1 Samweli 8

1 Samweli 8

Israeli waomba mfalme

1Samweli alipokuwa mzee, akaweka wanawe kuwa waamuzi wa Israeli.

2Mzaliwa wa kwanza aliitwa Yoeli, na wa pili aliitwa Abiya, nao wakatumika huko Beer-Sheba.

3Lakini wanawe hawakuenenda katika njia zake. Waliziacha wakageukia faida za udanganyifu nao wakapokea rushwa na kupotosha haki.

4Basi wazee wote wa Israeli wakakusanyika pamoja na kumjia Samweli huko Rama.

5Wakamwambia, “Wewe umekuwa mzee, nao wanao hawaenendi katika njia zako, sasa tuteulie mfalme wa kutuongoza, kama ilivyo kwa mataifa mengine yote.”

6Lakini wao waliposema, “Tupe mfalme wa kutuongoza,” hili lilimchukiza Samweli, hivyo akamwomba Bwana .

7Naye Bwana akamwambia: “Sikiliza yale yote watu wanakuambia. Si wewe ambaye wamekukataa, bali wamenikataa mimi kuwa mfalme wao.

8Kama vile walivyofanya tangu siku nilipowapandisha kutoka Misri hadi siku hii ya leo; wakiniacha mimi na kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokufanyia wewe.

9Sasa wasikilize, lakini waonye sana, na uwafahamishe yale watakayotendewa na mfalme atakayewatawala.”

10Samweli akawaambia wale watu waliokuwa wakiomba wapewe mfalme maneno yote ya Bwana .

11Akasema, “Hivi ndivyo atakavyowatendea mfalme atakayewatawala. Atawachukua wana wenu na kuwafanya watumike kwa magari yake ya vita na farasi, nao watakimbia mbele ya magari yake.

12Baadhi yao atawaweka kuwa majemadari wa jeshi wa maelfu na majemadari wa jeshi wa hamsini, wengine kulima mashamba yake na kuvuna mavuno yake, pia na wengine kutengeneza silaha za vita na vifaa kwa ajili ya magari yake ya vita.

13Atawachukua binti zenu kuwa watengeneza manukato, wapishi na waokaji.

14Atayachukua mashamba yenu yaliyo mazuri, mashamba ya mizabibu na mashamba yenu ya mizeituni na kuwapa watumishi wake.

15Ataichukua sehemu ya kumi ya nafaka yenu na ya zabibu zenu na kuwapa maafisa wake na watumishi wake.

16Atawachukua watumishi wenu wa kiume na wa kike, na ngʼombe wenu walio wazuri sana na punda kwa matumizi yake mwenyewe.

17Atachukua sehemu ya kumi ya makundi yenu ya kondoo na mbuzi, na ninyi wenyewe mtakuwa watumwa wake.

18Siku ile itakapowadia, mtalia kwa kutaka msaada kutokana na mfalme mliyemchagua, naye Bwana hatawajibu.”

19Lakini watu wakakataa kumsikiliza Samweli wakasema, “Hapana! Tunataka mfalme wa kututawala.

20Kisha tutakuwa kama mataifa mengine yote, tukiwa na mfalme wa kutuongoza na kwenda mbele yetu na kutupigania vita vyetu.”

21Samweli aliposikia yote watu waliyosema, akarudia kuyasema mbele za Bwana .

22Bwana akamjibu, “Wasikilize na uwape mfalme.”

Kisha Samweli akawaambia Waisraeli, “Kila mmoja arudi mjini kwake.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.