The chat will start when you send the first message.
1Katika mwaka wa sita, siku ya tano ya mwezi wa sita, nilipokuwa nimeketi katika nyumba yangu na wazee wa Yuda wakiwa wameketi mbele yangu, mkono wa Bwana Mwenyezi ulikuja juu yangu.
2Nikatazama, nikaona umbo mfano wa mwanadamu. Kutokana na kile kilichoonekana kuwa kiuno chake kuelekea chini alifanana na moto. Kuanzia kiuno kuelekea juu sura yake ilingʼaa vile chuma kingʼaavyo kikiwa ndani ya moto.
3Akanyoosha kitu kilichofanana na mkono, akaniinua kwa kushika nywele za kichwa changu. Roho akaniinua juu kati ya nchi na mbingu, na nikiwa katika maono ya Mungu, akanichukua hadi Yerusalemu, kwenye ingilio la lango la kaskazini mwa ukumbi wa ndani, mahali iliposimama ile sanamu inayochochea wivu.
4Tazama! Palikuwa na utukufu wa Mungu wa Israeli, kama utukufu ule niliouona katika maono kule kwenye nchi tambarare.
5Kisha akaniambia, “Mwanadamu, tazama kuelekea kaskazini.” Hivyo nikatazama na kwenye ingilio la kaskazini mwa lango la madhabahu, nikaona sanamu hii ya wivu.
6Ndipo akaniambia, “Mwanadamu, je, unaona yale wanayoyafanya: mambo ya kuchukiza kabisa ambayo nyumba ya Israeli wanayatenda hapa, yatakayonifanya niende mbali na mahali pangu patakatifu? Lakini utayaona mambo yanayochukiza hata zaidi.”
7Kisha akanileta hadi ingilio la ukumbi. Nikatazama, nami nikaona tundu ukutani.
8Akaniambia, “Mwanadamu, sasa toboa ukuta huu.” Ndipo nikatoboa ule ukuta, nikaona hapo pana mlango.
9Naye akaniambia, “Ingia ndani, ukaone maovu na machukizo wanayofanya humu.”
10Hivyo nikaingia ndani na kutazama. Nikaona kuta zote zimechorwa aina mbalimbali ya viumbe vinavyotambaa, na wanyama wanaochukiza, na sanamu zote za nyumba ya Israeli.
11Mbele ya hizo kuta walisimama wazee sabini wa nyumba ya Israeli, naye Yaazania mwana wa Shafani alikuwa amesimama miongoni mwao. Kila mmoja alikuwa na chetezo mkononi, na moshi wa harufu nzuri ya uvumba ulikuwa unapanda juu.
12Akaniambia, “Mwanadamu, umeona wanayoyafanya wazee wa Israeli wakiwa gizani, kila mmoja kwenye mahali pa ibada pa sanamu yake? Wao husema, ‘Bwana hatuoni, Bwana ameiacha nchi.’ ”
13Akasema tena, “Utawaona wakifanya mambo yaliyo chukizo zaidi.”
14Ndipo akanileta kwenye ingilio la lango la kaskazini la nyumba ya Bwana , nami nikaona wanawake wameketi hapo, wakimwombolezea Tamuzi.
15Akaniambia, “Je, mwanadamu, unaliona hili? Utayaona mambo yanayochukiza hata zaidi.”
16Ndipo akanileta hadi kwenye ukumbi wa ndani wa nyumba ya Bwana , na katika ingilio la Hekalu, kati ya baraza na madhabahu, palikuwa na wanaume wapatao ishirini na watano. Walikuwa wamelipa kisogo Hekalu la Bwana na kuelekeza nyuso zao upande wa mashariki, wakilisujudia jua upande wa mashariki.
17Akaniambia, “Je, umeona hili mwanadamu? Je, ni jambo dogo sana kwa nyumba ya Yuda kufanya machukizo wanayoyafanya hapa? Je, ni lazima pia waijaze nchi dhuluma na kuendelea siku zote kunikasirisha? Watazame wanavyonibania pua kana kwamba ninanuka!
18Kwa hiyo nitawaadhibu kwa hasira; sitawaonea huruma wala kuwarehemu. Hata wakipiga makelele masikioni mwangu, sitawasikiliza.”