katika imani.[#3:15 Tafsiri nyingine yamkini: “Wasalimu rafiki zetu waaminifu”.]

Nawatakieni nyote neema ya Mungu.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania