Kumbukumbu 16

Kumbukumbu 16

Pasaka

(Kut 12:1‑20)

1Shikeni mwezi wa Abibu, na kuiadhimisha Pasaka ya Bwana Mungu wenu, kwa sababu katika mwezi wa Abibu, Mungu aliwatoa Misri usiku.

2Mtatoa dhabihu ya Pasaka ya mnyama kwa Bwana Mungu wenu kutoka kundi lenu la mbuzi na kondoo, au la ngʼombe, mahali atakapopachagua Bwana kuwa makao kwa ajili ya Jina lake.

3Msile nyama hiyo pamoja na mikate iliyotiwa chachu, lakini kwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu, mikate ya kujitesa, kwa sababu mliondoka Misri kwa haraka, ili siku zote za maisha yenu mpate kukumbuka wakati wenu wa kuondoka Misri.

4Chachu isionekane kwenu katika nchi yenu yote kwa siku saba. Nyama yoyote ya dhabihu mtakayotoa jioni ya siku ya kwanza isibakizwe hadi asubuhi.

5Kamwe msitoe dhabihu ya Pasaka katika mji wowote ambao Bwana Mungu wenu amewapa,

6isipokuwa mahali atakapopachagua kuwa makao kwa ajili ya Jina lake. Hapo lazima mtoe dhabihu ya Pasaka jioni jua litakapotua, iwe kumbukumbu yenu ya kutoka Misri.

7Okeni na mle mahali atakapopachagua Bwana Mungu wenu, kisha asubuhi mrudi kwenye mahema yenu.

8Kwa siku sita mtakula mikate isiyotiwa chachu na siku ya saba fanyeni kusanyiko kwa ajili ya Bwana Mungu wenu na msifanye kazi.

Sikukuu ya Mavuno

(Kut 34:22; Law 23:15‑21)

9Mhesabu majuma saba tangu wakati mnapoanza kuchukua mundu kuvuna nafaka.

10Kisha msherehekee Sikukuu ya Majuma kwa Bwana Mungu wenu kwa kutoa sadaka ya hiari kwa kadiri ya baraka ambayo Bwana Mungu wenu amewapa.

11Shangilieni mbele za Bwana Mungu wenu mahali atakapopachagua kuwa makao ya Jina lake, ninyi, wana wenu na binti zenu, watumishi wenu wa kiume na wa kike, Walawi walio katika miji yenu, na wageni, yatima na wajane wanaoishi miongoni mwenu.

12Kumbukeni kwamba mlikuwa watumwa kule Misri na mfuate amri hizi kwa uangalifu.

Sikukuu ya Vibanda

(Law 23:33‑43)

13Adhimisheni sikukuu ya vibanda kwa siku saba baada ya kukusanya mazao kutoka sakafu yako ya kupuria nafaka, na kutoka shinikizo lako la kukamulia zabibu.

14Mfurahie sikukuu yenu, ninyi, wana wenu, binti zenu, watumishi wenu wa kiume na wa kike, Walawi, wageni, yatima na wajane ambao wanaishi katika miji yenu.

15Kwa siku saba mtaiadhimisha sikukuu ya Bwana Mungu wenu katika mahali atakapopachagua Bwana . Kwa kuwa Bwana Mungu wenu atawabariki katika mavuno yenu na katika kazi zote za mikono yenu na furaha yenu itakamilika.

16Wanaume wenu wote lazima wajitokeze mara tatu kwa mwaka mbele za Bwana Mungu wenu mahali atakapopachagua: kwa ajili ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, Sikukuu ya Majuma, na Sikukuu ya Vibanda. Hakuna mtu atakayejitokeza mbele za Bwana mikono mitupu:

17Kila mmoja wenu ni lazima alete zawadi kulingana na jinsi Bwana Mungu wenu alivyowabariki.

Waamuzi

18Wateue waamuzi na maafisa kwa kila kabila lenu katika kila mji ambao Bwana Mungu wenu anawapa, nao watawaamua watu kwa usawa.

19Msipotoshe haki wala msifanye upendeleo. Msikubali rushwa kwa sababu rushwa hupofusha macho ya wenye busara na kugeuza maneno ya wenye haki.

20Mfuate haki na haki peke yake, ili mweze kuishi na kuimiliki nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa.

Kuabudu miungu mingine

21Msisimamishe nguzo yoyote ya Ashera kando ya madhabahu mliyomjengea Bwana Mungu wenu,

22wala msisimamishe jiwe la kuabudu, kwa maana Bwana Mungu wenu anavichukia vitu hivi.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.