Sefania 2

Sefania 2

Mwito wa toba

1Kusanyikeni, kusanyikeni enyi taifa la watu wasio na aibu,

2kabla hamjapeperushwa mbali kama makapi,[#2:2 Makala ya Kiebrania si dhahiri. Lakini taz Yobu 21:18; Zab 1:4; Yer 13:24; Hos 13:3.]

kabla haijawajia siku ya hasira kali ya Mwenyezi-Mungu,

kabla haijawajia siku ya ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu.

3Mtafuteni Mwenyezi-Mungu enyi wanyenyekevu wote nchini,[#2:3 Hao ni wale walio maskini, wanaoonewa au kukandamizwa na ambao wameweka tumaini lao na tegemeo lao kwa Mwenyezi-Mungu kwani wanayo matumaini kwamba Mwenyezi-Mungu atawaletea msaada. Taz pia “Maskini” katika Orodha ya Maneno. Na kuhusu maneno “mtafuteni Mwenyezi-Mungu” ni lazima yaeleweke ki-Biblia: hutumika mara kwa mara katika Biblia sio kwa kuwa Mwenyezi-Mungu amepotea au amejificha ila kwa kutilia mkazo jambo muhimu ambalo binadamu anapaswa kulizingatia maishani mwake - kujua atakavyo Mwenyezi-Mungu na kuzingatia hilo (Isa 55:5-7; Yoe 2:13).]

enyi mnaozitii amri zake.

Tafuteni uadilifu, tafuteni unyenyekevu;

labda mtaiepa siku ya ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu.

Maangamizi kwa mataifa ya jirani

4Mji wa Gaza utahamwa,

Ashkeloni utakuwa tupu.

Wakazi wa Ashdodi watatimuliwa mchana,

na wale wa Ekroni watang'olewa.

5Ole wenu wakazi wa nchi za pwani,

watu mnaoishi huko Krete!

Mwenyezi-Mungu ametamka dhidi yenu

enyi wakazi wa Kanaani, nchi ya Filistia:

Mimi nitawaangamiza asibaki hata mkazi mmoja!

6Nanyi nchi za pwani mtafanywa kuwa malisho;

mtakuwa vibanda vya wachungaji

na mazizi ya kondoo.

7Nchi ya pwani itamilikiwa na mabaki ya ukoo wa Yuda.

Watachunga mifugo yao huko.

Nyumba za mji wa Ashkeloni

zitakuwa mahali pao pa kulala.

Maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wao atawakumbuka

na kuwarudishia hali yao njema.

8“Nimeyasikia masuto ya Moabu

na dhihaka za Waamoni;

jinsi walivyowasuta watu wangu,

na kujigamba kuiteka nchi yao.

9Kwa hiyo, niishivyo mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi,

mimi Mungu wa Israeli,

Moabu itakuwa kama Sodoma

na Amoni itakuwa kama Gomora.

Nchi zake zitakuwa za viwavi na mashimo ya chumvi,

zitakuwa ukiwa milele.

Watu wangu watakaobaki wataziteka nyara,

watu wa taifa langu waliosalia watazimiliki.”

10Hayo yatakuwa malipo ya kiburi chao,

kwa sababu waliwadhihaki na kujigamba

dhidi ya watu wa Mwenyezi-Mungu wa majeshi.

11Mwenyezi-Mungu atakuwa wa kutisha dhidi yao;

miungu yote ya dunia ataikondesha.

Mataifa yote duniani yatamsujudia;

kila taifa katika mahali pake.

12Nanyi watu wa Kushi pia[#2:12 Ingawa Kushi ni eneo kusini mwa Misri (kwa sasa Ethiopia, Eritrea na Sudani), hapa yaweza kuhusu Misri yenyewe ambayo mnamo miaka ya 715—663 K.K. ilikuwa inatawaliwa na ukoo wa kifalme wa Kushi. Manabii wengine pia wana ujumbe juu ya Misri na Kushi (rejea Isa 18—20; Yer 46; Eze 29—32).]

mtauawa kwa upanga wake.

13Mwenyezi-Mungu atanyosha mkono wake kaskazini,[#2:13 Adui mkuu wa Israeli katika karne ya saba K.K. ilikuwa Ashuru, dola ambayo mji wake mkuu ulikuwa Ninewi (taz Yona 1:2 maelezo). Nabii anatamka kwamba Mwenyezi-Mungu ndiye aliyesababisha kuangamia kwake. Rejea Isa 10:5-34; 14:24-27; Nah 1—3.]

na kuiangamiza nchi ya Ashuru.

Ataufanya mji wa Ninewi kuwa ukiwa,

kuwa mahali pakavu kama jangwa.

14Makundi ya mifugo yatalala humo,

kadhalika kila mnyama wa porini.

Tai na yangeyange na korongo wataishi juu ya nguzo zake,

bundi watalia kwenye madirisha yake,

kunguru watalia kwenye vizingiti,

maana nyumba zake za mierezi zitakuwa tupu.

15Je, huu ndio mji uliojivuna na kuishi kwa usalama,

mji uliojisemea, “Ni mimi tu, hakuna mwingine!”

Jinsi gani umekuwa mtupu

na makao ya wanyama wa mwituni!

Kila apitaye karibu atauzomea na kuudharau.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania