Kumbukumbu 26

Kumbukumbu 26

Malimbuko na zaka

1Mtakapokuwa mmeingia nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa kama urithi na mtakapokuwa mmeimiliki na kukaa ndani yake,

2chukueni baadhi ya mavuno ya kwanza ya yale yote mtakayozalisha kutoka udongo wa nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa na mweke kwenye kapu. Kisha uende mahali Bwana Mungu wako atakapopachagua kuwa makao kwa ajili ya Jina lake,

3na umwambie kuhani atakayekuwepo wakati huo, “Ninatangaza leo kwa Bwana , Mungu wako, kwamba nimekuja katika nchi ambayo Bwana aliwaapia baba zetu kwamba atatupa.”

4Kuhani atapokea lile kapu mikononi mwako na kuliweka chini mbele ya madhabahu ya Bwana Mungu wako.

5Kisha utatangaza mbele za Bwana Mungu wako: “Baba yangu alikuwa Mwaramu aliyekuwa anatangatanga, akaenda Misri pamoja na watu wachache, akaishi huko hadi akawa taifa kubwa, lenye nguvu na watu wengi.

6Lakini Wamisri walituonea na kututaabisha, wakitufanyisha kazi ngumu.

7Kisha tulimlilia Bwana , Mungu wa baba zetu, naye Bwana akasikia sauti yetu na akaona huzuni yetu, taabu yetu na mateso yetu.

8Kwa hiyo Bwana akatutoa nchi ya Misri kwa mkono wenye nguvu na ulionyooshwa, pamoja na utisho mkuu, ishara za miujiza na maajabu.

9Akatuleta mahali hapa akatupatia nchi hii, nchi inayotiririka maziwa na asali;

10nami sasa ninaleta malimbuko ya ardhi ambayo wewe, Ee Bwana , umenipa.” Weka kapu mbele za Bwana Mungu wako na usujudu mbele zake.

11Kisha wewe pamoja na Walawi na wageni wote walio miongoni mwenu mtafurahi katika vitu vyote vizuri ambavyo Bwana Mungu wenu amewapa pamoja na wa nyumbani mwenu.

12Utakapokuwa umeshatoa zaka zote za mazao yako katika mwaka wa tatu, ambao ni mwaka wa zaka, utampa Mlawi, mgeni, yatima na mjane, ili waweze kula katika miji yenu na kushiba.

13Kisha umwambie Bwana Mungu wako: “Nimeondoa katika nyumba yangu ile sehemu iliyowekwa wakfu na nimempa Mlawi, mgeni, yatima na mjane, kulingana na yote uliyoamuru. Sijazihalifu amri zako wala kusahau hata mojawapo.

14Sijala sehemu iliyowekwa wakfu wakati nilipokuwa nikiomboleza, wala sijaondoa mojawapo wakati nilipokuwa najisi, wala sijatoa sehemu yake yoyote kwa wafu. Nimemtii Bwana Mungu wangu; nimefanya kila kitu ulichoniamuru.

15Angalia chini kutoka mbinguni, maskani yako takatifu, uwabariki watu wako Israeli pamoja na nchi uliyotupatia kama ulivyoahidi kwa kiapo kwa baba zetu, nchi inayotiririka maziwa na asali.”

Fuata maagizo ya Bwana

16Bwana Mungu wako anakuagiza leo kufuata amri hizi na sheria; zingatia kwa makini kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote.

17Umetangaza leo kwamba Bwana ndiye Mungu wako na kwamba utafuata njia zake, kwamba utayashika maagizo yake, amri zake na sheria zake nawe utamtii.

18Naye Bwana ametangaza leo kwamba ninyi ni taifa lake, hazina yake ya pekee kama alivyoahidi, ili mpate kuyashika maagizo yake yote.

19Ametangaza kwamba atawaweka juu kuliko mataifa mengine aliyoyafanya katika sifa, kuwa fahari na heshima, na kwamba mtakuwa taifa takatifu kwa Bwana Mungu wenu, kama alivyoahidi.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.