Hekima ya Solomoni 14

Hekima ya Solomoni 14

1Tena mtu anajiandaa kusafiri kwa jahazi penye mawimbi baharini,

naye anakiomba msaada kipande cha mti kibovu kuliko jahazi atakalosafiria!

2Mtu fulani aliunda jahazi hilo ili kujipatia faida,

fundi akalitengeneza kwa ustadi wake.

3Lakini, ee Baba, uangalizi wako ndio unaoliongoza.

Kwa maana hata baharini wewe umetupa njia,

na katika mawimbi kuna mapito salama,

4ukionesha kuwa waweza kuokoa katika kila hatari,

hata mtu asiye na ufundi huo aweza kusafiri baharini.

5Ulitaka vitu ulivyoviumba kwa hekima yako viwe vya kufaa watu;

kwa hiyo watu huona wako salama hata katika kipande cha mti,

wakavuka mawimbi ya maji juu ya mti na kufika salama bandarini.

6Ndivyo pia ilivyokuwa hapo kale wakati majitu makorofi yalipokuwa yakiangamia,

yule mtu aliyekuwa tumaini la ulimwengu alikimbilia chomboni

na chini ya uongozi wako akauachia ulimwengu mbegu ya kizazi kipya.

7Kimebarikiwa chombo hicho cha mti kilichosababisha wokovu kutujia.

8Lakini kinyago kilichochongwa na mikono ya binadamu kimelaaniwa;

hali kadhalika naye yule aliyekitengeneza amelaaniwa,

huyo analaaniwa kwa sababu alikitengeneza,

na hicho chenye kuharibika kwa sababu kimeitwa mungu.

9Mungu anawachukia watu waovu pamoja na matendo yao maovu.

10Naam, Mungu atakiadhibu hicho kitu na huyo aliyekifanya.

11Basi, sanamu za kuabudiwa wanazofanya wasiomjua Mungu zitahukumiwa,

maana ingawa zimetengenezwa kwa vitu alivyoumba Mungu mwenyewe,

zimekuwa chukizo kubwa,

zimekuwa kitanzi kwa roho za watu,

zimekuwa mtego kwa miguu ya wapumbavu.

Chanzo cha kuabudu sanamu

12Wazo la kufanya sanamu za miungu ndicho chanzo cha uasherati;

naam, uvumbuzi wake ndio uharibifu wa maisha.

13Sanamu hazikuwako tangu awali,

na wala hazitaendelea huwako milele.

14Zililetwa ulimwenguni kwa kiburi cha binadamu,

ndiyo maana mwisho wake wa haraka umepangwa.

15Baba mmoja aliona uchungu sana kwa kifo asichotazamia,

basi, akatengeneza sanamu ya mwanawe aliyekufa ghafla;

akamheshimu kama mungu huyo aliyekufa kama kawaida ya binadamu;

kisha akawakabidhi watu waliokuwa chini yake taratibu za siri na kanuni za ibada.

16Baadaye, desturi hiyo mbovu ikazidi kuwa imara hata ikawa sheria,

na sanamu za kuchonga zikaabudiwa kwa amri ya wakuu!

17Ikawa watu walipoishi mbali isipowezekana kumheshimu mfalme wao ana kwa ana,

waliwaza sura yake ilivyo huko mbali

wakatengeneza sanamu ya mfalme waliyemheshimu,

ili kwa hamu kubwa ya kumheshimu huyo asiyekuwapo

wamheshimu kana kwamba alikuwapo.

18Kisha, kwa kushawishiwa na juhudi za wasanii,

ibada hiyo ya sanamu ilienea hata kwa watu ambao hawakumjua huyo mfalme.

19Msanii, labda kwa kutaka kujipendekeza kwa mtawala wake,

alitumia ufundi wake na kuchonga sanamu nzuri zaidi ya huyo mtawala.

20Hapo watu wengi huvutiwa na uzuri wa kazi hiyo,

wakamwona kuwa kitu cha kuabudiwa yule ambaye muda mfupi kabla walimheshimu kama mtu tu.

21Hivyo jambo hilo likawa mtego wa kuwanasa watu,

maana watu wakiwa katika taabu au chini ya utawala wa mabavu,

huchukua vitu vilivyotengenezwa kwa mawe au miti na kuvipa heshima anayostahili Mungu peke yake!

Matokeo ya kuabudu sanamu

22Lakini mambo yakawa mabaya zaidi.

Haikutosha kupotoka katika jambo la kumjua Mungu.

Watu waliishi katika maafa makubwa na vita kwa ujinga

hata wakaiita hali hiyo yao amani.

23Waliwachinja watoto wao katika ibada zao na kuadhimisha ibada za siri,

na kufanya mandari za wazimu na mambo yaliyo kinyume cha maumbile.

24Waliacha kuheshimu uhai au kujali usafi wa ndoa.

Mtu humuua mwenzake kwa hila au kumhuzunisha kwa kuzini na mkewe.

25Kila kitu ni fujo na mauaji ya ukatili,

wizi, udanganyifu, ufisadi,

ukosefu wa uaminifu, ghasia, uongo,

26kukandamiza wasio na hatia, utovu wa shukrani,

ukosefu wa uadilifu, uvurugaji wa nidhamu katika mambo ya ndoa,

uzinzi na uasherati.

27Kuabudu sanamu ambazo hata majina yake ni haramu kuyataja,

ndicho chanzo, sababu na matokeo ya kila uovu.

28Watu wanaoziabudu hurukwa na akili kwa furaha,

au kutabiri uongo au kuishi maisha mabaya

au kuapa uongo bila kufikiri.

29Watu hutegemea hizo sanamu zisizo na uhai ndani yake

na kuapa viapo vibaya wakifikiri kwamba hawataadhibiwa.

30Lakini adhabu itawawahi watu hao kwa sababu hizi mbili:

wamemwazia Mungu maovu kwa kuabudu sanamu;

hawakujali kamwe jambo la utakatifu, hata wakatamka kwa kiapo mambo ya uongo kuwadanganya watu.

31Watu waovu wanapokosa watakabiliwa na adhabu

sio kutokana na nguvu za vitu wanavyoapa navyo,

ila kwa adhabu wanayostahili watu waovu.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania