Ezekieli 7

Ezekieli 7

Mwisho umewadia

1Neno la Bwana likanijia kusema:

2“Mwanadamu, hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi kwa nchi ya Israeli:

“ ‘Mwisho! Mwisho umekuja

juu ya pembe nne za nchi!

3Sasa mwisho umekuja juu yenu,

nami nitamwaga hasira yangu dhidi yenu.

Nitawahukumu sawasawa na matendo yenu

na kuwalipiza kwa ajili ya desturi zenu zote za kuchukiza.

4Sitawaonea huruma

wala kuwarehemu.

Hakika nitawalipiza kwa ajili ya matendo yenu

na desturi za machukizo miongoni mwenu.

Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Bwana .’

5“Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi:

“ ‘Maafa! Maafa ambayo hayajasikiwa!

Tazama, yanakuja!

6Mwisho umewadia!

Mwisho umewadia!

Umejiinua wenyewe dhidi yenu.

Tazama, umewadia!

7Maangamizi yamekuja juu yenu,

ninyi mnaoishi katika nchi.

Wakati umewadia! Siku imekaribia!

Kuna hofu kuu ya ghafula juu ya milima, wala si furaha.

8Ninakaribia kumwaga ghadhabu yangu juu yenu

na kumaliza hasira yangu dhidi yenu.

Nitawahukumu sawasawa na matendo yenu

na kuwalipiza kwa ajili ya desturi zenu zote za machukizo.

9Sitawaonea huruma

wala kuwarehemu.

Nitawalipiza kwa ajili ya matendo yenu

na desturi za machukizo miongoni mwenu.

“ ‘Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Bwana ambaye huwapiga.

10“ ‘Tazama, siku imefika!

Tazama, imewadia!

Maangamizi yamezuka ghafula,

fimbo imechanua,

nayo majivuno yamechipua!

11Jeuri imeinuka

kuwa fimbo ya kuadhibu waovu.

Hakuna hata mmoja wa hao watu atakayeachwa,

hata mmoja wa kundi hilo:

hakuna utajiri wao utabaki,

wala chochote cha thamani.

12Wakati umewadia,

siku imefika.

Mnunuzi na asifurahi

wala muuzaji asihuzunike,

kwa maana ghadhabu iko juu ya kundi lote.

13Muuzaji hatajipatia tena

ardhi aliyoiuza

wakati wote wawili wangali hai.

Kwa kuwa maono kuhusu kundi lote

hayatatanguka.

Kwa sababu ya dhambi zao, hakuna hata mmoja

atakayeokoa maisha yake.

14“ ‘Wajapopiga tarumbeta

na kuweka kila kitu tayari,

hakuna hata mmoja atakayeenda vitani,

kwa maana ghadhabu yangu iko juu ya kundi lote.

15Nje ni upanga,

ndani ni tauni na njaa.

Walio shambani

watakufa kwa upanga,

nao waliomo mjini

njaa na tauni vitawala.

16Wote watakaopona

na kutoroka watakuwa milimani,

wakiomboleza kama hua wa mabondeni,

kila mmoja kwa sababu ya dhambi zake.

17Kila mkono utalegea

na kila goti litakuwa dhaifu kama maji.

18Watavaa gunia

na kufunikwa na hofu.

Nyuso zao zitafunikwa na aibu,

na vichwa vyao vitanyolewa.

19“ ‘Watatupa fedha yao barabarani,

nayo dhahabu yao itakuwa najisi.

Fedha yao na dhahabu yao

havitaweza kuwaokoa

katika siku hiyo ya ghadhabu ya Bwana .

Hawatashibisha njaa yao

au kujaza tumbo zao kwa hiyo fedha wala dhahabu,

kwa sababu imewaponza wajikwae dhambini.

20Walijivunia vito vyao vizuri

na kuvitumia kutengeneza sanamu za machukizo

na vinyago vya upotovu.

Kwa hiyo nitavifanya vitu hivyo kuwa najisi kwao.

21Nitavitia vyote mikononi mwa wageni

kuwa nyara na kuwa vitu vilivyotekwa mikononi mwa watu waovu wa dunia,

nao watavinajisi.

22Nitaugeuza uso wangu mbali nao,

nao waovu wa dunia watapanajisi mahali pangu pa thamani.

Wanyangʼanyi watapaingia

na kupanajisi.

23“ ‘Andaa minyororo,

kwa sababu nchi imejaa umwagaji wa damu

na mji umejaa udhalimu.

24Nitaleta taifa ovu kuliko yote

kumiliki nyumba zao.

Nitakomesha kiburi cha wenye nguvu

na mahali pao patakatifu patatiwa unajisi.

25Hofu ya ghafula itakapokuja,

watatafuta amani, lakini haitapatikana.

26Maafa juu ya maafa yatakuja,

tetesi ya mabaya juu ya tetesi ya mabaya.

Watajitahidi kupata maono kutoka kwa nabii;

mafundisho ya sheria toka kwa kuhani yatapotea,

vivyo hivyo shauri kutoka kwa wazee.

27Mfalme ataomboleza,

mwana wa mfalme atavikwa kukata tamaa,

nayo mikono ya watu wa nchi itatetemeka.

Nitawaadhibu kulingana na matendo yao,

na kwa kanuni zao wenyewe nitawahukumu.

“ ‘Ndipo watajua kwamba Mimi ndimi Bwana .’ ”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.