The chat will start when you send the first message.
1Baada ya mambo haya yote kumalizika, Waisraeli ambao walikuwa huko wakaenda kwenye miji ya Yuda, wakayavunja yale mawe ya kuabudia na kuzikatakata zile nguzo za Ashera. Wakabomoa mahali pa juu pa kuabudia pamoja na madhabahu zake kila mahali katika Yuda na Benyamini, na katika Efraimu na Manase. Baada ya kuviharibu hivi vyote, Waisraeli wakarudi miji yao wenyewe na kwenye milki zao.
2Hezekia akawapanga makuhani na Walawi katika migawanyo, kila mgawanyo kulingana na wajibu wao, kama ni makuhani au Walawi, ili kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, kuhudumu, kushukuru na kuimba sifa katika malango ya makao ya Bwana .
3Mfalme akatoa matoleo kutoka mali yake mwenyewe kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa za asubuhi na za jioni na sadaka za kuteketezwa kwa siku za Sabato, kwa Sikukuu za Mwezi Mwandamo na kwa ajili ya sikukuu zilizoamriwa kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Bwana .
4Akawaagiza watu wanaoishi Yerusalemu watoe sehemu iliyo haki ya makuhani na Walawi ili waweze kujitoa kikamilifu kutimiza wajibu wao katika Sheria ya Bwana .
5Mara tu baada ya kutolewa tangazo hilo, Waisraeli wakatoa kwa ukarimu malimbuko ya nafaka zao, divai mpya, mafuta na asali pamoja na vyote vilivyotoka mashambani. Wakaleta kiasi kikubwa cha fungu la kumi la kila kitu.
6Watu wa Israeli na Yuda walioishi katika miji ya Yuda wakaleta pia fungu la kumi la makundi yao ya ngʼombe na makundi ya kondoo na mbuzi pia na fungu la kumi la vitu vitakatifu vilivyowekwa wakfu kwa ajili ya Bwana Mungu wao na kuvikusanya katika malundo.
7Wakaanza kufanya haya katika mwezi wa tatu na kumaliza katika mwezi wa saba.
8Hezekia na maafisa wake walipokuja na kuona yale malundo, wakamsifu Bwana na kuwabariki watu wake Israeli.
9Hezekia akawauliza makuhani na Walawi kuhusu yale malundo,
10naye Azaria aliyekuwa kuhani mkuu, kutoka jamaa ya Sadoki, akajibu, “Tangu watu walipoanza kuleta sadaka zao katika Hekalu la Bwana tumekuwa na chakula cha kutosha na vingi vya kuweka akiba kwa sababu Bwana amewabariki watu wake, hivyo tumekuwa na kiasi kingi kilichobaki.”
11Hezekia akatoa agizo la kutengeneza vyumba vya ghala katika Hekalu la Bwana nalo hili likafanyika.
12Kisha kwa uaminifu wakaleta sadaka zao, mafungu yao ya kumi na vitu vilivyowekwa wakfu. Konania Mlawi, ndiye alikuwa msimamizi wa vitu hivi na Shimei ndugu yake ndiye alikuwa msaidizi wake.
13Yehieli, Azazia, Nahathi, Asaheli, Yeremothi, Yozabadi, Elieli, Ismakia, Mahathi na Benaya walikuwa waangalizi chini ya Konania na Shimei ndugu yake, waliokuwa wamewekwa na Mfalme Hezekia na Azaria, afisa msimamizi wa Hekalu la Mungu.
14Kore mwana wa Imna, Mlawi, bawabu wa Lango la Mashariki, alikuwa msimamizi wa sadaka za hiari zilizotolewa kwa Mungu, akiyagawanya hayo matoleo yaliyotolewa kwa Bwana na pia zile sadaka zilizowekwa wakfu.
15Edeni, Miniamini, Yeshua, Shemaya, Amaria na Shekania walimsaidia kwa uaminifu katika miji ya makuhani, wakiwagawia makuhani wenzao kufuatana na migawanyo yao, wazee kwa vijana sawasawa.
16Zaidi ya hao wakawagawia wanaume wenye umri wa miaka mitatu au zaidi ambao majina yao yalikuwa kwenye orodha ya vizazi, wale wote ambao wangeingia katika Hekalu la Bwana ili kufanya kazi zao mbalimbali za kila siku kulingana na wajibu katika mgawanyo wao.
17Kuandikishwa kwa makuhani kulikuwa kwa kufuata chimbuko la nyumba za baba zao na Walawi kuanzia umri wa miaka ishirini au zaidi ilikuwa kufuatana na huduma zao, kwa migawanyo yao.
18Makuhani waliandikishwa pamoja na watoto wao wadogo, wake zao, watoto wao wa kiume na wa kike, jamii yote iliandikishwa kwa kufuata orodha ya vizazi vyao. Kwa kuwa walikuwa waaminifu katika kujitakasa.
19Kuhusu makuhani, wazao wa Haruni walioishi kwenye mashamba yaliyozunguka miji yao au katika miji mingine yoyote, watu walitajwa majina ili kumgawia kila mwanaume miongoni mwao na kwa wote waliokuwa katika orodha ya vizazi vya Walawi.
20Hivi ndivyo Hezekia alivyofanya katika Yuda yote, akifanya lile lililo jema, sawa na la uaminifu mbele za Bwana Mungu wake.
21Katika kila kitu alichofanya katika huduma kwenye Hekalu la Mungu na katika kutii sheria na amri, alimtafuta Mungu wake na kufanya kazi kwa moyo wake wote. Naye hivyo akafanikiwa.