Ezekieli 1

Ezekieli 1

Viumbe hai na utukufu wa Bwana

1Katika mwaka wa thelathini, mwezi wa nne, siku ya tano ya mwezi, nilipokuwa miongoni mwa waliokuwa uhamishoni kando ya Mto Kebari, mbingu zilifunguka nami nikaona maono ya Mungu.

2Katika siku ya tano ya mwezi, mwaka wa tano wa kuhamishwa kwa Mfalme Yehoyakini,

3neno la Bwana lilimjia Ezekieli kuhani, mwana wa Buzi, kando ya Mto Kebari, katika nchi ya Wakaldayo. Huko mkono wa Bwana ulikuwa juu yake.

4Nilitazama, nikaona dhoruba kubwa ikitoka kaskazini: wingu kubwa sana likiwa na miali ya radi, likizungukwa na mwanga mkali. Katikati ya huo moto kulikuwa kama chuma inavyongʼaa ndani ya moto.

5Ndani ya ule moto kulikuwa na mfano wa viumbe wanne wenye uhai. Kuonekana kwao walikuwa na umbo la mwanadamu,

6lakini kila mmoja alikuwa na nyuso nne na mabawa manne.

7Miguu yao ilikuwa imenyooka; nyayo za miguu yao zilikuwa kama kwato za miguu ya ndama, nazo zilimetameta kama shaba iliyosuguliwa.

8Chini ya mabawa yao katika pande zao nne walikuwa na mikono ya mwanadamu. Wote wanne walikuwa na nyuso na mabawa,

9nayo mabawa yao yaligusana. Kila mmoja alienda kuelekea mbele moja kwa moja; hawakugeuka walipotembea.

10Kuonekana kwa nyuso zao kulikuwa hivi: Kila mmoja wa hao wanne alikuwa na uso wa mwanadamu, na kwa upande wa kulia kila mmoja alikuwa na uso wa simba, na kwa upande wa kushoto alikuwa na uso wa ngʼombe; pia kila mmoja alikuwa na uso wa tai.

11Hivyo ndivyo zilivyokuwa nyuso zao. Kila mmoja wao alikuwa na mabawa mawili yaliokunjuliwa kuelekea juu; kila bawa liligusa bawa la mwenzake kila upande; kila mmoja wao alikuwa na mabawa mawili yaliyofunika mwili wake.

12Kila mmoja alienda kuelekea mbele moja kwa moja. Popote roho alipoenda, walienda pasipo kugeuka.

13Kuonekana kwa wale viumbe hai kulikuwa kama makaa ya mawe yanayowaka au kama mienge. Moto ule ulikuwa ukienda mbele na nyuma katikati ya wale viumbe; ulikuwa na mwangaza mkali na katika ule moto kulitoka miali ya radi.

14Wale viumbe walipiga mbio kwenda na kurudi, kama miali ya radi.

15Nilipokuwa nikitazama wale viumbe hai, niliona gurudumu moja juu ya ardhi kando ya kila kiumbe na nyuso zake nne.

16Hivi ndivyo ilivyokuwa kuonekana kwa hayo magurudumu na muundo wake: yalimetameta kama zabarajadi, nayo yote manne yalifanana. Kila gurudumu lilionekana kuwa na gurudumu lingine ndani yake.

17Magurudumu yalipoenda, yalielekea upande mmoja wa pande nne walikoelekea wale viumbe; wale viumbe walipoenda, magurudumu hayakugeuka.

18Kingo za magurudumu zilikuwa ndefu kwenda juu na za kutisha, nazo zote nne zilijawa na macho pande zote.

19Wale viumbe hai walipoenda, magurudumu yaliyokuwa kando yao yalisogea; wakati hao viumbe hai walipoinuka kutoka ardhini, magurudumu nayo yaliinuka.

20Popote roho alipoenda, wale viumbe nao walienda, nayo magurudumu yaliinuka pamoja nao, kwa sababu roho ya wale viumbe hai alikuwa ndani ya hayo magurudumu.

21Viumbe wale waliposogea, nayo magurudumu yalisogea; viumbe waliposimama, nayo pia yalisimama; viumbe walipoinuka juu ya nchi, magurudumu yaliinuka pamoja nao, kwa kuwa roho ya hao viumbe hai alikuwa ndani ya hayo magurudumu.

22Juu ya vichwa vya hao viumbe hai palikuwa na kitu mfano wa eneo lililokuwa wazi, lililokuwa angavu kabisa na la kutisha.

23Chini ya hiyo nafasi, mabawa yao yalitanda moja kuelekea lingine, na kila mmoja alikuwa na mabawa mawili yaliyofunika mwili wake.

24Viumbe wale waliposogea, nilisikia sauti ya mabawa yao, kama ngurumo ya maji yaendayo kasi, kama sauti ya Mwenyezi, kama kishindo cha jeshi. Waliposimama, walishusha mabawa yao.[#1:24 Mwenyezi hapa ina maana ya Shaddai kwa Kiebrania.]

25Ndipo ikaja sauti toka juu ya ile nafasi ya wazi iliyokuwa juu ya vichwa vyao, waliposimama mabawa yao yakiwa yameshushwa.

26Juu ya ile nafasi ya wazi iliyokuwa juu ya vichwa vyao, kulikuwa na kitu mfano wa kiti cha utawala cha yakuti samawi. Na juu ya kile kiti cha utawala kulikuwa na umbo, mfano wa mwanadamu.

27Nikaona kwamba kutokana na kile kilichoonekana kuwa kiuno chake kuelekea juu, alionekana kama chuma inavyongʼaa ikiwa ndani ya moto, na kuanzia kiuno kwenda chini alionekana kama moto; mwanga wenye kungʼaa sana ulimzunguka.

28Kama vile kuonekana kwa upinde wa mvua mawinguni siku ya mvua, ndivyo ulivyokuwa ule mngʼao uliomzunguka.

Hivi ndivyo mfano wa utukufu wa Bwana ulionekana. Nilipouona, nikaanguka kifudifudi, nikasikia sauti ya mtu anaongea.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.