1 Samweli 12

1 Samweli 12

Hotuba ya Samweli ya kuaga

1Samweli akawaambia Israeli wote, “Nimesikiliza kila kitu mlichoniambia nami nimewawekea mfalme juu yenu.

2Sasa mnaye mfalme kama kiongozi wenu. Lakini mimi ni mzee na nina mvi, nao wanangu wapo hapa pamoja nanyi. Nimekuwa kiongozi wenu tangu ujana wangu hadi siku hii ya leo.

3Mimi ninasimama hapa. Shuhudieni dhidi yangu mbele za Bwana na mpakwa mafuta wake. Nimechukua maksai wa nani? Nimechukua punda wa nani? Ni nani nimepata kumdanganya? Nimemdhulumu nani? Nimepokea rushwa kutoka kwa nani ili nifumbe macho yangu? Kama nimefanya chochote katika hivi, nitawarudishia.”

4Wakajibu, “Hujatudanganya wala kutudhulumu. Hujapokea chochote kutoka mkono wa mtu yeyote.”

5Samweli akawaambia, “Bwana ni shahidi dhidi yenu, pia mpakwa mafuta wake ni shahidi siku hii ya leo, kwamba hamkukuta chochote mkononi mwangu.”

Wakasema, “Yeye ni shahidi.”

6Kisha Samweli akawaambia watu, “Bwana ndiye alimchagua Musa na Haruni, na kuwaleta baba zenu akiwapandisha kutoka Misri.

7Sasa basi, simameni hapa, kwa sababu nitakabiliana nanyi kwa ushahidi mbele za Bwana wa matendo yote ya haki yaliyofanywa na Bwana kwenu na kwa baba zenu.

8“Baada ya Yakobo kuingia Misri, walimlilia Bwana awasaidie, naye Bwana akawatuma Musa na Haruni, ambao waliwatoa baba zenu kutoka Misri na kuwakalisha mahali hapa.

9“Lakini wakamsahau Bwana Mungu wao, hivyo Mungu akawauza katika mkono wa Sisera, jemadari wa jeshi la Hazori na katika mikono ya Wafilisti na mfalme wa Moabu, ambaye alipigana dhidi yao.

10Wakamlilia Bwana na kusema, ‘Tumetenda dhambi; tumemwacha Bwana na kutumikia Mabaali na Maashtorethi. Lakini sasa tuokoe kutoka mikono ya adui zetu, nasi tutakutumikia.’

11Ndipo Bwana akawatuma Yerub-Baali, Baraka, Yefta na Samweli, naye akawaokoa kutoka mikononi mwa adui zenu kila upande, ili ninyi mpate kukaa salama.[#12:11 pia aliitwa Gideoni]

12“Lakini mlipomwona yule Nahashi mfalme wa Waamoni anakuja dhidi yenu, mliniambia, ‘Hapana, tunataka mfalme atutawale,’ hata ingawa Bwana Mungu wenu alikuwa mfalme wenu.

13Sasa huyu hapa ndiye mfalme mliyemchagua, yule mliyeomba; tazameni, Bwana amemweka mfalme juu yenu.

14Mkimcha Bwana , na kumtumikia na kumtii, nanyi msipoasi dhidi ya amri zake, ninyi pamoja na mfalme anayewatawala mkimfuata Bwana , Mungu wenu, mambo yatakuwa mema kwenu!

15Lakini kama hamkumtii Bwana , nanyi mkaasi dhidi ya amri zake, mkono wake utakuwa dhidi yenu, kama ulivyokuwa dhidi ya baba zenu.

16“Sasa basi, simameni kimya mkaone jambo hili kubwa ambalo Bwana anaenda kulifanya mbele ya macho yenu!

17Je, sasa si mavuno ya ngano? Nitamwomba Bwana ili alete ngurumo na mvua. Nanyi mtatambua jambo hili lilivyo baya mlilolifanya mbele za macho ya Bwana mlipoomba mfalme.”

18Kisha Samweli akamwomba Bwana , na siku ile ile Bwana akatuma ngurumo na mvua. Hivyo watu wote wakamwogopa sana Bwana na Samweli.

19Watu wote wakamwambia Samweli, “Mwombe Bwana Mungu wako kwa ajili ya watumishi wako, ili tusije tukafa, kwa kuwa tumeongeza uovu juu ya dhambi zetu nyingine kwa kuomba mfalme.”

20Samweli akajibu, “Msiogope, mmefanya uovu huu wote; hata hivyo msimwache Bwana , bali mtumikieni Bwana kwa moyo wote.

21Msigeukie sanamu batili. Haziwezi kuwatendea jema, wala haziwezi kuwaokoa kwa sababu hazina maana.

22Kwa ajili ya jina lake kuu Bwana hatawakataa watu wake, kwa sababu ilimpendeza Bwana kuwafanya watu wake mwenyewe.

23Lakini iwe mbali nami kutenda dhambi dhidi ya Bwana kwa kushindwa kuwaombea. Mimi nitawafundisha njia iliyo njema na nyoofu.

24Lakini hakikisheni mnamcha Bwana na kumtumikia kwa uaminifu kwa moyo wote; tafakarini mambo makubwa aliyoyatenda kwa ajili yenu.

25Hata hivyo mkiendelea kufanya uovu, ninyi na mfalme wenu mtafutiliwa mbali!”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.