Ezekieli 21

Ezekieli 21

Babeli, upanga wa Mungu wa hukumu

1Neno la Bwana likanijia kusema:

2“Mwanadamu, uelekeze uso wako juu ya Yerusalemu na uhubiri dhidi ya mahali patakatifu. Tabiri dhidi ya nchi ya Israeli

3uiambie: ‘Hili ndilo asemalo Bwana : Mimi niko kinyume nawe. Nitautoa upanga wangu kwenye ala yake na kumkatilia mbali mwenye haki na mwovu.

4Kwa sababu nitamkatilia mbali mwenye haki na mwovu, upanga wangu utatolewa alani mwake uwe dhidi ya kila mtu kuanzia kusini hadi kaskazini.

5Ndipo watu wote watajua ya kuwa Mimi Bwana nimeutoa upanga wangu kwenye ala yake, nao hautarudi humo tena.’

6“Kwa hiyo lia kwa uchungu, mwanadamu! Lia kwa uchungu mbele yao kwa moyo uliopondeka na kwa huzuni nyingi.

7Nao watakapokuuliza, ‘Kwa nini unalia kwa uchungu?’ Utasema hivi, ‘Kwa sababu ya habari zinazokuja. Kila moyo utayeyuka na kila mkono utalegea, kila roho itazimia na kila goti litalegea kama maji.’ Habari hizo zinakuja! Hakika zitatendeka, asema Bwana Mwenyezi.”

8Neno la Bwana likanijia, kusema:

9“Mwanadamu, tabiri na useme, ‘Hili ndilo asemalo Bwana:

“ ‘Upanga, upanga,

ulionolewa na kusuguliwa:

10umenolewa kwa ajili ya mauaji,

umesuguliwa ili ungʼae kama miali ya radi!

“ ‘Je, tuifurahie fimbo ya utawala ya mwanangu Yuda? Upanga unadharau kila fimbo kama hiyo.

11“ ‘Upanga umewekwa tayari ili kusuguliwa,

ili upate kushikwa mkononi,

umenolewa na kusuguliwa,

umewekwa tayari kwa mkono wa muuaji.

12Piga kelele na uomboleze, ee mwanadamu,

kwa kuwa upanga u dhidi ya watu wangu;

u dhidi ya wakuu wote wa Israeli.

Wametolewa wauawe kwa upanga

pamoja na watu wangu.

Kwa hiyo pigapiga kifua chako.

13“ ‘Lazima kuwe na kujaribiwa. Itakuwaje basi ikiwa fimbo ya ufalme ya Yuda inayodharauliwa na upanga haitakuwepo tena? asema Bwana Mwenyezi.’

14“Hivyo basi, mwanadamu, tabiri

na ukapige makofi.

Upanga wako na upige mara mbili,

naam, hata mara tatu.

Ni upanga wa mauaji,

upanga wa mauaji makuu,

ukiwashambulia kutoka kila upande.

15Ili mioyo ipate kuyeyuka

na wanaouawa wawe wengi,

nimeweka upanga wa mauaji

kwenye malango yao yote.

Lo! Umetengenezwa umetemete kama miali ya radi,

umeshikwa kwa ajili ya kuua.

16Ee upanga, kata upande wa kuume,

kisha upande wa kushoto,

mahali popote makali yako yatakapoelekezwa.

17Mimi nami nitapiga makofi,

nayo ghadhabu yangu itapungua.

Mimi Bwana nimesema.”

18Neno la Bwana likanijia kusema:

19“Mwanadamu, weka alama njia mbili ambazo upanga wa mfalme wa Babeli utapitia, njia hizo zikianzia katika nchi hiyo hiyo. Weka kibao pale ambapo njia zinagawanyika kuelekea mjini.

20Weka alama njia moja kwa ajili ya upanga upate kuja dhidi ya Raba ya Waamoni na nyingine upate kuja dhidi ya Yuda na Yerusalemu iliyozungushiwa ngome.

21Kwa kuwa mfalme wa Babeli sasa amesimama katika njia panda, katika makutano ya njia mbili, akipiga ramli: anapiga kura kwa kutumia mishale, anataka shauri kwa sanamu zake, anachunguza maini ya wanyama.

22Upande wake wa kuume inakuja kura ya Yerusalemu, ambapo ataweka magogo ya kubomoa, ili kuamrisha mauaji, kupiga ukelele wa vita, kuweka magogo ya kubomoa dhidi ya malango, kupandisha kilima hadi kuta zako, na kujenga husuru dhidi yako.

23Itakuwa kama kupiga ramli kwa uongo kwa wale watu ambao wameapa kumtii yeye. Lakini mfalme wa Babeli atawakumbusha kuhusu uovu wao na kuwachukua mateka.

24“Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi: ‘Kwa sababu ninyi mmefanya uovu wenu ukumbukwe kwa kuasi waziwazi, mkidhihirisha dhambi zenu katika yale yote mnayoyafanya: kwa kuwa mmefanya hivi, mtachukuliwa mateka.

25“ ‘Ee mtawala kafiri na mwovu wa Israeli, ambaye siku yake imewadia, ambaye wakati wake wa adhabu umefikia kilele chake;

26hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi: Vua kilemba, ondoa taji. Kwa kuwa mambo hayatakuwa vile yalivyokuwa. Aliye mnyonge atakwezwa, na aliyekwezwa atashushwa.

27Mahame! Mahame! Nitaufanya mji kuwa mahame! Hautajengwa upya hadi aje yule aliye mwenye taji kwa haki; huyo ndiye nitakayempa.’

28“Nawe, mwanadamu, tabiri na useme, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi kuhusu Waamoni na matukano yao:

“ ‘Upanga, upanga,

umefutwa kwa ajili ya kuua,

umesuguliwa ili kuangamiza

na unametameta kama miali ya radi!

29Wakati wanatoa maono ya uongo juu yako,

na wanapobashiri uongo juu yako,

upanga utawekwa kwenye shingo

za wapotovu watakaouawa,

wale siku yao imewadia,

wakati wa adhabu yao ya mwisho.

30“ ‘Urudishe upanga kwenye ala yake!

Katika mahali ulipoumbiwa,

katika nchi ya baba zako,

huko nitakuhukumu.

31Nitamwaga ghadhabu yangu juu yako

na kupuliza moto wa hasira yangu dhidi yako;

nitakutia mikononi mwa watu wakatili,

watu stadi katika kuangamiza.

32Mtakuwa kuni za kuwashia moto,

damu yenu itamwagwa katika nchi yenu,

wala hamtakumbukwa tena;

kwa maana Mimi Bwana nimesema.’ ”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.