The chat will start when you send the first message.
1Haya ndio maagizo, amri na sheria ambazo Bwana Mungu wenu aliniagiza niwafundishe ninyi ili mpate kuyashika katika nchi ambayo ninyi mnavuka Yordani kuimiliki,
2ili ninyi, watoto wenu na watoto wao baada yao wamche Bwana Mungu wenu siku zote kwa kushika amri na maagizo yake yote ninayowapa, ili mweze kuyafurahia maisha marefu.
3Sikia, ee Israeli, nawe uwe mwangalifu kutii ili upate kufanikiwa na kuongezeka sana katika nchi inayotiririka maziwa na asali, kama Bwana , Mungu wa baba zenu, alivyowaahidi ninyi.
4Sikia, ee Israeli: Bwana Mungu wako, Bwana ni mmoja.
5Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.
6Amri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako.
7Wafundishe watoto wako kwa bidii. Nena kuhusu amri hizi uketipo nyumbani na wakati utembeapo njiani, ulalapo na uamkapo.
8Zifunge kama alama juu ya mkono wako, na uzifunge juu ya paji la uso wako.
9Ziandike kwenye miimo ya milango ya nyumba yako na juu ya malango yako.
10Bwana Mungu wako atakapokuleta katika nchi aliyowaapia baba zako, Abrahamu, Isaka na Yakobo, kukupa wewe, nchi kubwa, yenye miji inayopendeza ambayo hukuijenga,
11nyumba zilizojaa vitu vizuri vya aina nyingi ambavyo hukuvijaza, visima ambavyo hukuchimba, na mashamba ya mizabibu na mizeituni ambayo hukupanda wewe, basi, utakapokula na kushiba,
12jihadhari usije ukamwacha Bwana , aliyekutoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa.
13Utamcha Bwana Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake na kuapa kwa jina lake.
14Usifuate miungu mingine, miungu ya mataifa yanayokuzunguka;
15kwa kuwa Bwana Mungu wako, ambaye yuko katikati yako, ni Mungu mwenye wivu na hasira yake itawaka dhidi yako, naye atakuangamiza kutoka uso wa nchi.
16Usimjaribu Bwana Mungu wako kama ulivyomjaribu huko Masa.
17Utayashika maagizo ya Bwana Mungu wako kwa bidii, na masharti na amri alizokupa.
18Fanya lililo haki na jema mbele za Bwana , ili upate kufanikiwa, uweze kuingia na kuimiliki nchi nzuri ambayo Bwana aliahidi kwa kiapo kwa baba zako,
19kuwafukuza kwa nguvu adui zako mbele yako kama Bwana alivyosema.
20Siku zijazo, mtoto wako atakapokuuliza, “Ni nini maana ya masharti haya, amri na sheria hizi ambazo Bwana Mungu wako alikuagiza wewe?”
21Mwambie: “Tulikuwa watumwa wa Farao huko Misri, lakini Bwana alitutoa sisi kutoka Misri kwa mkono wenye nguvu.
22Machoni petu, Bwana alitenda ishara za miujiza na maajabu makubwa na ya kutisha mno dhidi ya Misri, na dhidi ya Farao na nyumba yake yote.
23Lakini Mungu akatutoa huko, akatuleta na kutupatia nchi hii ambayo aliwaahidi baba zetu kwa kiapo.
24Bwana akatuagiza tutii amri hizi zote na kumcha Bwana Mungu wetu, ili tupate kustawi na kuendelea kuwa hai kama ilivyo leo.
25Tukizitii kwa bidii amri hizi zote mbele za Bwana Mungu wetu, kama alivyotuamuru sisi, hiyo itakuwa haki yetu.”