The chat will start when you send the first message.
1Rehoboamu alipofika Yerusalemu, akakusanya nyumba ya Yuda na ya Benyamini, vijana wenye uwezo elfu mia moja na themanini, ili kufanya vita dhidi ya nyumba ya Israeli, na kuurudisha ufalme kwa Rehoboamu.
2Lakini neno hili la Bwana likamjia Shemaya mtu wa Mungu:
3“Mwambie Rehoboamu mwana wa Sulemani mfalme wa Yuda, na Waisraeli wote walio Yuda na Benyamini,
4‘Hili ndilo asemalo Bwana : Msipande kupigana dhidi ya ndugu zenu. Nendeni nyumbani, kila mmoja wenu, kwa kuwa hili nimelitenda mimi.’ ” Kwa hiyo wakalitii neno la Bwana na kurudi, wakaacha kwenda kupigana dhidi ya Yeroboamu.
5Rehoboamu akaishi Yerusalemu akajenga miji yenye ngome katika Yuda:
6Akajenga Bethlehemu, Etamu, Tekoa,
7Beth-Suri, Soko, Adulamu,
8Gathi, Maresha, Zifu,
9Adoraimu, Lakishi, Azeka,
10Sora, Aiyaloni na Hebroni. Hii ilikuwa miji yenye ngome katika Yuda na Benyamini.
11Akaimarisha ulinzi wake na kuweka majemadari ndani yake, pamoja na maghala ya vyakula, ya mafuta ya zeituni, na ya divai.
12Akaweka ngao na mikuki katika miji na kuifanya iwe imara sana. Kwa hiyo Yuda na Benyamini zikawa zake.
13Makuhani na Walawi kutoka sehemu zote za Israeli wakawa upande wake.
14Pia Walawi wakaacha maeneo yao ya malisho na mali yao, wakaja Yuda na Yerusalemu kwa sababu Yeroboamu na wanawe walikuwa wamewakataa wasiwe makuhani wa Bwana .
15Naye akawa amechagua makuhani wake mwenyewe kwa ajili ya mahali pa juu pa kuabudia sanamu za mbuzi na za ndama ambazo alikuwa ametengeneza.
16Wale waliotoka katika kila kabila la Israeli ambao walielekeza mioyo yao kumtafuta Bwana , Mungu wa Israeli, wakawafuata Walawi huko Yerusalemu kumtolea Bwana dhabihu, Mungu wa baba zao.
17Wakaimarisha ufalme wa Yuda na kumuunga mkono Rehoboamu mwana wa Sulemani miaka mitatu, wakienenda katika njia za Daudi na Sulemani katika wakati huu.
18Rehoboamu alimwoa Mahalati aliyekuwa binti Yeremothi mwana wa Daudi; mamaye alikuwa Abihaili binti Eliabu mwana wa Yese.
19Mahalati alimzalia Rehoboamu wana: Yeushi, Shemaria na Zahamu.
20Kisha akamwoa Maaka binti Absalomu, aliyemzalia Abiya, Atai, Ziza na Shelomithi.
21Rehoboamu akampenda Maaka binti Absalomu kuliko wakeze wengine na masuria wake. Kwa jumla alikuwa na wake kumi na wanane na masuria sitini, wana ishirini na wanane na binti sitini.
22Rehoboamu akamweka Abiya mwana wa Maaka, kuwa mkuu wa wana wa mfalme miongoni mwa ndugu zake ili amfanye mfalme.
23Akatenda kwa busara, akiwasambaza baadhi ya wanawe katika wilaya zote za Yuda na Benyamini, pamoja na miji yote yenye ngome. Akawapa mahitaji tele na kuwaoza wake wengi.