The chat will start when you send the first message.
1Roho wa Mungu akamjia Azaria mwana wa Odedi.
2Akatoka ili kumlaki Asa na kumwambia, “Nisikilizeni, Asa na Yuda wote na Benyamini. Bwana yu pamoja nanyi mkiwa pamoja naye. Mkimtafuta, ataonekana kwenu, lakini mkimwacha, naye atawaacha.
3Kwa muda mrefu Israeli walikuwa hawana Mungu wa kweli, walikuwa hawana kuhani wa kuwafundisha na wala hawakuwa na sheria.
4Lakini katika taabu yao walimrudia Bwana , Mungu wa Israeli, na kumtafuta, naye akaonekana kwao.
5Katika siku hizo hapakuwa na amani kwa yeyote aliyesafiri, kutoka wala kuingia, kwa kuwa wakazi wote wa nchi walikuwa katika machafuko makubwa.
6Taifa moja lilipigana na taifa lingine na mji mmoja ukapigana na mji mwingine, kwa sababu Mungu alikuwa anawahangaisha kwa taabu za kila aina.
7Lakini ninyi, kuweni hodari wala msikate tamaa, kwa kuwa mtapata thawabu kwa kazi yenu.”
8Asa aliposikia maneno haya na unabii wa Azaria mwana wa Odedi yule nabii, akajipa moyo. Akaziondoa sanamu zote zilizokuwa machukizo katika nchi yote ya Yuda na Benyamini, na kutoka miji aliyoiteka katika nchi ya vilima ya Efraimu. Akakarabati madhabahu ya Bwana iliyokuwa mbele ya ukumbi wa Hekalu la Bwana .
9Kisha akakutanisha Yuda wote, Benyamini na watu kutoka Efraimu, watu wa Manase na Simeoni walioishi miongoni mwao, kwa maana idadi kubwa walikuwa wamemjia kutoka Israeli walipoona kwamba Bwana Mungu wake alikuwa pamoja naye.
10Basi wakakusanyika huko Yerusalemu mwezi wa tatu katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Asa.
11Wakati huo wakamtolea Bwana dhabihu za ngʼombe mia saba, kondoo na mbuzi elfu saba kutoka nyara walizoteka.
12Wakafanya agano kumtafuta Bwana , Mungu wa baba zao, kwa moyo wao wote na kwa roho yao yote.
13Wale wote ambao hawangemtafuta Bwana , Mungu wa Israeli, wangelazimika kuuawa, akiwa mdogo au mkubwa, mwanaume au mwanamke.
14Wakamwapia Bwana kwa sauti kuu, kwa kelele, na kupiga tarumbeta na mabaragumu.
15Yuda wote wakafurahia kile kiapo kwa sababu walikuwa wameapa kwa moyo wao wote. Wakamtafuta Mungu kwa bidii, naye akaonekana kwao. Kwa hiyo Bwana akawapa amani pande zote.
16Mfalme Asa akamwondolea Maaka, bibi yake, wadhifa wake kama mama malkia kwa sababu alikuwa ametengeneza nguzo ya Ashera ya kuchukiza. Asa akaikata hiyo nguzo, akaivunjavunja na kuiteketeza kwa moto katika Bonde la Kidroni.
17Ijapokuwa hakuondoa mahali pa juu pa kuabudia katika Israeli, moyo wa Asa ulikuwa umejiweka kwa Bwana kikamilifu maisha yake yote.
18Akaleta ndani ya Hekalu la Mungu fedha na dhahabu na vile vyombo ambavyo yeye na baba yake walikuwa wameviweka wakfu.
19Hapakuwa na vita tena hadi mwaka wa thelathini na tano wa utawala wake Asa.