The chat will start when you send the first message.
1Hii ndiyo baraka Musa mtu wa Mungu aliyotamka kwa Waisraeli kabla ya kifo chake.
2Alisema:
“Bwana alikuja kutoka Mlima Sinai,
akachomoza kama jua juu yao
kutoka Mlima Seiri,
akaangaza kutoka Mlima Parani.
Alikuja pamoja na watakatifu makumi elfu
kutoka kusini,
kutoka miteremko ya mlima wake.
3Hakika ni wewe ambaye huwapenda watu,
watakatifu wako wote wamo mkononi mwako.
Miguuni pako wote wanasujudu,
na kutoka kwako wanapokea mafundisho,
4sheria ile Musa aliyotupatia sisi,
tulio milki ya kusanyiko la Yakobo.
5Alikuwa mfalme juu ya Yeshuruni[#33:5 maana yake Yeye aliye mnyofu , yaani Israeli]
wakati viongozi wa watu walipokusanyika,
pamoja na makabila ya Israeli.
6“Reubeni na aishi, asife,
wala watu wake wasiwe wachache.”
7Akasema hili kuhusu Yuda:
“Ee Bwana , sikia kilio cha Yuda,
mlete kwa watu wake.
Kwa mikono yake mwenyewe hujitetea.
Naam, uwe msaada wake
dhidi ya adui zake!”
8Kuhusu Lawi alisema:
“Thumimu yako na Urimu yako ulimpa,
mtu yule uliyemfadhili.
Ulimjaribu huko Masa
na kushindana naye
kwenye maji ya Meriba.
9Alinena hivi kuhusu baba yake na mama yake,
‘Mimi siwahitaji kamwe.’
Akawasahau jamaa zake,
asiwatambue hata watoto wake,
lakini akaliangalia neno lako
na kulilinda agano lako.
10Humfundisha Yakobo mausia yako
na Israeli sheria yako.
Hufukiza uvumba mbele zako
na sadaka nzima za kuteketezwa
juu ya madhabahu yako.
11Ee Bwana , bariki ustadi wake wote,
nawe upendezwe na kazi ya mikono yake.
Vipige viuno vya wale wainukao dhidi yake;
wapige adui zake hata wasiinuke tena.”
12Kuhusu Benyamini akasema:
“Mwache mpendwa wa Bwana
apumzike salama kwake,
kwa maana humkinga mchana kutwa,
na yule Bwana ampendaye
hupumzika kati ya mabega yake.”
13Kuhusu Yusufu akasema:
“Bwana na aibariki nchi yake
kwa umande wa thamani
kutoka juu mbinguni,
na vilindi vya maji
vilivyotulia chini;
14pamoja na vitu vilivyo bora sana
viletwavyo na jua,
na vitu vizuri sana vinavyoweza
kutolewa na mwezi;
15pamoja na zawadi bora sana
za milima ya zamani
na kwa wingi wa baraka
za vilima vya milele;
16pamoja na baraka nzuri mno
za ardhi na ukamilifu wake,
na upendeleo wake yeye
aliyeishi kwenye kichaka
kilichokuwa kinawaka moto.
Hivi vyote na vikae juu ya kichwa cha Yusufu,
juu ya paji la uso la aliye mkuu
miongoni mwa ndugu zake.
17Katika fahari yeye ni kama fahali mzaliwa wa kwanza;
pembe zake ni pembe za nyati,
na kwa pembe hizo atapiga mataifa,
hata yaliyo miisho ya dunia.
Hivyo ndivyo yalivyo makumi elfu ya Efraimu;
hivyo ndivyo yalivyo maelfu ya Manase.”
18Kuhusu Zabuloni akasema:
“Shangilia, Zabuloni, wakati wa kutoka nje,
nawe Isakari, katika mahema yako.
19Watawaita mataifa kwenye mlima,
na huko mtatoa dhabihu za haki;
watajifurahisha kwa wingi uliojaza bahari,
kwa hazina zilizofichwa mchangani.”
20Kuhusu Gadi akasema:
“Atabarikiwa yeye aongezaye milki ya Gadi!
Gadi huishi huko kama simba,
akirarua kwenye mkono au kichwa.
21Alijichagulia nchi nzuri kuliko zote
kwa ajili yake mwenyewe;
fungu la kiongozi lilikuwa limehifadhiwa
kwa ajili yake.
Viongozi wa watu walipokusanyika,
alitimiza haki ya mapenzi ya Bwana ,
na hukumu zake kuhusu Israeli.”
22Kuhusu Dani akasema:
“Dani ni mwana simba,
akiruka kutoka Bashani.”
23Kuhusu Naftali akasema:
“Naftali amejaa tele upendeleo wa Bwana ,
naye amejaa baraka yake;
atarithi magharibi na kusini.”
24Kuhusu Asheri akasema:
“Aliyebarikiwa zaidi sana katika wana ni Asheri;
yeye na apate upendeleo kwa ndugu zake,
yeye na anawe miguu yake kwenye mafuta.
25Makomeo ya malango yako yawe chuma na shaba,
nazo nguvu zako zitakuwa sawa na siku zako.
26“Hakuna mwingine kama Mungu wa Yeshuruni,
ambaye hupanda juu ya mbingu ili akusaidie,
na juu ya mawingu katika utukufu wake.
27Mungu wa milele ni kimbilio lako,
na chini kuna mikono ya milele.
Atamfukuza adui yako mbele yako,
akisema, ‘Mwangamize yeye!’
28Hivyo Israeli ataishi salama peke yake.
Mzao wa Yakobo ni salama
katika nchi ya nafaka na divai mpya,
mahali mbingu hudondosha umande.
29Ee Israeli, wewe umebarikiwa!
Ni nani kama wewe,
taifa lililookolewa na Bwana ?
Yeye ni ngao yako na msaada wako,
na upanga wako uliotukuka.
Adui zako watatetemeka mbele yako,
nawe utapakanyaga
mahali pao pa juu.”